martes, 5 de julio de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 14 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 14 YA MWAKA-C
Somo: Hos 11:1-4, 8c-9
Zab: 80:2ac, 3b, 15-16
Injili: Mt 10:7-15
Nukuu:
 “Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao,” Hos 11:4 

Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja,” Hos 11:8d 

Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji,” Hos 11:9

“Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8

“Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo ktika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu,” Mt 10:14

TAFAKARI:Mmepata bure, toeni bure.” 
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na ukweli kwamba ilimpendeza Mungu kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27, Mungu hakutuumba mithili ya ‘maroboti,’ bali alituumba huru na ndivyo tulivyo. Ni kwa uhuru huu tunapoutimia vibaya tunakuwa waasi mbele ya macho yake. Hata katika hali hiyo ya uasi, tunaweza kumrudia tena Mungu katika njia ya toba na majuto ya kweli kwa uhuru huo huo. Ni katika hali hii ya kuwa huru kwamba kila mmoja wetu anawajibika kwa makosa yake mbele za Mungu. Hata hivyo kwa Sifa na Utukufu wake Mungu, yaani; Upendo, Huruma, Haki, Unyenyekevu, Kweli, na Msamaha, hakuchoka kamwe kuturudisha pale tulipopotoka kwa kutumia watumishi wake mbalimbali katika historia nzima ya wokovu wetu. Na hivi ndivyo asemavyo Mungu, Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya,” Hos 11:3. Kwa nini Mungu anayafanya haya yote? Bila shaka Mungu anayafanya haya yote kwa lengo hili madhubuti, yaani, ‘katuumba ili tuishi milele.’

Hivyo utambuapo lengo la kuumbwa kwako linakuwajibisha na kukunyenyekesha wakati huo huo. Wajibu wetu mbele ya Mungu ni kama ifuatavyo; tumjue, tumpende, tumtumikie, na mwisho turudi kwake na kuishi milele. Haya ambayo ni wajibu wetu wa kwanza mbele ya Mungu siyo tokeo la nguvu zetu au juhudi zetu binafsi, bali uwezo huo umewekwa ndani yetu na Mungu mwenyewe kwa sababu Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kutupenda. Naye Yesu anatuambia, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Kumbe ni jambo la msingi sana kuujua lengo la kuumbwa kwako. Kujua lengo hii ni kuanza kuuonja upendo wa Mungu kwako kwamba haupo ulimwenguni hapa kwa bahati mbaya. Hivi ndivyo Mungu anavyolithibitisha jambo hili kwa wana wa Israeli, na kusema,  Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao,” Hos 11:4. Hata pamoja na upendo huu kwa kutotambua lengo la kuumbwa kwao, hawakuacha kutolea sadaka miungu ya Baali na kumwacha Mungu wa kweli, Hos 10:2.

Katika hali na mazingira haya, Mungu huyu wa kweli hakuacha kujinyenyekeza na kutoa fursa ya sisi kumjua. Naye anasema, Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji,” Hos 11:9. Je, Mungu angekuwa ni hakimu wa kutoa adhabu za ‘papo kwa papo,’ ni nani kati yetu angesalimika? Ni wazi hata mbinguni kusingekuwa na Watakatifu. Hapa ndipo tunapoiona huruma ya Mungu. Naye anasema, Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja,” Hos 11:8d. Huyu ndiye Mungu anayemtakia kila mmoja wetu utakatifu kama yeye alivyo mtakatifu, na uzima wa milele. 

Katika somo letu la Injili tunaona wosia wa Yesu anapotuhimiza kutenda bila kujibakiza katika maisha yetu mara zote lile lililo jema na lenye kumpendeza Mungu tukiwa kama viumbe shirikishwa pekee katika uumbaji. “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8. Huu ni wajibu msingi kabisa. Na tunawajibika kufanya hivyo bure kwa vile tumepewa bure. Kama wanadamu mali yetu halali ni dhambi zetu. Hivyo, jambo la msingi la kuelewa juu ya kweli hii ni kwamba tufanyacho ni kwa mkono wa Mungu nasi twafanya tu kama watumishi tena wasio na faida, na tumefanya tu yaliyotupasa kufanya, Lk 17:10.  Ndugu yangu, tuyafanyavyo mambo haya hatufanyi kwa kumpendezesha mtu, bali twayafanya kwa kutimiza wajibu wetu  na hasa kwa kufanya lile linalompendeza Mungu. Hivyo,  “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu,” Mt 10:14. Kukung’uta mavumbi ya miguu ni kutenda lililo jema na kutokutegemea shukrani yoyote. Kama wapo watakao beza tendo hili la wema, adhabu yake ni hapa hapa duniani. Mfano wa adhabu hayo ni kama asemavyo Yesu, kwamba, “itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule,” Mt 10:15 

Ndugu yangu, usipompa Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yako chochote kile chaweza kuyaongoza maisha yako, na mwisho wake ukawa mbaya kwa sababu kitu hicho kama kilivyo hakina umilele. Maadili ya Mbatizwa yeyote yule ni kuwahubiria watu habari njema ya wokovu na ufalme wa Mungu. Yesu anasisitiza jambo hili na kusema,Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 10:7. Na kama lengo la kuumbwa kwetu, tumeumbwa tuishi milele, na duniani hapa siyo makao yetu ya kudumu. Tupo hapa kwa maandalizi tu huku tukijua maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda mfupi. Kila mmoja kadiri ya wito na karama zake, yampasa kutumia vyema karama hizo. Kwa namna hiyo Yesu anatoa wito na kusema, Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 10:8.  Kama ilivyokuwa wajibu ule msingi, yaani viumbe shirikishwa pekee katika uumbaji, hapa msisitizo upo katika matumizi sahihi ya karama na vipaji alivyotujalia Mungu. Pamoja na wajibu huu, Yesu anatoa angalizo pia kuhusu tatizo la kushikamana na mali za dunia hii. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake,” Mt 10:9-10. Kuambatana na mambo haya na kuyapa nafasi ya kwanza upunguza hari na kasi ya kuyatimiza yale tupasayo kufanya.

Ni vyema pia tukawa waangalifu kwa wale watukaribishao na kutupatia ukarimu wao na hifadhi. Maisha ya kutangatanga pasipo mwelekeo sahihi ni hatari sana kwa uchungaji na umisionari kwa ujumla wake. Hivyo Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka,” Mt 10:11. Ni vyema kufanya kile kilichokupeleka pale, na fanya hicho tu. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi,” Mt 10:12-13. Tatizo kubwa hutokea pale tunapobadili nia na sababu ya kuwa pale tulipopaswa kuwa. Tatizo hili ni sawa na “kubadili gia angani ilihali hujui utaangukia wapi kwa maamuzi hayo.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake,” Mt 10:9-10


Tusali:-Ee Bwana tufanya mara zote vyombo vya kuyatimiza mapenzi yako na siyo yetu, hata pale itakapotubidi kutoa sadaka kubwa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario