JUMANNE WIKI YA 17 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 14:17-22
Zab: 79:8, 9, 11, 13
Injili:
Mt 13:36-43
Nukuu:
“Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa
upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa!
Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala
hawana maarifa,” Yer 14:18
“Je!
Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na
dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia
wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!” Yer 14:19
“Ee
Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi,”
Yer 14:20
“Basi, kama vile
magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa
dunia,” Mt 13:40
“Mwana
wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo
yote, na hao watendao maasi, na
kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno,” Mt
13:41
TAFAKARI:
“Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba
zetu; maana tumekutenda dhambi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
pasipo na amani hakuna chochote kile ambacho mimi na wewe twaweza kukifanya kwa
utulivu. Pasipo amani hakuna matumaini. Na kama hakuna matumaini ni vigumu
kuwashawishi watu juu ya kile utakacho waelewe hata kama dhamiri yako ni safi
na njema. Pamoja na hali hiyo, Mungu anamtuma Nabii Yeremia kulisema hili
ambalo Yeye, Mungu amekwisha liona. “Nawe
utawaambia neno hili, Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala
yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu,
kwa jeraha isiyoponyeka,” Yer 14:17. Lililo la kweli lisemwe kama lilivyo ili
kuleta uponyaji, na kufungua milango ya kukabiliana nayo. Ni ajabu sana, na
hasa kwenye jamii yetu leo, wengi wetu wamefikia hatua ya kuubatiza uongo na
kuwa “kweli au utakatifu buniwa.” Je, tunayafanya haya kwa faida ya nani kama
siyo kujichimbia kaburi?
Kwa
nini hatupendi kusema kweli na badala yake twapamba lililo ovu? Kwa nini
tunashindwa kusema na kuona iliyo kweli kama
afanyavyo Nabii Yeremia? Nabii Yeremia anaona iliyo kweli na kusema, “Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko
waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa
sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika
nchi, wala hawana maarifa,” Yer 14:18. Badala yake, leo waliopewa dhamana na
umma wamejiridhisha na kujisahau. Wimbo wao kila siku ni ule wa kurembesha
iliyo ovu na kusema “yote yapo salama, hakuna haja ya kuwa na hofu.” Kama hakuna hofu kwa nini watu hawana furaha?
Kwa nini kila kukicha ni kilio? Kwa nini watu wanapigwa butwaa muda wote?
Kukosa matumaini katika
maisha, ni kifo halisi cha maisha. Maisha hukosa mvuto na mwelekeo. Katika
mazingira ya mtindo huu, mwanadamu huzika rasmi uwezo wake katika ubunifu. Mtu
ubaki kuwa kama tenga tupu! Na hii ndiyo hali iliyowafika wana wa Israeli
katika ya ‘toweko’ la lile tumaini na kusema, “Je!
Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na
dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia
wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!” Yer 14:19. Jamii yoyote ile
inapofikia hatua ya kufanya ‘maamuzi mazito juu ya mstkabali wa maisha yao,’ na
mambo kwenda ndivyo sivyo, matokeo yake ndiyo wingi wa maswali haya yasiyo na
majibu na wakujibu, na mwisho wa siku jamii husika kukosa mwelekeo.
Hata hivyo hakuna jambo
lolote lisilo kuwa na chanzo chake. Ni kweli pasipo shaka kwamba wakati fulani,
na watu fulani, hawakufanya yastahiliyo kweli na haki. Na kuanzia hapo tatizo
hilo lawezekana kukuzwa na kuendelezwa kama utamaduni fulani usio na kweli
ndani yake. Hakika kwa ung’ang’anizi huu wa mila na desturi hizi, wachache
huneemeka nazo ilhali kundi kubwa la watu uteseka na kulipa gharama za
wachache, ‘akina mangi meza.’ Uponyaji wa dhambi hii ya kijamii, yaani “social
sin,” ni kujirudi tu. Na hivi ndivyo Nabii Yeremia anavyotambua chanzo cha uovu
wote na kusema, “Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana
tumekutenda dhambi,” Yer 14:20. Ukiri wa kweli ni tiba ya kweli na mwanzo mpya
wa kulitatua tatizo.
Je, ni
wangapi walio tayari kuzivua tai zao na kuvaa mavazi ya kawaida na kuonekana wa
kawaida mbele ya jamii iliyowakuza na kuwa mamangi meza? Wengi wa watu hawa
hukubali kufa na tai zao shingoni, yaani uovu wao. Lakini bila kujisalimisha
hakuna usalama. Ifike mahali tukiri na kusema, “Usituchukie,
kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako,
kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi,” Yer 14:21. Hivi Mungu akivunja
agano lake, yaani, ‘kuto kuurithi ufalme wa mbinguni,’ umaana wa maisha yako ya
kujibohofisha kwa anasa na starehe yana nafasi na faida gani?
Kumbe ni vyema
nikafahamu njia zangu, na uhalisia wa ufalme wa Mungu. Na hivi ndivyo Yesu
anavyofafanua mfano ule wa magugu na ngano kuota pamoja. Naye anasema, “Azipandaye zile mbegu
njema ni Mwana wa Adamu,” Mt 13:37. Mbegu hizi ni wana wa ufalme wa Mungu, kwa
kupitia Yesu Kristo kwa kifo kile cha Msalaba tulichohesabiwa haki. Magugu ni
wana wa yule mwovu shetani mwenye kwenda kinyume cha lolote lile jema katika
kweli na haki. Hivyo, “lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni
wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu,” Mt 13:38. Wana wa hawa
mwovu hawawezi kuyafanya hayo bila kusukumwa na roho ovu ndani yao. Na msukumo
huu ni kuridhia hali hiyo. Shetani hawezi kufanya chochote bila maridhiano
nawe. Kwa maana hiyo, “yule adui
aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni
malaika,” Mt 13:39. Kumbe si vyema kumsingizia shetani tu na kuitoa nafsi yetu
iliyoshiriki moja kwa moja au kwa sehemu katika kweli hiyo.
Hata hivyo, pamoja na
huruma na upendo wa Mungu kuwa mkubwa kuliko dhambi zetu, na mwisho wa siku
tukashindwa kuuridhia upendo na huruma hiyo, kifuatacho ni hukumu ya kweli na
haki. “Basi,
kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika
mwisho wa dunia,” Mt 13:40. Kumbe hukumu ya mwisho ni hakikisho la haki tu,
yaani, ‘justification’ kwa yale yote tuliyoyatenda ambayo kwayo ndiyo kweli
ipasayo hukumu. Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, ndiye mwenye
kuyaratibisha yote hayo siku ile ya mwisho kwa sababu kwa kumwilishwa kwake
kumempa fursa kubwa ya kuujua ubinadamu wetu katika wema na mabaya. Na hivi
ndivyo itakavyo kuwa, yaani, “Mwana wa
Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake
machukizo yote, na hao watendao maasi, na
kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno,” Mt
13:41-42. Ndugu yangu, utalikwepa fekeo hili?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi,
kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika
mwisho wa dunia,” Mt 13:40
Tusali:-
Ee Yesu na Mkombozi wetu, tujalie nguvu ya kuushinda uovu kwa wema nasi kuwa
watu wema. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario