JUMATANO
WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Yer 1:1, 4-10
Zab: 71:1-2, 3-4a, 5-6ab, 15ab y 17
Injili: Mt 13:1-9
Nukuu:
“Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa,” Yer 1:5
“Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema;
maana mimi ni mtoto,” Yer 1:6
“Akawaambia mambo
mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda,” Mt 13:3
“nyingine
zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja
thelathini,” Mt 13:8
TAFAKARI: “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa.”
Wapendwa wana wa Mungu, kuzaliwa siyo lazima,
ila ukisha zaliwa kufa ni lazima. Kama kufa ni lazima, basi yakupasa kufa kifo
chenye hadhi, yaani uache simulizi jema. Hapa ndipo penye tofauti kati ya
“Lihoka na Muhenga.” Lihoka ni Roho Chafu au mbaya, na ndani yake hakuna
chochote cha kujifunza, zaidi ya uharibifu. Mhenga ni Roho njema, na yenye
kuigwa hata baada ya nafsi husika kutoka kwenye ulimwengu huu na kuingia katika
ulimwengu wa roho. Mfano: leo kila mtu anapotaka kuelezea Tanzania anayoipenda
na angependa iwe hivyo haachi kumnukuu Mwalimu Nyerere, Rais wa kwanza wa
Jamuhuri ya Tanzania. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa Taifa la Tanzania
leo ni Mhenga, yaani, ameacha mazuri ya kujifunza. Leo Baba huyu anatambulika
kama “Baba wa Taifa la Tanzania,” pasipo kikao chochote rasmi cha kumtambulisha
hivyo. Sifa hii imekuja kama ilivyo kutokana na mastahili yake kama yalivyo.
Hakika ni jambo la ajabu sana, na kama muhujizi wa kutambua utakatifu wake,
basi tuanze hapa.
Ndugu yangu tunayesafari sote katika tafakari
hii, ni vyema ukaelewa jambo hili; kama leo upo hai na unapumua, elewa kwamba
“kabla hujaumbwa katika tumbo la Mama yako Mungu alikujua, na kabla hujatoka
tumboni mwa Mama yako alikutakasa.” Nini maana ya maneno haya? Moja, wewe si wa
bahati mbaya hapa duniani. Inawezekana kuna utata fulani katika kuzaliwa kwako
kusikofuata utaratibu wa bila na desturi zetu, yaani, (Baba halali, nk), lakini
elewa kwamba Mungu ndiye aliyekupa kibali cha kuishi na ndivyo ulivyo leo kama
ulivyo. Pili, kwa uhai wako leo, Mungu anapenda mwisho wa siku uwe Mhenga,
yaani, ‘uache kitu cha kuigwa katika ulimwengu huu.’ Na hii ndiyo maana ya
maneno haya; “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni
alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Kumbe mwisho wa siku wa maisha yangu kama Mhenga ni
kuwa Mtakatifu kama Baba yangu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Utakatifu kwa
hakika ndicho cheo chetu cha juu kabisa kuliko vyeo vyote. Bila Utakatifu
huwezi kumwona Mungu hata kama leo katika ulimwengu huu kila mwanadamu
atakuabudu na kukutukuza. Lakini kwa ubinadamu wao hawawezi kukupatia cheo
hiki, yaani, utakatifu. Ndiyo twasema, ‘waweza kuwa na marafiki wengi, ila siyo
‘watakatifu.’
Hivyo, kama leo uwepo wako hapa duniani ‘sio kwa bahati
mbaya,’ Mungu anamaanisha haya aliyomaanisha alipo mwita Nabii Yeremia, kwamba,
“Kabla sijakuumba katika
tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii
wa mataifa,” Yer 1:5. Mungu asemapo ‘ndiyo,’ hakuna malaka yoyote hapa duniani
yenye uwezo wa kupindisha matakwa ya Mungu. Mamlaka hizi hapa duniani zinaweza
kuchelewesha tu (na Mungu kuruhusu hali hiyo) kile apendacho Mungu uwe kwa
lengo la kukuimarisha, na wakati huo huo kutoa fundisho wa jamii husika.
Ni kweli isiyo shaka kwamba tuupimapo uwezo wetu na mazingira
yetu, ni vigumu kukubaliana na matakwa ya Mungu kwa sababu sisi kama wanadamu
tuna mipaka na kikomo chetu. Mungu ni zaidi ya mipaka na vikomo vyetu. Katika
mazingira na hali hii, Yeremia anajibu wito huo mbele ya Mungu kama ifuatavyo, “Aa,
Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto,” Yer 1:6. Ni kweli
hakuna anayekua kwa mzazi wake. Kama mzazi wako yu hai, basi kwa hakika huwezi
kuondoa ukweli wa wewe kuwa mtoto. Ila utoto huu si katika hali ya ‘kitoto,’
bali utoto wa ‘kujitambua,’ na wenye kubeba wajibu. Kwa mantiki hii, Mungu
alimjibu Yeremia na kumwambia, “Usiseme, Mimi ni mtoto; maana
utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno
nitakalokuamuru,” Yer 1:7. Hapa ndipo kwenye wajibu. Ndugu yangu, uwepo wako
hapa ulipo ni ‘WAJIBU.’ Kile kisichokuwa na wajibu si ‘hai.’ Mimi na wewe leo
tunaposema ‘sina cha kufanya,’ ni sawa na kuukubali ‘ufu’ ungali hai. Ni kweli
kabisa kwamba ‘wajibu’ fulani ututia hofu kwa sababu wajibu huo unatutaka
‘kuvuja’ ili ‘uhai’ uwepo pale tulipo. Hata katika mazingira haya ya hofu,
Mungu anasema, “Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja
nawe nikuokoe,” Yer 1:8. Je, kwa hakikisho hili la Mungu bado waikumbatia hofu
yako?
Ndugu yangu, ni pale tu unapoishinda hofu yako ndipo Mungu
huunyoosha mkono wake na kuyatakasa mapungufu yako na kukupa uwezo ya
kuyakabili yote katika njie ile aliyokuitia. Hivi ndivyo anavyokiri Nabii
Yeremia, “Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa
changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia,
nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na
kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda,” Yer 1:9-10. Je, naamini nguvu
ya Mungu ndani yangu?
Wapendwa wana wa Mungu, Injili ya leo inatoa mifano
mbalimbali namna tuupokeapo ujumbe wa Mungu na kuufanyia kazi. Yesu anatumia
lugha ya picha kuelezea kweli hiyo ndani ya mioyo yetu. Kuufikisha ujumbe huo,
Yesu anatupa mfano wa mpanzi. Afanyacho mpanzi huyu ni namna neno la Mungu
lifanyavyo kazi ndani ya mioyo yetu na kutubadilisha. Ili neno la Mungu liwe
tumaini la kweli, na ushuhuda wa kweli ndani yetu na kwa wale wanaotuzunguka,
lazima neno hilo tulisikie, tulipokee, kulitafakari, kulishirikishe, na mwisho
tuwe sehemu ya neno hilo kwa kuwa mashahidi wa neno hata ikibidi kufa kwa kweli
hiyo. Kulipokea neno lazima uwe na utayari wa kulisikia neno. Usipokuwa na
utayari huu ni sawa na “mbegu nyingine
zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila,” Mt 13:4.
Kulitafakari
neno la Mungu kunakuhitaji kulisikia neno hilo na liguse maisha yako.
Kutafakari neno ni kama kucheua kile ulichokula. Kama hili halikufanyika ni
sawa na mbegu zile “zilizoanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo
mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina, na jua lilipozuka ziliungua; na
kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka,” Mt 13:5-6.
Ndugu
yangu, kuwa na uwezo wa kulishirikisha neno la Mungu kunategemea sana namna
tunavyolicheua neno la Mungu, yaani, uwezo ule wa kulitafakari neno la Mungu.
Tunaposhindwa kufanya hivyo ni sawa na mbegu “zilizoanguka penye miiba; ile
miiba ikamea, ikazisonga,” Mt 13:7. Kumba tunaweza kushirikisha neno la Mungu
vizuri pale tunapokuwa na mazingira mazuri ya kulitafakari neno la Mungu kama
lilivyo, na siyo tulivyo kwa kujionea huruma. Tunapofanikiwa katika hatua hii,
ni wazi tu mashahidi wazuri wa neno la Mungu ndani yetu na wale wote
wanaotuzunguka.
Kuwa mashahidi na washuhuda wa neno ni sawa na
mbegu zile zilizoanguka “penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini,
moja thelathini,” Mt 13:8. Hiki ndicho atakacho Yesu kwako na kwangu, yaani,
tuwe mashahidi wa kweli wa neno la Mungu.
Tumsifu
Yesu Kristo
“Nyingine
zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja
thelathini,” Mt 13:8
Tusali:-Ee
Yesu, tufanye mbegu bora na zenye kuzaa vizuri pale tulipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario