JUMATANO
WIKI YA 15 YA MWAKA-C
Somo: Isa 10:5-7, 13-16
Zab: 94:5-6, 7-8, 9-10, 14-15
Injili: Mt 11:25-27
Nukuu:
“Nitamtuma
juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu,
ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani,” Isa
10:6
“Je! Shoka lijisifu juu yake
alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake
auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo
ingemwinua yeye ambaye si mti,” Isa 10:15
“Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo
haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga,” Mt 11:25
“Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye
Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana
apenda kumfunulia,” Mt 11:27
TAFAKARI: “Bwana
hatawatupa watu wake wanyenyekevu na wanyofu wa moyo.”
Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu anapokumbana
na sintofahamu nyingi katika maisha yake, na kukosa mwanga na matumaini kwa
kile akitazamiacho, huishia kukosa maana ya maisha ya maisha yale anayoyaishi.
Pigana ya mwanadamu kila siku ni kuwa mahali pazuri zaidi na penye maana zaidi.
Mwanadamu huyu ukosa mwelekeo na matumaini pale ambapo licha ya jitihada zake
azifanyazo katika usahihi wake anashindwa kujikwamua. Je, tatizo lipo wapi?
Kama tatizo halipo kwake binafsi, basi tatizo hilo lipo kwenye mfumo wa maisha
anayoishi katika jamii husika. Hapa ndipo tunapoona dhambi ya jamii-‘social
sin,’ au uovu katika jamii unavyokuwa sababu ya wengi kuteseka na kukata tamaa.
Je, Mungu anaruhusu haya?
Ni vyema nikajua jambo hili kwamba, Mungu
kaniumba kwa sura na mfano wake, na ndani yangu kanipa uhuru na utashi wa kupembua
katika kujua lililo jema na baya. Hivyo ninavyoshindwa kutumia mizania hii
vizuri, kifuatacho katika ubaya wake hujulikana kama ‘uovu wa kimaadili’ kwa
sababu ni tokeo la kutokutumia uhuru na utashi wangu vyema. Hapa ndugu yangu,
Mungu hausiki kabisaaa.
Ila tulitazamapo somo letu la leo tunaweza
kuona kwa kiasi fulani Mungu huweza kuruhu lililo ovu ili mwisho wa suku liwe
tunda la wema na mafaa. Mungu huweza kutumia njia hii kama tiba kwa mtu au
jamii, somo kwa mtu au jamii hasa pale mtu au jamii inapokengeuka. Katika
mazingira kama haya, agizo la Mungu huwa kama ifuatavyo; “Nitamtuma (mtu au hali fulani katika maana ya kuruhusu) juu
ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke
nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani,” Isa 10:6. Hapa Mungu anatumia tendo hili kama tiba na somo
ili watu wajue uovu na sababu ya kuteseka kwao na mwisho wairudie njia ya
kweli. Mungu analifanya hili, au kuruhusu jambo hili akijua na akiwa malengo
chanya. Naye anasema, “Kwa nguvu za
mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara;
nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu
ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa,” Isa 10:13. Hivyo kwa upande wangu na wewe
ni hatari sana kufanya vitu kwa mazoea au ushabiki. Madhara yake kwa mtu mmoja
au jamii ni makubwa sana.
Na hapa ndipo tunapoongelea juu ya upumbavu wa mtu au watu,
na mwisho wa siku kinakuwa kilio cha wengi katika wingi wao (wapumbavu), na
wachache katika uchache wao (walio simama katika kweli na haki). Je, Mungu katika uchache wa hawa waliosimama
katika kweli na haki, na wakazidiwa na kundi kubwa la wapumbavu waliotumia
vibaya uhuru na utashi wao kwa ushabiki, atakaa kimya? La hasha! “Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala
hutauacha urithi wake, Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa
moyo wataifuata,” Zab 94:14-15. Ukweli ni kwamba, ‘uovu hauwezi kudumu katika
umilele kwa sababu hauna asili hiyo ya milele.’ Hivyo uovu kamwe hauwezi kujisifu
kwa sababu hauna pa simimamia. Ila mtu mwenye kusimama katika kweli na haki
anamahali pakusimamia kwa sababu kweli na haki hiyo ina umilele ambao ndiyo
sifa ya Mungu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Je!
Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye?
Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye
ambaye si mti,” Isa 10:15. Kumbe hakuna sababu ya kukata tamaa ikiwa umesimama
katika kweli na haki, licha ya kuzungukwa na tufani la uovu na wasioona tena
kweli na haki kwani hali hiyo (ovu) haina umilele. “Kwa
hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na
badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto,” Isa
10:16. Tena kumbe hakuna sababu ya kukata tamaa pale mtu anapojiinua kwa uovu
na wakati mwingine akijilinganisha na kujifananisha na Mungu. Mtu huyo au
mazingira hayo ‘ovu’ ni ya leo na kesho tu. Hivyo,
‘Bwana hatawatupa watu wake wanyenyekevu na wanyofu wa moyo.’
Wapendwa
wana wa Mungu, tuitazamapo historia ya wokovu wetu, tunagundua kwamba Mungu
hufanya kazi na wale wajishushao na wanyenyekevu wa Moyo. Licha ya tabia na
mwono huu wa Kimungu, wale wate wanoshirikishwa mpango wa Mungu katika tendo la
Kimungu, huwa ni watu wa kawaida sana, na mara nyingine huwa wale
waliodharaulika na jamii husika. Mama Bikira Maria ni mmoja wa wale
walioshiriki mambo makuu ya Mungu katika unyonge na unyenyekevu wake. Naye
Bikira Maria analitambua jambo hili na kusema, “Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita
mbarikiwa,” Lk 1:48. Bikira Maria
anatambua pia kile kinachotendeka kwake ni upendeleo wa Mungu ndani mwake, na
hivyo kinamakusudi makubwa kadiri ilivyompendeza Mungu. Naye anasema, “Amewaangusha wakuu katika
viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Mama Bikira Maria
anayasema haya toka ndani ya mtima wake, na anamaanisha vivyo. Bikira Maria
hayasema haya ili apate huruma kwa watu au ya watu. La hasha! Bikira Maria
anayasema haya mambo mazito akitazama kuinuliwa kwake kusiko mastahili yake
binafsi bali kwa kujinyenyekesha kwake, na hasa upendeleo aliopewa na Mungu wa
kushiriki fumbo hili la wokovu wa mwanadamu. Hakika, Mama Bikira Maria kama
mwanadamu ni mfano halisi wa yeyote yule mwenye kupewa dhama na umma wa watu.
Kujishusha huku na kuwa
wanyenyekevu mbele ya Mungu mwenye kuyaweza yote, ndiko kunakotutafakarisha
maneno na sala hii ya Yesu katika Injili ya leo: “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi,
kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto
wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako,” Mt
11:25-26. Je, twatoa shukrani kwa Mungu hata kwa kile kidogo Mungu
alichotuwezesha kukifanya? Je, mafanikio niyapatayo natambua ni mkono wa Mungu,
au ni akili zangu na ujanja wangu? Ndugu yangu, ‘moyo usio na shukrani hukausha
mema yote.’
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nimekabidhiwa
vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye
Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Mt 11:27
Tusali:-Ee Yesu na
Mwalimu wangu, nipe macho na moyo wa unyenyekevu wa kuona yote niyafanyayo si
kwa akili zangu tu, bali neema ile itokayo kwako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario