ALHAMISI
WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Yer 2:1-3, 7-8, 12-13
Zab: 36:6-7ab, 8-9, 10-11
Injili: Mt 13:10-17
Nukuu:
“Enenda
ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakukumbuka, hisani
ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko
jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu,” Yer 2:2
“Israeli
walikuwa utakatifu kwa Bwana; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa
na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana,” Yer 2:3
“Ninyi mmejaliwa
kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano;
kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa,” Mt 13:11,
13
“Lakini, heri
macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia,” Mt 13:16
“Kwa
maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona
mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie,” Mt
13:17
TAFAKARI: “Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope
sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana.”
Wapendwa wana wa Mungu, hakika yapo mambo ya
ajabu sana katika jamii yetu leo ambayo twahitaji ujasiri wa ndani na imani kuyasema,
kuyakemea, na kusema iliyo kweli kadiri ya mapenzi ya Mungu. Nabii Yeremia
anaitwa kwenye jamii ambayo haikuwa tena na hofu ya Mungu. Hata wale ambao
waliujua ukweli kuhusu matakwa ya Mungu waliingiwa upofu na kufuata mkondo wa
‘upepo uovu’ kama ulivyokuwa. Haikuwa ajabu kuwaona makuhani kusimama na
kuwatetea watawala hata pale walipokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu katika
ubovu na uovu wao. Makuhani hawa waliyafanya hayo kwa kuwapendezesha watawala
ili kukidhi mahitaji yao binafsi. Ni katika mazingira haya Mungu anamwinua
Nabii wake Yeremia na kusema ujumbe wa Mungu na matakwa yake.
Wapendwa wana wa Mungu, maisha yako katika ulimwengu huu licha ya
kwamba kuwa siyo ya bahati mbaya, yanamaanisha kwa kiasi kikubwa kwa wakili wa
Mungu katika utume maalumu pale ulipo. Pamoja na mambo yote mazuri ambayo
waweza kufanya, mimi na wewe kama wana wa Mungu, na wafuasi wake Kristo, kila
siku tunaitwa kupambana na aina yoyote ile ya uovu na yenye kufifisha uwepo wa
Mungu pale ulipo. Na hivi ndivyo Nabii Yeremia anatumwa na kuwajibika katika
vita hii ya kweli dhidi ya uovu, kwamba, “Enenda
ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakukumbuka, hisani
ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko
jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu,” Yer 2:2. Kwanza kabisa Mungu anataka
watu wake waelewe nafasi yake na yao ikiwa ni pamoja na yale yote
aliyowatendea. “Israeli walikuwa utakatifu
kwa Bwana; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu
utawajilia; asema Bwana,” Yer 2:3. Bila utakatifu
hakuna uwezekano wa kuwa rafiki na Mungu, kwa sababu asili ya Mungu ni Takatifu
na Utakatifu wenyewe. Mungu wetu ni Mtakatifu!
Pili, Mungu anatoa angalizo la kuuacha uovu
huo ambao unaweka tengano kati yake na wao-‘watu wake.’ Naye Mungu anawakumbusha,
na anatukumbusha pia leo kwamba, “Nami
nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini
ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu
mliufanya kuwa chukizo,” Yer 2:7. Mungu aliye huruma, hapendi watu wake
waangamie katika ujinga na upumbavu wao. Kwa maana “Bwana ana fadhili, ni
mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,” Zab 145:8. Kumbe
ni jambo la busara kujirudi pale unatambua kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.
Tatu,
hata kama mwanadamu ataenenda katika njia yake hatoweza kushinda vita hiyo bila
uwepo wa Mungu. Katika hili Mungu
anawaambia wana wa Israeli, na sisi pia kwamba, “Nami
nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini
ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu
mliufanya kuwa chukizo,” Yer 2:7. Ndugu yangu na Mtanzania mwenzangu, hakuna
aliyejichagua kuzaliwa katika Taifa hili. Ni maajabu yake Mungu wakati
ulipotimia na alipoona inafaa, akafanya kile ambacho leo ndicho ulicho ikiwa ni
utaifa wako kama Mtanzania. Hata kwa kutokuchagua kwako kuwa kile tulicho leo,
ikiwa ni pamoja na kuzaliwa kwako na utaifa wako leo kama Mtanzania,
haikuondolei kutokuwajibika kwa kile Mungu alichokukirimia bure, ikiwa ni
pamoja na rasilimali za Taifa hili. Leo kila mwenye nguvu na nafasi bila kujali
umma uliompa nguvu hizo, tumekuwa chukizo mbele ya macho ya Mungu kwa kutapanya
urithi tuliopewa bure ikiwa si kwa kizazi hiki tu, bali kwa vizazi vyote. Watu
hawa wanaishi kama vile kesho haipo, na leo ndiyo mwisho wa kila kitu. Hivyo
wajibu wao wa kwanza ni kujinufaisha wenyewe na familia zao, huku kundi kubwa
la watu maisha yakiwa heri ya jana.
Jambo
lingine la ajabu nyakati zile za Nabii Yeremia lilikuwa kwamba hata wale ambao
kwa uhakika walijua matakwa ya Mungu, na hivyo kuwa sauti ya wasio na sauti,
waliingiwa upofu na mwisho wa siku waliyapigania matumbo yao na katika ubinafsi
wao. “Makuhani
hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi,
nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu,” Yer
2:8. Je! leo ni jambo la ajabu ‘kuibuka
manabii wa kujitengeneza mwenyewe’ na kutoa sifa kemkem juu ya udhalimu,
utawala dhalimu, na wala rushwa na mafisadi? Leo wako wapi ‘wana-sheria’? Leo
wapo wapi wachungaji wenye hofu ya Mungu wenye kuona kweli kama ilivyo, na
sivyo kama walivyo? Leo wapo wapi wasemaji wa wasio na sauti? Hakika sote
tunaangamia kwa upofu wakujitakia na kwa kuliheshimu tumbo kuliko kweli ya
Mungu. Na hiki ndicho kilio cha Mungu kwetu leo, kwamba, “Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili,
mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana,” Yer 2:12. Ndugu yangu,
inawezekana kabisa kutoka katika hadha hii ikiwa wewe uliye mwananchi mwema na
mwenye hofu ya Mungu ukajua wajibu wako msingi katika Taifa hili na kufanya
sehemu yako kikamilifu. La sivyo Taifa linaangamia licha ya kuzisadifu mbwembwe
za hapa na pale. Hivyo, Wewe uliye mwana sheria, simama katika kweli na haki,
na kwa kufanya hivyo ‘kweli na haki’ ya Mungu itaonekana kwa watu wake na Taifa
lake. Wewe uliye mchungaji, simama vizuri hapa ulipo, lisimamie vyema kundi
ulilopewa, jua wajibu wako wa kusimama katika kweli, haki, huruma, msamaha, na
upendo wa Mungu. Mara zote usukumwe na kiu ya kweli na haki ya Mungu kwa neno
lile ulisomalo kila siku na kulitafakari, na siyo upofu wa tumbo na hitaji
binafsi ambalo mwisho wa siku ni kihama kitupu.
Na
kama ilivyokuwa enzi za Nabii Yeremia, hata leo uovu huja vaa suti mpya na
kubadili madhari yake kama asemavyo Mungu, kwamba, “Kwa
maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi
ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka
maji,” Yer 2:13. Ndugu yangu, hakuna uhai bila Mungu, hakuna njia bila Mungu,
na hakuna kweli bila Mungu. Yesu anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Je, njia zako za panya zitakufikisha kwa Mungu?
Kweli yako ya kughushi ghushi itaifunua kweli ya Mungu ndani yako? Na uzima
wako wa kuzikanyaga haki za watu, na kudhulumu haki za watu una umilele ndani
yake? TAFAKARI!
Wapendwa
wana wa Mungu, yote tuliyoyaona hapo juu, yanasemwa kwa ufupi wa maneno
machache kutoka Injili ya leo; “Kwa
maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye
na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mt 13:12. Ndugu yangu, elewa
kweli hii kwamba, wewe leo katika ulimwengu huu haupo hapa kwa bahati mbaya.
Upo hapa kuwa wakili wa kweli wa Mungu katika wito na utume ule uliokirimiwa na
Mungu mwenyewe kadiri ya hali na nafasi yako. Kwa maana nyingine, usipolifanya
jambo hili ilhali Mungu kakupa uwezo huo bure, ni sawa na mfano ule wa chumvi.
Naye Yesu anasema, “Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena,
mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa
ninyi,” Mk 9:50. Ni kweli kwamba mimi na wewe kama chumvi lazima tuthibitishe
hilo. La sivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwa kama tulivyo. Naye Yesu anasema,
“ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata
ikolee? Haifai tena kabisa ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu,” Mt 5:13. Na
hiki ndicho kihama katika ujumbe wa Injili ya leo, na ndiyo maana ya maneno
hayo ya Yesu kwamba, ‘mwenye
kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho
nacho atanyang'anywa.’ Mt 13:12.
Ni kweli isiyo shaka
kwamba kwa uwezekano wa kuwa wana wa Mungu kwa sadaka ile ya Yesu pale
msalabani, na kwa kuzaliwa upya kwa Sakramenti ya Ubatizo kama ishara ya wazi
ya kufa pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye, mimi na wewe tumefunuliwa
siri za ufalme wa mbinguni. Hivyo mifano anayoitumia Yesu yatupasa
kutufikirisha juu ya siri hiyo kwa sababu hatma yetu ni maisha ya milele.
Hivyo, “Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za
ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa
sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia
hawasikii, wala kuelewa,” Mt 13:11, 13. Ni heshima kubwa sana kuwa wana wa
Mungu na warithi wa ufalme wake. Na huku ndiko kule kuhesabiwa haki.
Wapendwa wana wa Mungu, mambo haya
niyasemayo leo siyo mageni masikioni mwenu. Ila hili ni dhahiri kama wasemavyo
waswahili, ‘sikio la kufa halisikii dawa.” Ni wajibu wa kila kwenye hofu ya
Mungu kuusema ukweli, kuutetea ukweli, na kusimama katika kweli na haki hata
kama kwa kufanya hivyo kutakugharimu maisha yako. Ndugu yangu, Yesu katika hili
anahoji nafsi yako na yangu kwa kuuliza, “itamfaidi mtu nin kuupata ulimwengu
wote, akipata hasara ya nafsi yake. Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?” Mk
8:36-37. Nisipo kuwa tayari kupokea kweli hii leo, unabii wa Isaya kama
asemavyo Yesu ni dhahiri kwetu leo pia, kwamba, “Neno likisema, Kusikia
mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona,” Mt 13:14. Huku
ni kuukubali upofu kwa kuitanguliza nafsi na maslahi binafsi. “Maana
mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho
yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao,
Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya,” Mt 13:15. Je, katika hali na
mazingira kama haya, twaweza kuushinda uovu ilhali tunauatamia?
Ndugu yangu, hakuna
lisilowezekana kwa Mungu kama kila mmoja wetu atajua sababu ya kuumbwa kwake
kama tunavyojifunza kutoka kwenye Katekisimu yetu Katoliki, kwamba, ‘tumeumbwa
ili tumjue Mungu, tumpende, tumtumikie, na mwisho turudi kwake Mbinguni.’ Wenye
kufanya haya watakuwa katika mikono salama ya Mungu kwa sababu wapo tayari
‘kuona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao.’ Hawa ni wale wanye hofu ya
Mungu. Na hawa ndio Yesu anaosema kwamba, “heri
macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia,” Mt 13:16.
Hawa wenye uwezo huu wa ‘kuona kwa vile wana macho yenye uwezo huo, na kusikia
kwa sababu wana masikio yenye uwezo huo wa kusikia, ni zaidi ya manabii. Katika
kweli hii Yesu anatuambia, “amin,
nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi,
wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie,” Mt 13:17. Ndugu yangu
uliyesafiri nami katika tafakari hii, je, wahitaji malaika washuke kutoka
mbinguni na kusema ili uelewe?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona;
na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia,” Mt 13:16
Tusali:-Ee
Yesu, nikumbushe kila siku sababu ya kuumbwa kwangu, na niwe mwaminifu kwa hilo
daima. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario