domingo, 24 de julio de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU YAKOBO MTUME

SIKUKUU YA MTAKATIFU YAKOBO MTUME
25/7
Somo: 2Kor 4:7-15
Zab: 126:1bc-2ab, 2cd-3, 4-5, 6
Injili: Mt 20:20-28
Nukuu:
Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu,” 2Kor 4:8-10

Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti,” 2Kor 4:11 

 “Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako,” Mt 20:21

Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza,” Mt 20:22 

Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,” Mt 20:23 

TAFAKARI: “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yakobo Mtume. Mtume Yakobo kama walivyo kuwa Mitume wengine, alikuwa kielelezo halisi cha upendo wa Kristo na mfano wake hasa katika kuisimamia na kuitetea imani ya kweli bila kujibakiza na kuwa na hofu yoyote ile. Mtume huyu alisimama imara hata pale ilipompasa kufa kwa ajili ya kweli, na imani ya kweli. Msingi wa Kanisa ukiwa ndiye Kristo mwenyewe, Mtume Yakobo kama walivyokuwa Mitume wengine ndizo nguzo za Kanisa la Kristo. Hili liliwezekana kwa Mitume pale walipojichukulia kuwa hazina katika vyombo vya udongo, ili adama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwao.

Hivyo leo kwa namna ya pekee masomo yetu mawili yanamlenga mwanadamu katika uwezo wake na mapungufu yake. Uwezo wa binadamu utiwa nguvu na kusimama imara endapo kutakuwa na muunganiko wa kweli na wa haki kati yake na Muumba wake. Muunganiko huu msingi wake mkubwa ni kujitambua kwake huyu mwanadamu kunakolenga kuweka wazi mafanikio yake, na udhaifu wake. Msingi huu unawezekana kujengwa tu pale ambako binadamu huyu atakubali kujinyenyekeza. Hivyo unapojinyenyeza unafungua ufahamu mwingine wa kujiona kama ulivyo, na si kama watu wasemavyo ulivyo, au mazingira yako unayoishi yanavyokuelekeza na kukutafsiri. Huku ndiko kujitambua kama “u chombo cha udongo.”

Ndugu yangu, ni pale tu unapojitambua kama u chombo cha udongo ndipo zile hazina zilizojificha, mathalani vipaji vyako hujidhihirisha. Ni wakati wa kuishi kile ulicho katika ukweli wake. Tulio wengi hatuishi kile tulicho, bali twaishi vivuli vya wengine. Tunajivika vinyago vya wengine na mwisho wa siku tunabakia kuwa vituko tu. Moja ya sababu kubwa ya watu wengi kutokuwa na furaha ya kweli ndani yao ni kwamba hawajawahi kuishi kile walicho hata mara moja. Hupenda kuwa kama mtu fulani muda wote. Unapoikataa nafsi yako, unajikataa wewe mwenyewe. Je, ni kwa namna gani unaweza kuwa na furaha ya kweli katika mazingira kama hayo? Ni lini basi utavijua vipaji na karama zako kama hukuwahi kuwa kile alichokuumba Mungu? Utawezaje basi kuvithamini vipaji vya wengine kama vyako huvijui? Hivyo, Mtume Paulo anatukumbusha jambo hili, na kusema, Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu,” 2Kor 4:7

Ni katika kujiona kama vyombo vya udongo twaweza kuyakabili yote katika maisha na kuyachukulia bila woga kwa sababu tunajua anayetuimarisha na kutupa nguvu, ni Kristo mwenyewe. Ni kwa sababu hii kwamba, Siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu,” 2Kor 4:10. Hatuna hofu ya kufa wala kupata mateso kwa sababu mwenye nguvu na mamlaka ya mwili na roho ni Mungu mwenyewe, na kwa hali ya kibinadamu twa mtazama Kristo, neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu. Hivyo Yesu anatutia nguvu na kutufanya imara kwa neno hili, “msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28. Nani kama Mungu? Wapo wengi sana leo tunaishi kwa hofu, tena wakati mwingine hofu ya kurogwa na tunapoteza wakati mwingi kuhangaika kwa waganga na kupoteza rasilimali nyingi sana kupitia mlango huu wa shetani. Je, lipi lililo la heshima na baraka kwako; kufa mikononi mwa Kristo, au kufa mikononi mwa mganga wa kienyeji? Mtume Paulo anasema, kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti,” 2Kor 4:11. Hii ndiyo heshima kubwa kwa Mkristo na mfuasi wa Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, ndani na katika Kristo ndiko kwenye uhakika wa kweli kwa sababu pamoja na kuyaonja mauti, Kristo yu hai milele. Je, hizo hirizi unazozivaa, na hayo mazindiko uliyochimbia kwenye kuta za nyumba yako yanausalama zaidi ya usalama ndani na katika Kristo? Ndugu yangu, “tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi,” 2Kor 4:14. Uzima wa kweli upo kwa Kristo tu, na si vinginevyo. Ni vyema kuanzia leo ukafuta kabisa ziara zako hizo rasmi na zisizo rasmi kwa waganga wa kienyeji. Safari hizo sinakukosesha neema na uzima wa Mungu na kujichumia wingi wa laama.

Injili yetu ya leo inalizungumzia kwa mapana swala hili la kujitoa na kutumika kwa ajili ya ufalme wa Mungu, na ndiyo sababu ya Ukristo wetu, na utambulisho wetu mbele ya Mungu. Utambulisho wetu mbele ya Mungu hautokani na sababu ya kukaa kushoto kwake au kulia kwake, bali ni kwa namna gani naishi kwa uaminifu na bila kujibakiza katika mapaswa yake kile alichoniita leo na sasa. Tukiwa waaminifu katika hilo, Yesu anasema, “kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,” Mt 20:23b. Waliowekewa tayari kwa maanisha wale walioyafanya mapenzi ya Mungu kwa uaminifu. Swala hili halipo mwishoni mwa maisha yetu kama kupokea tunzo fulani, bali kila siku ya maisha yetu twaishi tunzo hiyo, au kupokonywa tunzo hiyo. Kila siku ya maisha yetu tupo  darasani, na mtihani wetu ni UPENDO. Upendo ndiyo mizania ya kila kitu tufanyacho.

Ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, UTAMBULISHO wetu mbele ya Mungu, si maisha ninayoishi, mfano; Maisha ya ndoa, Utawa, na Ukleri, au cho chote kile ninachoishi kadiri ya wito wa Mungu, bali utambulisho wetu ni kwa namna gani tunavyotumika kwa kuyatoa maisha yetu bila kujibakiza kwa upendo wake Mungu kwa kile tulichoitiwa, na Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo kuwa kielelezo chetu. Bila hivyo, maisha unayoishi au ninayoyaishi huwa ni maigizo tu. Utambulisho huu kwa maana nyingine ni UTAKATIFU tunaojichotea kwa maisha tunayoyaishi hapa duniani kila mmoja kadiri ya wito wake. UTAMBULISHO huu ndiyo tunzo na UTAKATIFU wetu mbele ya Mungu. Na kwa mantiki hii ndiyo sababu leo Mama Kanisa kwa heshima kubwa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yakobo Mtume, aliyeishi upendo wa Kristo bila kujibakiza, na kuyatoa maisha yake kwa ushuhuda wa kweli hiyo kwa watu wote.

Ndugu yangu, kwa Mungu hatuendi na “CV” zetu, kama tulivyozoea kusikua historia fupi ya Marehemu. Huko Mbinguni hakuna kazi tena zaidi ya kuishi umelele tulioandaliwa, au kuteseka katika umilele tuliojiandalia kwa kuishi ndivyo sivyo. Vyeti vyako, na historia yako kitaaluma ikuwezeshe kuupata utakatifu huo kwa kutumika vyema leo na sasa. Kielelezo chetu kama wafuasi wa Kristo, ni Kristo Yesu Mwenyewe.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu,” Mt 20:23

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tufanye vyombo vyako vya udongo, na katika udogo wetu tujitoe bila kujibakiza. Amina

Mtakatikfu Yakobo Mtume, Utuombee. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario