domingo, 3 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 14 YA MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 14 YA MWAKA-C
Somo: Hos 8:4-7, 11-13
Zab: 115: 3-4, 5-6, 7-8, 9-10
Injili: Mt 9:32-38
Nukuu:
Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali,” Hos 8:4 

 “Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza,” Hos 8:7 

 “Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache,” Mt 9:37

“Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Mt 9:38

TAFAKARI: “Nia ovu haziwezi kuhalalisha lengo jema. Mungu hafananishwi na uovu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ‘nia ovu haiwezi kamwe kusadifu lengo jema. Mungu wetu hafananishwi na uovu.’ Bila shaka kwa matakwa na matarajio yetu binafsi na kwa makundi yetu kiitikadi tungependa kumchonga Mungu kama tunavyotaka awe. Ila ukweli ni kwamba, hatuwezi kumbeba Mungu katika mikomo yetu na ubinadamu wetu. Hatuna uwezo huo wa kumshikilia ndani na katika ubinadamu wetu. Aliyetuumba kwa sura na mfano wake anatujua vizuri kuliko sisi tumjuavyo. Tangu lini kwa mfano, mashine ikawa na uwezo kuzidi ya yule aliyeibuni na kuitengeneza? Ni ajabu!

Hivyo kufuru hujijenga pale tunapoyalazimisha yale ambayo hata kwa uwezo wetu na mikomo yetu ni vigumu kufanyika. Huu ndio ujumbe wa Mungu kupitia mtumishi wake Nabii Hosea, Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali,” Hos 8:4. Yote haya yamefanyika ili kukidhi matamanio ya watu, au kundi la watu ambalo halitaki kuukubali ukweli wa mambo kama ulivyo.  Mfano halisi ni huu: Nchi nyingi za Bara letu la Afrika, na Tanzania ikiwepo “huwa tunafanya uchaguzi wa kidemokrasia, kuruhusu uwepo wa vyama vingi, katika maana pia ya kuruhusu uwezekano wa fikra tofauti.”

Lakini jambo la kushangaza ni hili; “licha ya kwamba wengi huchagua fikra tofauti kama njia mbadala ya kwenda pale tunapopatamani kwa sababu na mang’amuzi yatokanayo na historia yetu, wapo wachache na tena wasiozidi wakati mwingine watu watano, wanaopindisha matakwa ya walio wengi.” Mara hili linapotendeka kwa manufaa ya kulinda kundi la watu wachache au historia ya walio na historia mbovu, halina jina lingine zaidi ya UOVU. Kama sauti ya watu ni sauti ya Mungu, hakika Mungu si wa kuchezewa katika mantiki hii. Na hii ndiyo maana ya maneno haya: Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande,” Hos 8:6. Mateso tuyapatayo leo katika jamii siyo kusudi la kweli katika uhasilia wake, bali ni matokeo ya tamaa ya watu wacheche waliopewa dhamana katika kundi kubwa la watu.

Mengi yawezekana kufanyika ili kuzima sauti za walio wengi, bali Mungu hachezewi hata kidogo. Kifuatacho katika uovu huu uliofanywa kwa makusudi maalumu ni anguko kubwa sana. Mtindo wa kulazimisha mambo katika bara letu la Afrika utokanao na wenye uchu wacheche umekuwa sababu ya vifo vingi vya watu wasio na hatia. Damu hizi hazipotei bure! Hakuna yeyote kati yetu aliyeko katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya hadi mwanadamu mwenzake autoe uhai wake kwa sababu tu ya kuyatetea maslahi yake binafsi, au kundi lililomweka hapo alipo na kuwa na mamlaka hayo maovu. Kufanya hivyo ni kupenda upepo na faida yake i waza kama asemavyo Nabii Hosea,  kwamba Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza,” Hos 8:7.

Kama kile tupandacho ndicho tukivunacho, kwa nini basi kutegemea miujiza katika uovu wetu? Yesu anatuambia hivi; Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Je, tutegemee maajabu kwa lile lililo ovu tena kukifanya huku tunajua? Mungu wetu si ‘mdoli’ wa kuchezea! Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Mungu kupitia Mtumishi wake Nabii Hosea kwamba, Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake,” Hos 8:11. Kwa maana nyingine tungesema hivi; “kwa kuwa watawala wa watu wangu Tanzania wameongeza madhababu kwa dhambi, madhababu hizo zimekuwa dhambi kwao.” Huu ni uovu kwa kiimaadili ufanywao na mtu akijua na tena mwenye dhamira chanya.

Wapendwa, kila siku tunaitwa kutenda na kuishi yale yanayompendeza Mungu. Tatizo kubwa katika ukweli huu ni kwamba hatupo tayari kuyafanya hayo. Wazo lolote lenye kutuhitaji kufanya kile kilicho cha pekee katika maisha yetu kinaitaji kujitoa kusipo na kipimo. Pamoja na ukweli kwamba waitwayo ni wengi, ila wanaokubali wito huu ni wachache. Ni wachache katika maana ya kwamba nguvu na akili zetu tuziwekazo katika utume huu hazima majibu ya haraka na mepesi. Ndipo  Yesu alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache,” Mt 9:37. Sote tumeitwa kuwa watendaji wa kazi ya Mungu bia kujibakiza. Hatuwezi kuona makusudia ya Mungu juu ya maisha yetu yanapotea bure.

Hivyo kila siku tunaalikwa kujitoa kwa ajili ya wito Mtakatifu. Kujitoa huku ni kuwa na dhamira chanya ya kuiombea miito mitakatifu. Tusipolifanya jambo hili kwa ukweli na umakini wake, yote hupotea kama moshi. “Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Mt 9:38. Kama wewe ni Padre unayefanya utume wako katika parokia, ni vyema ukayatazama kwa ukaribu makundi haya: Kuwa na wakati ujayo mwema, unapaswa kuwa karibu sana na vijana. Kuyapata mang’amuzi ya wakati uliopita yakupasa kuwa karibu sana na wazee. Kujua mahangaiko ya familia ya kila siku, wewe kama mchungaji na padre yakupasa kuwa karibu sana na wazazi. Kujua furaha ya kweli, wewe kama mchungaji mwema yakupasa kujua furaha ya kweli iliyopo kwa watoto.

Tumsifu Yesu Kristo!

Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si mungu kamwe,” Hos 8:6a


Tusali:- Ee Yesu mwema, tupe nguvu kuushinda uovu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario