JUMAPILI YA 16 YA MWAKA-C
Somo
I: Mwa 18:1-10a
Zab: 15:2-3, 3-4, 5
Somo
II: Kol 1:24-28
Injili:
Lk 10:38-42
Nukuu:
“Bwana
wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa
wako,” Mwa 18:3
“Akamwambia,
Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana
wa kiume,” Mwa 18:10a
“Sasa
nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili
wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani,
kanisa lake,” Kol 1:24
“sisi tunamhubiri habari
zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate
kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo,” Kol 1:28
“Lakini
Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana,
huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie
anisaidie,” Lk 10:40
“lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua
fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42
TAFAKARI:
“Kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
bila shaka si mgeni wa neno hili ‘ukarimu.’ Mtume Paulo anatupa maana halisi ya
neno ukarimu. “Lakini
nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa
ukarimu. Kila mtu na atende kama
alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu
humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” 2Kor 9:6-7. Ni kwa maana hii
Ukarimu ujeuka kuwa baraka kwani ndivyo Mungu apendavyo tufanye.
Ibrahimu anabarikiwa na
kuhaidiwa kutokana na ukarimu wake. Anapowaona wageni wale watatu, anawahudumia
bila kujibakiza, Mwa 18:5-8. Naye anasema, Bwana
wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa
wako,” Mwa 18:3. Maneno haya; “usinipite sasa mimi mtumwa wako,” yanaelezea ni
kwa kiasi gani Ibrahimu alivyo yaweka matumaini yake yote kwa Mungu kwa kile
alichokuwa anakitamani, yaani, kuwa na Mtoto. Wageni hawa watatu ni fumbo zima
la UTATU MTAKATIFU, Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Huu ni ugeni mkubwa
sana. Tupatapo mgeni au wageni, yatupasa kuwahudumia kama walivyo kadiri ya
kile wanachohitaji wakati ule. Tulifanye jambo hili bila kuwa na upendeleo au
utofauti wa kulifanya kutoka na mwono wa yule tuleyekutana naye kama mgeni.
Ibrahimu anajitoa bila kujibakiza kwa hali na mali alizokuwa nazo.
Ukarimu
ni uwepo wa kimungu ndani yetu. Unapofanya tendo la ukarimu unaakisi uwepo wa
Mungu ndani yako. Mungu ni MKARIMU! Tunapowakarimia wenzetu wenye mahitaji
mbalimbali twafanya tendo la Kimungu, na tendo hilo Mungu usimama hapo. Mungu
hutujibu mara moja tulifanyapo tendo hili bila kujibakiza. “Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa
maskini chakula chake,” Mit 22:9. Ibrahimu
anapewa hakikisho hilo na baraka hizo mbele ya Mungu. Naye “Akamwambia,
Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana
wa kiume,” Mwa 18:10a. Ndugu yangu, unapomkarimu mtu usiangalie alikotoka,
undugu uliokua nao naye, ukabila wako naye, ukanda wenu, na hata utaifa wenu.
Yatupasa kulenga kwenye hitaji la mtu husika, na tulifanye jambo hilo bila
kujibakiza.
Ni
ukweli usiotia shaka kwamba kadiri ya mtazamo wetu wa kibinadamu, na hali
tuliyonayo kibailoogia-elimu viumbe, ni vigumu kuamini kutendeka kwa yale
ambayo kiualisia yeshapitwa na wakati wake. Hatuwezi kutegemea mwanamke mwenye
umri mkubwa na hasa katika uzee wake kuwepo uwezekano wa kumpata mtoto.
Maandiko Matakatifu yanatuambia kwamba Sara alikwisha fikia kikomo katika
desturi ya wanawake. Habari kama hii inakuwa kichekesho kwa Ibrahimu ambaye
alikuwa na umri wa miaka mia, Mwa 17:17. Hapa ilimaanisha kwamba kwa hali ya
kawaida, ilikuwa vigumu kupata mtoto. Hivyo jambo hili kwa Sara mwenye umri wa
miaka tisini ni kama kichekesho fulani. “Kwa
hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na
bwana wangu mzee?” Mwa 18:12. Pamoja na
kihoja hiki, Mungu anasimama na kuonyesha Ukuu na Umungu wake pale mitazamo
yetu, desturi zetu, na uwezo wa akili zetu unapofikia kikomo chake. Huyu ndiye
Mungu!
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu siyo wa kushindwa hata mara moja. Mungu wetu ni mweza wa mambo yote,
na huyafanya mambo hayo si tu kwa kuonyesha Ukuu wake, bali ndivyo ilivyo asili
yake. Kama yeye ndiye mwanzo na mwisho-‘alfa na omego’ ni kitu gani chini ya jua
kitamshinda? Kama uwepo wetu leo na sasa ni kwa sababu yake, je, atashindwaje
kuyarekebisha maisha na mfumo wetu? Hivyo Mungu anasimama katika ukweli huu na
kumwambia Ibrahimu, “Mbona
Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda
Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata
mwana wa kiume,” Mwa 18:13-14. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Tunapoitafakari
habari hii ya Ibrahimu na mkewe Sara inatupelea karibu zaidi kuelewa maneno
haya ya Yesu kwa Martha, kwamba, “Martha,
Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na
Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42. Kitu
hicho ni ‘kujisalimisha’ moja kwa moja bila kujibakiza katika mikono sala ya
Mungu.
Biblia
iko wazi kabisa kuhusu unavyoweza kufaidika unapojisalimisha kikamilifu kwa
Mungu. Kwanza, unapata amani: “Acha kugombana na Mungu! Ukikubaliana naye,
utapata amani hatimaye, na mambo yatakunyookea.” Ayu 22:21. Pili, unapata
uhuru: “jitoeni nafsi zenu kuzifuata njia za Mungu na uhuru hautatoka
kamwe….Amri zake zinawaweka huru kuishi kwa uwazi katika uhuru wake!” Rum. 6:17
Tatu,
unapata nguvu za Mungu katika maisha yako. Majaribu makali na matatizo mazito
yanaweza kushindwa na Kristo kama atakabidhiwa. Joshua alipoviendea vita vile
vikubwa maishani mwake, Yosh. 5:13-15 alikutana na Mungu, akamsujudia, na
akasalimisha mipango yake. Kujisalimisha huko kulileta ushindi mkubwa pale
Yeriko.
Hiki
ni kitendawili: Ushindi huja kwa kujisalimisha, kujisalimisha hakukudhoofishi
wewe; kunakutia nguvu. Jisalimishe kwa Mungu, hauhitaji kuogopa au
kujisalimisha kwa chochote kile. William Booth, wanzilishi wa Jeshi la wokovu,
alisema, “ukuu wa nguvu za ubinadamu unapimwa kwa kiwango chake cha
kujisalimisha.”
Watu
waliojisalimisha ndio Mungu anaowatumia. Mungu alimchagua Mariamu kuwa mama wa
Yesu, siyo wa sababu alikuwa na kipawa, au utajiri au uzuri wa umbile, lakini
kwa sababu alikuwa amejitoa kikamilifu kwake. Malaika wa Bwana alipomwelezea
mpango mgumu wa Mungu, alijibu kwa upole, “mimi ni mjakazi wa Bwana, na niko
tayari kupokea chochote anachotaka.”Lk. 1:38 Hakuna kitu kikubwa kama maisha ya
kujisalimisha katika mikono ya Mungu. “Hivyo zikabidhini nafsi zenu kikamilifu katika
mikono ya Mungu.” Yak. 4:7a
Katika
somo la Injili ya leo, Mariamu ndugu yake Martha anajielewa na kumfahamu yule
anayemtumikia aliye kweli katika yote, na mwisho anajisalimisha kwake.
Yawezekana mimi na wewe tumeyapa maisha yetu kipaumbele chake cha kwanza katika
kujishughulisha katika mambo mengi yasiyo na mwelekeo. Maisha yetu hayajengwi
kwa wingi wa vitu tunavyofanya, bali uelewa wa yale tunayoyafanya, na kwa nini
tunafanya kama tunavyoyafanya. Martha kama tulivyo wengi, anajilinganisha na
yale anayofanya na kukosa muda wa kujua chanzo ya yale yote anayoyafanya na kwa
nini anayafanya kwa namna hiyo, na ni nani anayeyaratibisha. Martha
anamlalamikia Yesu kwa nini Mariamu ndugu yake hamsaidii. Yesu anamkumbusha
Martha jambo la muhimu na kusema, “Martha,
Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi,” Lk 10:41. Furaha
yetu haitokani na wingi wa vitu tuvifanyavyo. Tuyafanyayo yakikosa sababu na
malengo yake husika, ni wazi kwayo kama yalivyo hayawezi kuwa sababu ya furaha
yetu. Kujishughulisha huku katika maana ya kufanya hivyo tu, kutakuletea
mfadhaiko mkubwa sana pale mambo hayo yatakapo kwenda ndivyo sivyo.
Maisha
yetu yana maana kwanza kabisa tunapojitambua na mwisho kujisalimisha muda wote
kwa Yule aliye sababu ya ishi yetu na atupaye uzima wa milele. Huyu ndiye
chanzo cha furaha yetu na umilele wa maisha yetu. Kwake yatupasa kutumia muda
mwingi naye. Huyu ndiye Kristo; njia, ukweli, na uzima wetu, Yoh 14:6. Kuwa na Kristo
ni kuchagua fungu lililo jema ambalo kwalo hatuwezi ondolewa. Ukweli huu ndio
Yesu anaomwambia Martha na sisi leo kwamba pamoja na yote tuyafanyayo, “lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:42. Kukaa chini ya
miguu ya Yesu ni ule utayari wa kulishwa neno la uzima, na kujazwa ufahamu na
kufunuliwa siri ya uzima wa milele.
Kujisalimisha
ndani na katika Kristo Yesu hukupa maana ya maisha yako. Mtume Paulo
anathibitisha kweli hiyo kwa kusema, “Sasa
nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili
wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa
lake,” Kol 1:24. Kristo ndiye uzima ule
uupiganiao kila siku. Na hii ndiyo siri iliyofIchwa kwa wamchao Mungu, yaani
Watakatifu wake. Ni “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote
na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake,” Kol 1:26. Na
kwa siri hii, Mtume Paulo amefanywa ‘mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa
Mungu, aliyopewa kwa faida watu, akilitimize neno la Mungu,’ Kol 1:25. Ndugu
yangu, Kristo ndiyo njia ile sahihi
unayoitafuta kila siku na mara nyingine kupotea kabisa. Na Kristo ndiye kweli
yenyewe kwa sababu ndiye ufunuo wa kweli ya Mungu Baba. Ni katika kweli hii “ambayo
Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa Utukufu wa siri hii katika
Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la Utukufu,” Kol 1:27. Kumbe wito
wako na wangu kama wabatizwa na wafuasi wa Kristo walio hai kama asemavyo Mtume
Paulo ni “kuhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha
kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo,”
Kol 1:28. Na huu ndio ushuhuda wa kweli.
Wapendwa wana wa Mungu,
hatutaweza kutoa ushuhuda huu wa Mungu kama hatupo tayari kulishirikisha kwa
ukarimu neno la Mungu. Ushirikishaji huu wa Neno la Mungu kwa ukarimu tumeona
leo ukifanyika kwa vitendo kutoka kwa Ibrahimu kwa wale watu watatu wageni,
kutoka kwa Mariamu kwa kujisalimisha chini ya miguu ya Yesu, na kutoka kwa
Mtume Paulo kwa kujitoa bila kujibakiza kwa Kanisa la Kristo na watu wake. Hata
hivyo tutaweza tu kulishirikisha neno la Mungu kwa ukarimu kama tutaweza
kulitafakari kwa kina Neno la Mungu. Kulitafakari kwa kina neno la Mungu
kunahitaji utayari bila shuruti wa kulipokea Neno la Mungu. Na tutaweza
kulipokea Neno la Mungu bila shuruti pale tu tutakapokuwa tayari kulisikia Neno
la Mungu.
Familia ya Mzee Rajabu
inatoka Kigango cha Kona Mbili. Familia hii ni ya kawaida kabisa lakini
iliyojaa upendo na hofu ya Mungu. Kigango cha Kona Mbili kilikuwa na adhimisho
la mwezi mzima kuutembeza Msalaba Mtakatifu.
Maandamano haya ya Msalaba Mtakatifu kila siku yalianza majira ya saa
tisa alasiri ili kuwapa nafasi hata wale waliokuwa wameajiriwa kushiriki zoezi
hili Takatifu. Na ilipofika saa mbili usiku Msalaba ulikesha kwenye mji wa
mwaamini yeyote aliyetayari kufanya hivyo. Watu waliweza tena kupata nafasi ya
kusali, kutafakari Neno la Mungu, na kuimba usiku kucha.
Siku moja ya alhamisi
ilipofika saa mbili usiku ikiwa ni karibu na Familia ya Mzee Rajabu ambaye
alikuwa safarini kwa siku saba, na siku hiyo ndiyo alikuwa ana rudi nyumbani,
kulikuwa na ‘ukimya’ mkuwa wa nani atakaye uchukuwa Msalaba ule ukalale kwake
hadi kesho. Hofu haikuwa kuuogopa Msalaba Mtakatifu, bali ni utayari katika
maana ya ‘ukarimu wa wana familia’ husika kwa usiku ule ikiwa ni pamoja na
kuwapatia watu maji na chai. Ndipo bila kusita Mke wa Mzee Rajabu aliomba
Msalaba ule ulale kwenye familia yao. Kwenye mkusanyiko ule wa watu, wengine
walisikia wakiguna kwa sababu waliijua familia ile katika umasikini wao. Hata
hivyo wanafamilia ile wengine waliwahi nyumbani haraka na kuandaa mazingira ya
watu kukaa na sehemu ya kuuweka Msalaba ule hadi asubuhi.
Kasukari kalichokuwepo
chote kalitumia, na ajabu wote waliokuwa nyumbani pale walipata chai. Na
ilipofika saa nne za usiku, Mzee Rajabu aliingia na boda boda akiwa na
vifurushi vyake vya heshima. Mzee Rajabu akiwa anashangaa umati wa watu
nyumbani mwake wakiimba kwa furaha, Mke wake alipigwa na butwaa kuona mme wake kuja
na mfuko wa sukari wa kilo 25. Haikuwahi
kutokea katika familia hiyo. Mambo yalienda vizuri hadi asubuhi. Watu
walifurahi sana na kila mtu alisema yake.
Ndipo Mama Rajabu
alipotaka kujua ukweli wa ile Sukari kutoka kwa mme wake. “Hata mimi sijui nikuambiaje
mke wangu. Kwa ufupi ni kwamba nilikutana na Mtani wangu ambaye tulikuwa
tunafanya kazi kampuni moja na sasa yupo kampuni moja ya usafirishaji wa
Sukari. Kwa furaha aliyokuwa nayo kwa jinsi nilivyomsaidia kwenye msiba wa
mwanaye, akanipa sukari hiyo na kuniambia ‘ndugu yangu na Mtani wangu, kapate
chai na watoto wangu,’ na nasema asante kwa ukarimu wako. Hivyo ndivyo
ilivyokuwa. Maajabu!” Kwa furaha mke wake akamjibu, “Kwa kweli ni maajabu, sifa
na shukrani kwake yeye ajuaye maisha yetu. Amina.”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Siri
ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa
kwa watakatifu wake,” Kol 1:26
Tusali:-Ee
Yesu tukirimie moyo wa utayari na ukarimu kujitoa bila kujibakiza na hasa
tunapojisalimisha kwako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario