jueves, 21 de julio de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 16 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Yer 3:14-17
Zab: Yer 31:10, 11-12ab, 13
Injili: Mt 13:18-23
Nukuu:
Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana,” Yer 3:14a

nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu,” Yer 3:15

 “Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini,” Mt 13:23 

TAFAKARI: “Bwana asema, Rudini, enyi watoto wenye kuasi.”

Wapendwa wana wa Mungu, ujumbe wa Mungu mara zote, nyakati zote, na kwa namna moja au nyingine, ujumbe huo uelezea upendo na huruma yake. Hivyo kazi kubwa ipo upande wako na wangu kuridhia upendo na huruma hii ya Mungu. Ni upendo na huruma yake Mungu anasema, “sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi,” Eze 33:11. Ni kwa huruma na upendo wa ajabu aliokuwa nao Mungu kwetu kwamba ‘neema na huruma yake ni kubwa kuliko dhambi zetu.’ Na hiki ndicho Mungu kwa upendo na huruma yake anacho kidhihirisha kwetu kwa kusema, Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18. Mungu hakuacha kamwe na hataacha daima kutupenda na kutuhurumia pale tunapokuwa tayari kwa kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi zetu na kuridhia upendo na huruma yake. Kama watoto wake, Mungu kwa kupitia kinywa cha Mtumishi wake Nabii Yeremia anatuambia, Rudini, enyi watoto wenye kuasi,” Yer 3:14a. Kumuasi Mungu hakuna heri wala usalama.

Tunapomrudia Mungu kwa wema na unyenyekevu hatoshindwa kuijenga tena nyumba yake iliyobomoka, yaani, Taifa lake, kama tokeo la dhambi. Naye anasema, nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu,” Yer 3:15. Huyu ndiye Mungu aliye Upendo na Huruma, “amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili,” Zab103:8. Ni Mungu mwenye kutimiza ahadi zake na mwenye kumtakia kila mmoja heri na neema kwa sababu ndani ya kila mmoja kuna chapa yake, Mwa 1:27. Na kwa ahadi zake Mungu anasema, Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha Bwana; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la Bwana; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya,” Yer 3:17. Hakika hakuna lisilowezekana kwa Mungu.

 Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo inatoa ufafanuzi wa habari ile ya Mpanzi. Leo Yesu anafafanua lugha ile ya picha aliyoitumia kadiri ya mazingira na watu wake. Lengo la lugha ile ya picha kuhusu Mpanza, ni kuelezea kweli hiyo ya Mungu ndani ya mioyo yetu. Hivyo alichokifanya  Mpanzi ilikuwa ni namna neno la Mungu lifanyavyo kazi ndani ya mioyo yetu na kutubadilisha. Ili neno la Mungu liwe tumaini la kweli, kama tulivyokwisha kuona siku mbili zilizopita, na ushuhuda wa kweli ndani yetu, na kwa wale wanaotuzunguka, lazima neno hilo tulisikie, tulipokee, kulitafakari, kulishirikishe, na mwisho tuwe sehemu ya neno hilo kwa kuwa mashahidi wa neno hata ikibidi kufa kwa kweli hiyo. Kulipokea neno lazima uwe na utayari wa kulisikia neno. Usipokuwa na utayari huu ni sawa na  “mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila,” Mt 13:4. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu; Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia,” Mt 13:19 

Kulitafakari neno la Mungu kunakuhitaji kulisikia neno hilo na liguse maisha yako. Kutafakari neno ni kama kucheua kile ulichokula. Kama hili halikufanyika ni sawa na mbegu zile zilizoanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina, na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka,” Mt 13:5-6. Na hapa Yesu anatuambia kwa kuifafanue lugha ile ya picha, kwamba, Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa,” Mt 13:20-21. Kulipokea neno kwa furaha na kukosa mizizi ndani yake, ni kukosa tafakari ya kina juu ya kile ulichokisikia au kukisoma. Ni kutokulicheua neno, na hivyo neno hilo kutokuwa sehemu ya maisha yako, na kutokukupa uwezekano wa kulishirikisha kwa wengine. Huwezi kutoa usichokuwa nacho. Je, itawezekana kweli kushirikisha kwa wengine kile usichokuwa nacho?

Wapendwa wana wa Mungu, kuwa na uwezo wa kulishirikisha neno la Mungu kunategemea sana namna tunavyolicheua neno la Mungu, yaani, uwezo ule wa kulitafakari neno la Mungu na kuleta mabadiliko kwanza ndani yetu. Tunaposhindwa kufanya hivyo ni sawa na mbegu  “zilizoanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga,” Mt 13:7. Kumbe tunaweza kushirikishana neno la Mungu vizuri pale tunapokuwa na mazingira mazuri ya kulitafakari neno la Mungu kama lilivyo, na siyo tulivyo kwa kujionea huruma. Na hapa Yesu anafafanua lughu hii ya picha na kusema, Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai,” Mt 13:22. Leo ni wangapi tu sehemu ya Jumuiya ndogo ndogo iliyopo kwenye eneno lako, ikiwa ni pamoja na kwenda kwenye jumuiya hiyo na kuwa sehemu ya familia hiyo, ukiumega mkate na kushirikishana neno la Mungu? Leo jumuiya hizi sehemu nyingi zimekuwa kundi la watoto, akina mama, tena wajane, na wazee. Hakuna vijana, na wala hakuna akina Baba. Je, hayo malimwengu unayoyakubatia yana uzima ndani yake au umebaki kujifariji katika upumbavu? Tukifanikiwa katika hatua hii, yaani, kuliishi neno la Mungu, ni wazi tu mashahidi wazuri wa neno la Mungu ndani yetu na wale wote wanaotuzunguka.

 Kuwa mashahidi na washuhuda wa neno ni sawa na mbegu zile zilizoanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini,” Mt 13:8. Hiki ndicho atakacho Yesu kwako na kwangu, yaani, tuwe mashahidi wa kweli wa neno la Mungu. Na huu ndio ufafanuzi wa Yesu juu ya udongo mzuri;Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini,” Mt 13:23. Kuzaa huku matunda kwa viwango tofauti tofauti kunatokana na nguvu ya Roho ile isukumayo ufahamu wetu juu ya neno ambalo sasa siyo tu tumelisika, bali tumelipokea. Na siyo tu tumelipokea, bali tumelitafakari kwa kina na kulicheua. Na siyo tu tumelitafakari kwa kina na kulicheua, bali kwa sasa tumelishirikisha vyema kwa wengine (uinjilishaji upya). Na mwisho siyo tu tumelishirikisha neno hilo kwa wengine bali tumekuwa sehemu ya neno hilo, kwa kuwa mashahidi na washuhuda wa kweli kwa sababu maisha yetu yanaakisi kweli hiyo. Kumbe haitoshi kufanya mambo mazuri katika ukamilifu wake, bali yakupasa kuwa mkamilifu katika maana halisi ya ukamifu kama anavyotuasa Yesu, Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.

Tumsifu Yesu Kristo!

Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini,” Mt 13:23


Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie nguvu, neema, hekima na uwezo wa kulisikia neno lako, kulipokea, kulitafakari, kulishirikisha, na kuwa mashahidi na washuhuda wa Neno hilo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario