JUMAPILI YA 14 YA MWAKA-C
Somo
I: Isa 66:10-14c
Zab: 66:1-3, 4-5, 6-7, 16, 20 (K) 1
Somo
II: Gal 6:14-18
Injili:
Lk 10:1-12, 17-20
Nukuu:
“Furahini
pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao;
furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate
kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa
kwa wingi wa utukufu wake,” Isa 66:10-11
“Maana Bwana
asema hivi, Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama
kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti
mtabembelezwa,” Isa 66:12
“Lakini mimi,
hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu
Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,”
Gal 6:14
“Kwa
sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya,” Gal 6:15
“Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni
wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno
yake,” Lk 10:2
“Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie
mtu njiani,” Lk 10:4
TAFAKARI: “Furahi pamoja na Kristo, tafakari juu
ya Msalaba Mtakatifu, kwani hapo ndipo penye kigoto cha furaha yako, na ndiyo
fahari yako.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya ‘14’ ya mwaka ‘C’ wa Kanisa. Leo Mama
Kanisa kwa namna ya pekee anatutaka tufahamu kwa undani sababu ya furaha yetu,
na hapo ndipo penye kigoto chetu. Ni ‘kufurahi pamoja na Kristo, kutafakari juu
ya Msalaba Mtakatifu, kwani hapo ndipo penye kigoto cha furaha yako, na ndiyo
fahari yako.’ Ikiwa sadaka yake Yesu pale Msalabani inadhihirisha upendo wa
kweli juu yako na yangu, kwa kututoa katika utumwa wa dhambi na kuhesabiwa haki
kuwa wana wa Mungu, safari hii Mungu alianza mapema hata kabla ya kuumbwa kwa
ulimwengu. Uumbaji katika upana wake unadhihirisha makusudi ya Mungu
kutushirikisha furaha yake.
Na ndiyo maana pamoja
na mateso ya wana wa Israeli yaliyoyapitia katika historia hii ya wokovu, leo
Mungu anawafunulia lengo na furaha yake kupitia Nabii wake Isaya. Naye anasema,
“Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili
yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao
kwa ajili yake; mpate
kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa
kwa wingi wa utukufu wake,” Isa 66:10-11. Hata hivyo furaha ya kweli siyo hii
itokanayo na kushibishwa kwa maziwa na yote yale yaharibikayo, bali, “Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na
utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa;
na juu ya magoti mtabembelezwa,” Isa 66:12. Furaha hii yote inaelekezwa katika
tendo lile la kumwilisha kwa Neno na kukaa kwetu, Yoh 1:14.
Neno
huyu aliyemwishwa, yaani Bwana wetu Yesu Kristo, “Nanyi
mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi;
na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake,” Isa 66:14. Na hivi
ndivyo iliyokuwa kwamba, “Hata
ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na
mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi
awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa
wana,” Gal 4:4-5. Huyu mwana, yaani, Yesu Kristo, ndiye kigoto cha furaha yetu
na fahari yetu. Kama
jumuiya ya wenye hofu ya Mungu, Yesu anatualika kuliomba hili kadiri ya maitaji
ya Kanisa lake, na kusema, “Mavuno
ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno
apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Lk 10:2. Hili ni jukumu la kila
mbatizwa.
Kufikia
lengo la kuutangaza ufalme wa Mbinguni kwa wengine, sisi tuliopata habari hii
ya wokovu yatupasa kulisimamia jambo hilo kwa weledi mkubwa, kwa kuwa waaminifu
kwalo, na kuushikilia ukweli huu bila kutetereka. Yesu anatutaka kuwa makini
sana huko tuendako kuupeleka ujumbe wa wokovu. Naye anasema, “Basi,
kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi
amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii,”
Lk 10:7. Na lifanyike jambo moja kwa wakati. Hii ni pamoja na kuwa makini kwa
jambo lile lile tu. Tusibebe ajenda nyingi katika safari hii ya uinjilishaji.
Mambo hayo {mfuko, mkoba, viatu na wala kuwaamkie mtu njiani} tukiambatana nayo
yatatuchanganya na kutufanya tupoteze mwelekeo. Tuambatane na kubeba yale tu
tunayohitaji kwa utume huo. Tusipokuwa na uchache wa vitu furaha na amani ya
kweli hutoweka. Tusiuzunike pale ambapo tunaona mambo hayakwenda kama
tulivyotarajia. Kufanya hivyo ni kupoteza muda bure kwani muda hautungoji hata
kidogo.
Katika
jambo hili Yesu anasema, “Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi,
tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu
yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya
kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia,” Lk 10:10-11. Jambo la msingi na la kuzingatia
ni kufanya yale tu tuliyotarajia kuyafanya na kuwa na mahusiano mazuri na wale
tuliokusudia kuwainjilisha neno la Mungu. “Na
mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele
yenu; waponyeni wagonjwa waliomo,
waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia,” Lk 10:8-9. Tuyafanyapo haya kwa
unyenyekevu bila kujibakiza huwa msingi wa furaha na Amani yetu.
Wanafunzi
wa Yesu wale sabini, wanarudi katika utume wao na kustajabia mambo makuu ya
Mungu aliowatendea. Uhusiano wetu mzuri na Mungu ni chanzo kikubwa sana cha
furaha yetu ya kweli. Lakini Yesu anawaambia wasiwe na furaha tu kwa sababu
walimwana shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme, bali ndani yao Mungu
aweza kufanya mambo makubwa zaidi ya hayo. “Tazama,
nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na n’nge, na nguvu zote za yule adui, wala
hakuna kitu kitakachowadhuru,” Lk 10:19. Huu
ndio msingi wa furaha ya kweli kwa wale wote wenye hofu ya Mungu. Mahusiano
mazuri na Mungu, hutujengea uwezo mkubwa sana wa kupambana na uovu.
Mara tuyaonapo haya
makuu yakifanyika ndani mwetu tusibweteke. Dunia hii tunapoishi pomoja na uzuri
wake na mambo yake, siyo mahali petu pa kudumu. Hapa ni mahali tu pa maandalizi
ya umilele. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupafanya hapa duniani kuwa sehemu
nzuri zaidi ya kuishi huku tukijua siyo sehemu ya mwisho na ya umilele.
Maandalizi mazuri ya hapa duniani ndiyo jibu la uhakika wa maisha hayo ya
umilele. Hivyo furaha yetu kwa yote tutakayoyapata hapa duniani itupe taswira
halisi ya maisha baada ya haya. Kuhusu ukweli huu Yesu anawaonya wanafunzi wake
nasi pia kwa kusema, “Lakini,
msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu
yameandikwa mbinguni,” Lk 10:20. Furaha yetu isiwe tu ya leo na kesho, bali
furahi hii ipewe kibali na Mungu Baba wa Mbinguni. Tufurahi na Mungu milele
mbinguni. Je, nini hasa kigoto cha furaha yako?
Ndugu
yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, ni vyema leo ukajua
‘kigoto’-‘tumaini la kweli la furaha yako.’ Furaha anayotutaka Yesu tuwe nayo
siyo furaha ya leo na kesho. La hasha! Furaha hii isiwe sababu ya yale tuliyo
nayo au kumiliki, bali furaha ile iliyopo ndani mwetu hata kwa kuyakosa hayo ya
leo na kesho. Ni furaha yenye kuakisiwa na ‘kigoto,’ tumaini la kweli. Hii
ndiyo furaha anayoisema Yesu Kwamba, “ninyi hivi sasa mna
huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu
hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Hii ni furaha ya kupendwa na Yesu upeo, Yoh
13:1. Upendo huu wa ajabu kwetu ndiyo sababu ya Yesu kuutoa uhai wake kwa ajili
yako na yangu. Kwa upendo huu, hakuna aliye ‘chuma chakavu,’ yaani, ‘kisichofaa kwa kilivyo’ mbele
ya uso wa Mungu. Thamani yako na yangu mbele ya Mungu ni kubwa kuliko vitu
vyote, na ndiyo maana ilimpendeza kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Na
hivi ndiyo Mtume Petro anavyoelezea thamani hii yako na yangu mbele ya Mungu; “Nanyi
mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu;
mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa
damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya
Kristo,” 1Pet 1:18-19. Thamani hii uliyonayo mbele ya Mungu ni upendo na furaha
ya kweli iliyo ndani ya fumbo zima la Msalaba. Hivyo niutazamapo Msalaba
Mtakatifu nione ‘kigoto’ cha furaha yangu kwa kupendwa na Kristo, na thamani
niliyopewa na Kristo, leo kuhesabiwa haki kuwa mwana wa Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
Msalaba Mtakatifu ambao ndio kigoto cha furaha yangu, na ufunuo wa kweli na
wawazi wa kupendwa kwangu Kristo, na sababu ya kuhesabiwa haki ya kuwa mwana wa
Mungu, ndiyo furaha na fahari yangu hapa duniani. Hatua hii ya uelewa ndiyo
hatua ya juu na ya pekee ya fumbo hili zima la maisha ya kiroho ambayo mti huu
wa ajabu wa Msalaba kutokea katika historia ya mwanadamu, ndipo ulipotundikwa
wokovu wetu. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Mtume Paulo kwamba, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu
cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Huku ndiko
kujisalimisha pasipo kujibakiza, na ndiyo kuabudu kuliko kweli na haki. Hatua
hii ndiyo hali ile ya kufanywa kiumbe kipya ndani na katika Kristo. Mengine
katika maisha ni mbwembwe za hapa na pale ambazo ndani yake hakuna uzima wa
milele. “Kwa
sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya,” Gal 6:15.
Je, hatua hii ya maisha ya kiroho na furaha yake, yupo wa kukuondolea?
Basi na tusema pamoja na Mtume Paulo
kwamba, “Tangu
sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu,”
Gal 6:17. Na chapa za Kristo ni zile tuzitafakarizo tunapomtazama Kristo kama
Mfalme. Na Ufalme wa Kristo ni ufalme wa haki na uzima, ufalme wa utakatitifu
na Neema, ufalme wa mapendo na amani. Hivyo mimi kama mwana wa Mfalme, nifanane
na Yesu Kristo nifanane na kusimama katika Haki na Uzima, Utakatifu na Neema,
Upendo na Amani. Ndugu yangu, nje ya ukweli huu tufanyacho kama wafuasi wa
Kristo ni ‘maigizo tu.’ Na nisipo fanya haya na kuyaishi ni dhahiri kwamba
neema ya Bwana wangu Yesu Kristo haipo pamoja nami. Nitakuwa ninamwakilisha mtu
mwingine au kitu kingine katika maisha yangu hapa duniani. “Ndugu
zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina,” Gal
6:18
Mzee Makokoto hujikimu
yeye na familia yake ya watu saba kwa kazi ya kupasua mawe na kuyapondaponda
hadi kuwa kokoto. Na kazi hii ndiyo sababu ya jina lake. Siku mmoja jua likiwa
linawaka sana hakuweza kuendelea na kazi ile, hivyo ilimpasa atafute mahali
penye kivuli na kusubiri ‘jua lisogee kidogo.’ Basi umbali kidogo karibu na
eneo lile kulikuwa na mti wa mzambarau na pembeni yake kulikuwa na mmea wa boga
ukiwa na maboga mengi na makubwa.
Mzee Makokoto akiwa
anastaajabia mmea ule teketeke na maboga yake, alianza kumkosoa Mungu na
kusema, “kumbe tufauti za kimaisha siyo kwetu tu wanadamu, hata na mimea pia?
Ona boga hili teketeke limepewa tunda kubwa kweli, na mti huu mkubwa wa
zambarau umepewa vitunda vidogo kama gololi.” Mara akiwa katika tafakari ile,
punje moja ya zambarau ilidondoka sambamba na jicho lake la kushoto. Mzee
Makokoto akiwa na nyundo yake ya kupasua mawe aliruka na kuhama kabisa kwenye
kivuli kile cha mzambarau. Kisha akajiuliza, “kama boga lingekuwa ndilo tunda la
huu mzambarau nini ingekuwa hatma ya jicho langu? Je, ningeweza kweli kufanya
kazi hii ya kuponda kokoto nikiwa chongo na jua hili kali hivi? Ningekuwa mgeni
wa nani na ugumu huu wa maisha unaozidi kila siku?”
Baada ya takakari ile,
Mzee Makokoto alipiga ishara ya Msalaba na kusema, “Asante Mungu kwa kulinusuru
jicho langu. Utukuzwe milele! Mzee Makokoto aliondoka mahali pale na kuendelea
na kazi yake huku akijawa furaha. Ndugu yangu, bila shaka nawe pamoja na
mahangaiko yako, bado unayo mengi ya kusema kama Mzee Makokoto, “Asante Mungu
kwa……Utukuzwe milele!”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini
mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu
Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa
ulimwengu,” Gal 6:14
Tusali:-Yesu Asante kwa mema yote unayonijalia.
Hakika ni mengi ajabu. Sifa na Utukufu ni yako Milele na Milele. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario