viernes, 15 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 15 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 15 YA MWAKA-C
Somo: Mik 2:1-5
Zab: 10:1-2, 3-4, 7-8, 14
Injili: Mt 12:14-21
Nukuu:
Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao,” Mik 2:1 

Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake,” Mik 2:2

Basi Bwana asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya,” Mik 2:3

Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe,” Mt 12:15-16

Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda,” Mt 12:20

Na jina lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21

TAFAKARI:Na jina lake Mataifa watalitumainia.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni ukiri ulio wazi kwamba jumuiya ya kwanza ya Wakristo waliona ‘Ukuu na Utukufu’ wa jina ya ‘Yesu Kristo’ katika maisha na changamoto zao za kila siku. Na kwa matiki hiyo, Mtume Petro anayasema haya; “hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana ‘hapana jina’ linguine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, pamoja na Imani yangu kama Mkristo, kuna jambo moja ambalo sina shaka nalo kabisa katika njia hii niifuataya. Tuitazamapo historia ya mwanadamu na wokovu wake, wametokea watu wengu na wenye uwezo (kiimani na kimaadili) kiasi cha kwamba waliweza hata kuanzisha mitindo ya maisha na imani zake na kupokelewa kwa wingi wa watu. Hata pamoja na ukweli huo, watu hawa waliishi na mwisho wa siku walikufa.

 Pamoja na ukweli kwamba Bwaba wetu Kristo naye aliishi na mwisho wa siku alikufa, tofauti na hawa wengine ni kwamba, ‘Kristo baada ya siku tatu alifufuka kutoka wafu.’ Kwa kweli hii na tendo hili, sina shaka kabisa kwa njia hii niifuatayao hasa kwa maneno haya ya uzima ya Bwana wangu Yesu Kristo, kwamba, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Yesu anaenda mbali zaidi na kusema, “Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,” Yoh 17:3. Ni katika mantiki hii kwamba, kama wote tupo hapa duniani kwa sababu na malengo, na mwisho wa siku kuna maisha baada ya kifo, ni dhahiri kwamba, “jina lake (Yesu Kristo) Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21.

Kuishi katika tumaini la kweli na haki ni kutenda yale yampendezayo Mungu. Ni kuishi maisha ya ukamilifu kila siku ingawa udhaifu upo. Na hivi ndivyo Mfalme Sulemani anavyowaswa na Mungu kuishi; “na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli,” 1Fal 9:4-5. Kwa wanyofu wa moyo ‘ukamilifu’ ni akiba ya ‘hekima kamili,’ kama tusomavyo kutoka kitabu cha Mithali, “kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu; Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu,” Mit 2:6-7. Kumbe njia iliyo salama ni kutenda kadiri ya Hekima ya Mungu tukilenga ule ukamilifu ingawa udhaifu upo. Na angalizo ni hili; Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao,” Mik 2:1. Mimi na wewe yatupasa kuwaza na kutenda lililo kweli na haki kwa yeyote yule ninayekutana naye. Wale wote wasio na soni machoni mwao na kupoteza kweli na haki, hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake,” Mik 2:2. Ni kuwa na tamaa ya kila kitu, ilihali uwezo huo hauna kwa sababu katika ulimwengu huu sote twaishi kwa wakati tu.

Ndugu yangu, Bwana asema hivi, ‘Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya,’” Mik 2:3. Kumbe hatupaswa kuuchukulia upole na huruma ya Mungu kama nafasi ya kukwepa wajibu wetu. Hakuna haki pasipo wajibu.

 Hata hivyo ni vigumu sana kuukataa mfumo wa maisha ambao kwayo tumeishi muda mrefu hata kama hauna tija. Wengi wetu huogopa sana kile tusichokijua kwa yale tuyatarajiayo. Ni ndani na katika Kristo tunapata uhakika wa kile tusichokijua na tusichokuwa nacho katika uhasilia wake licha ya shida na dhiki tuzipatazo kadiri ya wito kwa kila mmoja wetu. Mungu anasema hivi juu ya Yesu, yaani, uwezo na mamlaka aliyonayo, kwamba, Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda,” Mt 12:20. Huyu ndiye Yesu!

Wapendwa wana wa Mungu, ni kupitia jina lake Yesu Kristo twaponywa na twalitumainia milele yote. Ukweli huu si kwa sisi tu wafuasi wake, yaani wabatizwa-wakristo, bali kwa mataifa yote.Na jina lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21. Kwa hiyo ndugu yangu, popote pale ulipo mfanye Yesu kuwa sababu ya ukweli ndani yako, njia ya maisha yako, na uhai wako.

Tumsifu Yesu Kristo!
Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao!” Mik 2:1a


Tusali:-Ee Yesu Mwema nitalihimidi jina lako milele. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario