ALHAMISI
WIKI YA 15 YA MWAKA-C
Somo: Isa 26:7-9, 12, 16-17
Zab: 102:13-14ab, 15, 16-18, 19-21
Injili: Mt 11:28-30
Nukuu:
“Njia
yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki,”
Isa 26:7
“Mtu
mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu
atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa Bwana,” Isa 26:10
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu,” Mt 11:29
“kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt
11:30
TAFAKARI: “Njia yake mwenye haki ni unyofu.”
Wapendwa wana wa Mungu, tuyatazamapo mazingira
yetu leo na fursa azipatazo kila mmoja wetu, kutumika kumekuwa kudogo sana
kuliko kufaidi na kufisadi fursa hiyo. Je, tuogelee katika wimbi hili lisilo na
unyofu ndani yake? La hasha, “Njia
yake mwenye haki ni unyofu; Wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki,”
Isa 26:7. Elewa pale ulipo wewe ni nuru na mwanga hata kama unazungukwa na giza
tororo la ubatili na ufisadi. Yesu anasema hivi katika kweli hii, “ninyi ni
nuru ya ulimwengu…vivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona
matendo yenu mema, wamtukuze Baba yetu aliye mbinguni. Taa ya mwili ni jicho;
basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Basi ile nuru
iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!” Mt 5:14b, 16, Mt 6:22, 23b. Jambo
lingine ni hili, katika mazingira ya kawaida kuna msemo huu, ‘aliye
muhuni-mwenye kutembea na kila mtu katika maisha yake kamwe hawezwi
kubadilishwa tu kwa siku ile ya tukio lake la kufunga ndoa.’ Hivyo, “Mtu
mbaya ajapofadhiliwa, Hata hivyo hatajifunza haki; Katika nchi ya unyofu
atatenda udhalimu, Wala hatauona utukufu wa Bwana,” Isa 26:10. Mtu huyu au kwenye hali hii anaitaji muda, na
hasa utayari wa kuachana na hali hiyo.
Hata pamoja na hali na
mazingira hayo, pale tunapokuwa tayari na kufanya maamuzi ya ndani na katika
Kristo kutoka nafsini mwetu, vita hiyo ya nafsi inaushindi. Leo kwa yeyote yule mbatizwa na mwenye kumwamini Kristo, anapata
kitulizo cha kweli ndani na katika Kristo. Ni kupitia Kristo wote twaweza
kuiona nuru na kuishi katika nuru ya kweli. Hakuna jina lingine hapa dunia
twaweza kuokolewa nalo nje ya jina hili, Yesu Kristo, Mdo 4:12. Yesu ndiye
njia, kweli na uzima wetu, Yoh 14:6. Yesu anasema, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na
mizigo, nami nitawapumzisha,” Mt 11:28. Kiboko cha mahangaiko yetu kama watu
waaminio na wafuasi wa Kristo ni Yesu mwenyewe.
Mizigo
yetu na taabu zake zote ni Kristo mwenyewe anayeweza kutubebea tukiwa naye. “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye
kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha,” Mt 11:28. Hakuna pumzisho la kweli nje ya Kristo. Mwongozo
wa kweli katika mahangaiko yetu ni Kristo mwenyewe. Mwongozo wake ni UPENDO, na
hii ndiyo nira yake. “Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu,” Mt 11:29. Ndugu yangu kwa nini hupendi kupenda? Kwa nini
humpendi huyo uliye weka mipaka naye? Je, Yesu angefanya hayo unayoyafanya leo
ungekuwa wapi? Mbona bado anakupa nafasi na hilo bado haulioni katika maisha
yako.
Ndugu
yangu, ukipenda katika kweli yote, yote huwa mepesi. Kipimo cha kupenda
kinawiana na kipimo cha kusamehe. Usipo kuwa mwepesi wa kusamehe bado hujaijua
kweli ya Mungu. Katika hili Yesu anasema, “kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,”
Mt 11:30. Ndugu yangu, ni mzingo upi ulio nao ni mzito ambao Yesu atashindwa
kuubeba?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole
na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu,” Mt 11:29
Tusali:-Ee
Yesu, wewe ndiye kila kitu kwangu. Amina!
No hay comentarios:
Publicar un comentario