JUMAMOSI
WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Yer 7:1-11
Zab: 84:3, 4, 5-6a, 8a, 11
Injili: Mt 13:24-30
Nukuu:
“Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni
njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa,” Yer 7:3
“Msitumainie
maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana
ndiyo haya,” Yer 7:4
“Baadaye majani
ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu,” Mt 13:26
“Viacheni
vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao,
Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano
ikusanyeni ghalani mwangu,” Mt 13:30
TAFAKARI: “Tengenezeni njia zenu, na matendo
yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.”
Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu ya leo,
yanaweka bayana ukweli huu kwamba ‘upendo na huruma ya Mungu vi kwa watu wote.’
Katika kweli hii hakuna ubaguzi wowote ule kwa yeyote yule sababu ikiwa Mungu
ndiye aliyekuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27 iweje basi ajibague
mwenyewe? Hivyo tuzamapo katika hasili na tabia ya Mungu; Upendo, Huruma, Haki,
na Msamaha, tunagundua kwamba mimi na wewe ndio wapinzani wakubwa wa upendo
huo, huruma hiyo, haki hiyo na msamaha huo wa Mungu. Tunayapinga hayo yote kwa
kutokuukubali ubinadamu wetu, na kutaka kuwa kitu kingine. Hicho tupendacho
kuwa kwa uhuru wako hakina chapa ile ya Mungu ndani yako.
Kwa kuukataa ubinadamu wako na kupenda kitu
kingine ambacho kwa hakika siyo asili yako, tendo hilo uzifukuza au kukwamisha
‘neema zote ndani yako.’ Neema hizi ndizo zituwekazo karibu na Mungu muda wote.
Hata pamoja na uasi wako, kwa kutambua kosa hili waweza kuutumia uhuru ule ule
ulioutumia kumwasi Mungu na kujirudi na kumrudia Mungu. Na hili linawezekana
kadiri ya wito wake Mungu kwetu kwamba, “Tengenezeni
njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa,” Yer 7:3.
Ndugu yangu, neno “Mahali hapa,” linabeba tafsiri ya pale ulipo kama mwana
jamii ikiwa ni pamoja na Taifa na utaifa wako. Leo kwa mfano, mimi ni Mtanzania
kwa sababu mahali pangu na hapa ni Tanzania hata kama kwa nyakati fulani
nitakuwa sehemu nyingine au nchi nyingine.
Kumbe kama nipo nje ya kweli na taratibu hiyo niliyoisema,
yanipasa kuitengeneza njia yangu, na matendo yangu, ili Mungu aweze kunikalisha
pale nipaswapo kuwepo. Huku ndiko kujaliwa neema za Mungu, na neema hizo ndizo
zituwezeshazo kuwa karibu na Mungu. Mungu wetu utuwazia yaliyo mema muda wote
kwa sababu mimi na wewe ni tokeo la upendo wake. Ni tunda la upendo wa Mungu. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema
Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za
mwisho,” Yer 29:11. Iwapo mawazo ya Mungu kwetu ni amani na ndivyo ilivyo,
lengo lake ni mimi na wewe tuwe na tumaini la kweli katika maisha yetu. Maisha
yasiyo na tumaini ni sawa na gari lililo kwenye mwendo wa kasi pasipo usukani
licha ya uwepo dereva.
Simama imara yangu na yako leo na sasa iwe katika kweli na
haki. Na hivi ndivyo Mungu anavyotuwasa, kwamba, “Msitumainie
maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana
ndiyo haya,” Yer 7:4. Ni katika kuzitengeneza njia zetu zilizo mbaya na
kusimama katika kweli na haki, Mungu ataonekana kwa wote tunao kutana nao, na
hasa katika maeneo haya, “kama mkihukumu
hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kama
hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia
mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe; ndipo nitakapowakalisha mahali hapa,
katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele,” Yer 7:5-7.
Lakini jambo la kusikitisha leo ni kwamba kila kona uendayo kumejaa ujanja
ujanja, na kufaidiana kuliko kwa upotofu
na uongo mwingi. Mungu asema hivi katika hili, “Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia,”
Yer 7:8. Jamii yenye kusukumwa na tabia za mtindo huu hudumaa kimwili na
kiroho, na hivyo kubaki kuwa ni ndoto kupiga hatua mbele.
Swali kwako na kwangu ni hili; “Je!
Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na
kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua; kisha
mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na
kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?” Yer 7:9-10. Leo kumetokea akina ‘Baali wengi na miungu’ yenye
mifanano hiyo. Akina Baali wetu wa leo ni ‘ung’ang’anizi wa madaraka hata
ikibidi kumwagika damu. Ni utajiri wa kupindukia na wakutokujali haki za watu.
Ni ushirikina uliokidhiri hadi kuhadhiri mfumo mzima wa fikra huru. Ni umaarufu
kwa sababu ya umaarufu tu, na wakati mwingine wengi kulipa gharama yake. Swali
lingine kwangu na kwako pia ni hili; “Je! Nyumba hii (au Taifa hili), iitwayo kwa jina langu,
imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi,
nimeliona jambo hili, asema Bwana,” Yer 7:11. Ndugu yangu, Mungu siyo kwamba
haoni kilio cha watu wake na wanyonge wake kinachosababishwa na watu wacheche
wenye uchu wa hayo niliyokwisha yasema.
Ukimya wa Mungu katika
nyakati hizi ngumu kwetu kama wanadamu, siyo ruksa kwa uovu huo kuendelea, bali
Mungu hutoa nafasi ya kuongoka kwa yule autendao uovu huo. Kuongoka kwa mtu
mwovu ni furaha kubwa kwa Mungu wetu kwani ni kurejea kwa upendo ulioasi. Ni
vyema nikaelewa kwamba hata aliye mwovu ni tokeo la upendo wake Mungu. Na hii
ndiyo maana halisi ya maneno haya ya Injili ya leo, hasa pale Watumwa
walipomtaka Bwana wao awape ruhusa ya kwenda kuyang’oa magugu yaliyoota pamoja na ngano. Kwa watumwa hawa
kutaka kufanya hivyo, Bwana wao anawaambia, “La; msije mkakusanya magugu, na
kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na
wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge
matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu,” Mt 13:29-30. Kwa neno hili la Bwana huyu wa shamba lililomea
ngano na magugu ni dhahiri kwa mwono na msimamo huu wa Mungu juu ya mtu mwovu, “Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana
MUNGU; basi ghairini, mkaishi,” Eze 18:32. Mtakatifu Augustino katika moja ya
maandishi yake anasema, “usimchukie mtu, bali ichukie tabia yake mbaya.” Je,
natumia vyema nafasi na wakati nilionao sasa kutengeneze njia yangu, na matendo
yangu?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Viacheni
vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao,
Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano
ikusanyeni ghalani mwangu,” Mt 13:30
Tusali:-Ee Mungu uliye kimbilio letu, watazame wana
wako na Taifa lako, ili sote kwa umoja wetu tutembee katika kweli na haki.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario