IJUMAA WIKI YA 17 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 26:1-9
Zab: 69:5, 8-10, 14
Injili: Mt 13:54-58
Nukuu:
“Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana,
useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao
maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja,” Yer 26:2
“Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia,
kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu, kuyasikiliza maneno ya watumishi
wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini
ninyi hamkuwasikiliza; basi,
nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa
taifa zote za dunia,” Yer 26:4-6
“Na alipofika
nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu
amepata wapi hekima hii na miujiza hii?” Mt 13:54
“Huyu
si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na
Yusufu, na Simoni, na Yuda?” Mt 13:55
“Na
maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?” Mt 13:56
“Wakachukizwa
naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake,
na nyumbani mwake mwenyewe,” Mt 13:57
TAFAKARI:
“Je, tuache kutenda mema? Tutende mema kwa sababu wema ni uhasilia wa Mungu
mwenyewe.”
Wapendwa
wana wa Mungu, vile vyote vilivyotumika kuwakilisha Ukuu na Umungu wa Mungu
havikuwa vya ajabu sana wala kustaajabisha sana. Mungu hupenda kutumia watu na
mazingira ya kawaida kuufikisha ujumbe wake. Jambo la maana na muhimu lipo
katika ‘ufahamu na umaana’ wa kile kisemwacho na chenye uhusino na Mungu.
Mfano; Mama Bikira Maria alikuwa Binti na Bikira kama walivyokuwa mabinti
wengine katika jamii ile ya Kiyahudi. Ila, Mungu alipenda na ilimpendeza
kumchagua Mama Bikira Maria kumshirikisha katika ukombozi wa mwanadamu na
kuinua kile kilichoanguka kutoka kwa wazazi wetu wa mwanzo, yaani, Hawa na
Adamu. Ni kwa namna hiyo hiyo, Mungu aliweza kuwachagua watu wa kawaida kutoka
jamii husika ili kuufikisha ujumbe wake. Na ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii
Yeremia. Na mambo yalikuwa kama hivi; “Mwanzo
wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili
lilitoka kwa Bwana, kusema, Simama
katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu
katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie
hata neno moja,” Yer 26:1-2. Bila shaka wapo wakupuuza na wapo wa kutilia
maanani. Mara nyingi katika ubinadamu wetu tunatazama yule atoaye ujumbe, na sio
uzito wa ujumbe ule utolewao.
Ukitaka
kujua ukweli huu, chunguza jumuiya zetu za Kikristo. Wakati mwingine wale wenye
nazo, yaani, ushawishi wa pesa na mali, usikilizwa zaidi kuliko akina kapuku
kama mimi. Tunaporuhusu hali hii, Mungu ujitenga nasi hadi pale tutakapojirudi.
Akiijua hali hiyo, Mungu anamsihi Nabii Yeremia na kusema, “Labda
watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi
mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao,” Yer 26:3.
Ndugu yangu, chochote kile ukisikiacho chenye kubeba uzima wako na umilele
wako, tafakari ujumbe ule katika ‘ufahamu wake na umaana’ wake, na siyo mtoa
ujumbe, ingawa kufanya hivyo siyo mbaya. Na
ujumbe wa Mungu ni huu; “Nawe
utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria
yangu, niliyoiweka mbele yenu, kuyasikiliza
maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema
na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza; basi,
nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa
taifa zote za dunia,” Yer 26:4-6. Ndugu
yangu, ujumbe wa Mungu waweza kuwa wa kutia moyo, kuonya, kufundisha, na
kufurahisha. Kinachotakiwa ni kuufanyia kazi ujumbe huo. Ila mara nyingi mambo
hayawi hivyo.
Kwa ujumbe huu Nabii
Yeremia anakuwa hatiani. “Ikawa,
Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote Bwana aliyomwamuru kuwaambia
watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema,
Bila shaka utakufa,” Yer 26:8. Hili lililomkuta Yeremia silo geni katika
mazingira yetu tata ya siasa zetu zisizo na mwelekeo na zilizojaa ubinafsi.
Wale wote wasiotaka maslahi yao kuguswa hawatakaa kimya. Watatafuta kila njia
kuhalalisha uovu wao na kukutia hatiani. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Nabii
Yeremia, nao wakamuohoji na kusema, “Kwa
nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na
mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia
katika nyumba ya Bwana,” Yer 26:9. Ndugu yangu, pamoja na utata huu, lililo
kweli na lisemwe katika kweli na haki. Hii njia pekee ya kuushinda uovu, tena
ule unao sababishwa na uhuru na utashi wetu kama binadamu. Kama hili linatokea
leo kwako kupata upinzani katika kweli na haki, wewe sio mtu wa kwanza, kwani
hata Kristo alikumbana na hali hiyo hiyo. Kristo kwa wakati na jamii yake,
alikuwa ishara ya utata na changamoto ya Imani. Na hili ndilo linalohusu Injili
yetu la leo.
Wapendwa
wana wa Mungu, ukaribu wa binadamu na Muumba wake hujidhihirisha katika tendo
la kuabudu na kujisalimisha kwa mwanadamu huyu kuliko kwa pekee na kwa namna ya
juu kabisa. Tendo hili la kiibada huthibitisha udogo wa mwanadamu na ukuu wa
Muumba wake. Kwa ufahamu huu, hakuna njia iliyo bora zaidi ya kujisalimisha
yenye kuonyesha ukaribu huu kati ya kiumbe na Muumba nje ya tendo la kuabudu.
Ndugu
unayesafiri nami katika tafakari hii, ni vyema tukaona na kuzama katika neno
hili: “Yesu Kristo ishara ya utata na changamoto ya Imani yetu.” Hatuwezi
kuelewa vizuri historia ya wokovu wetu na sababu ya umilele wetu nje na ndani
ya Kristo katika maana ya mwanzo na ukamilifu wa historia hii ya wokovu. Mwanzo
wa safari hii, Yesu Kristo anasimama katika mizania ya NENO. “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1. Kwa
maana hii, hakuna jambo lolote lile tulionalo leo kwa namna lilivyo pasipo
Kristo katika uhasilia wake.
“Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,”
Yoh 1:3. Na ndivyo ilivyo pia katika ukamilifu wa historia hii ya wokovu,
Kristo anasimama kama kielelezo na umilele wa kitu hicho. “Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14.
Ni katika
msingi huu Yesu Kristo ni ishara ya utata na changamoto ya Imani yetu. Utata
uliopo katika fumbo hili la wokovu ni ukweli ulio wazi juu ya mianzo na miisho
ya vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. “Kwa kuwa katika utimilifu
wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa
mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:16-17.
Pamoja na
hayo yote niliyoyaelezea hapo juu, uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila
siku unatutaka kwenda juu zaidi tunapotazama mwanzo wa historia ya wokovu watu,
na ukamilisho wake ambao kwa vyote viwili Kristo ndiye msingi wa vyote. Hivyo
kwa maana nyingine hapakuwa na sababu kubwa na yaajabu kustaajabia yale
aliyokuwa anayafanya Yesu kama Wayahudi wangefikiria fumbo hili la wokovu
katika upana wake. Tatizo kubwa walilokuwa nalo Wayahudi na hata sisi pia
katika changamoto ya Imani yetu, tunaubeba zaidi ubinadamu wetu na kuufanya
miwani ya kutazamia Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tufanyapo tendo hili,
hatuwezi kuepuka utata katika Kristo. Nasi tutabakia katika hatua hii ya chini
kabisa na kujiuliza kama Wayahudi: “Huyu si mwana wa
seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na
Simoni, na Yuda?” Mt 13:55. Ni kweli kwamba
hatuwezi kuepuka ubinadamu wetu, ila yatupasa kuushinda ubinadamu wetu siku kwa
siku kadiri tunavyokua kiimani.
Ni ukweli pia usiotia
shaka kwamba tusipoushinda ubinadamu wetu lazima tutachukizwa na yale
ayatendayo Kristo ndani na katika mazingira yetu. Wayahudi “wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima,
isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe,” Mt 13:57. Ndugu yangu,
yaliyomkuta Yesu hasa katika safari hii ya ukamilifu na umilele wa wokovu wetu,
hutupata pia sisi pale tunafuata nyayo zake Kristo kwa ukamilifu. Kwetu nasi
tutabakia kuwa “ishara ya Utata na Changamoto katika Imani,” ndani na katika
Kristo.
Ndugu yangu, ukweli ni
kwamba, ukifanya mema utasemwa vibaya, na ukifanya vibaya utasemwa pia. Je,
tuache kutenda mema? Tuendelee kufanya mema na kuyatenda mema hayo si kwa
kutazamwa na watu. Tunafanya mema kwa sababu wema ni uhasilia wa Mungu
mwenyewe, na kutenda jema ni kutenda linalompendeza Mungu lipendwe au
likataliwe machoni mwa Mungu halipotezi uhalali wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi
kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe,” Mt
13:57
Tusali:- Ee Yesu na Mkombozi wetu, tupe ujasiri wa kupambana na ouvu pasipo
woga. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario