viernes, 29 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 18 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 18 YA MWAKA-C
Somo I: Mhu 1:2; 2:21-23
Zab: 95:1-2, 6-7, 8-9
Kol 3:1-5, 9-11
 Injili: Lk 12:13-21
Nukuu:
 “Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu,” Mhu 2:21 

 “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1 

 “Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11 

Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14

Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo,” Lk 12:15

Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21

TAFAKARI: “Na jina lake Mataifa watalitumainia. Kristo ni yote, na katika yote.”

Wapendwa wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 18 ya mwaka “C” wa Kanisa. Tunapoyatazama masomo yetu ya leo tunazamishwa na Mama Kanisa kutafakari na kushirikishana kweli hii, kwamba, “Na jina lake Mataifa watalitumainia. Kristo ni yote, na katika yote.” Somo la kwanza kadiri ya Mhubiri, anayaona maisha si kitu wala chochote, bali ni ‘ubatili mtupu, ubatili mtupu, mambo yote ni ubatili,’ Mhu 1:2. Swali la msingi na la kujiuliza ni hili, nitawezaje kuitamani hiyo kesho kama sioni maana ya leo? Kama tumeumbwa ili tuishi milele, na Mungu akaona inafaa tuwepo ulimwenguni hapa, iweje tena niwe na mawazo haya kwamba mtu apata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua?’ Mhu 2:22.

Ndugu yangu, ni vyema nikaelewa kwamba vyote vinavyoonekana na visivyoonekana alivyoviumba Mungu kwa asilimia kubwa vinamlenga huyu mwanadamu aliyepewa heshima ya juu kabisa kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni katika mantiki hiyo, “Bwana aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18. Pamoja na mahangaiko na sintofahamu za maisha, ulimwenguni hapa pana kusudio la Mungu katika maisha yetu. Hapa ndipo uwanja wa kujua kusudi la kuumbwa kwetu na kujiandaa katika uzima ule wa milele. Na kwa kusudi la kuumbwa kwetu, hapa duniani ndipo tutakapo mjua Mungu, mpenda Mungu, mtumikia Mungu, na mwisho kurudi kwake mbinguni.

Ni kweli kabisa hapa na pale tutakatishwa tamaa, ila isiwe sababu ya kutokuona kusudi la Mungu katika upana wa uumbaji wake. Ufanyalo zuri leo, kesho laweza kufutwa kwa hila tu na kutoweka. Ila pamoja na hali hiyo, hatuwezi kufuta wema wa lililo jema mbele ya macho ya Mungu. Na hata jambo hilo linapobaki katika historia yake, huendelea kuwa somo kwa vizazi na vizazi. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu,” Mhu 2:21. Pamoja na mtizamo huu wa Mhubiri, maisha ni zaidi ya yale tuyafanyayo leo au kuyamiliki. Jambo la maana na muhimu ni kuwa huru nje ya yale tuyafanyayo na kuyamiliki. Tusipojibadua katika haya, maisha hukosa maana na hasa pale yanapotoweka yale tuyafanyayo na kuyamiliki. Ni swala la wakati kwamba itafika mahali hatutaweza kufanya chochote.

Je, katika hali hiyo ya kutokufanya chochote, utu wetu utatoweka kwa sababu tu wazee? Utajiri na mali tulizonazo tumemilikishwa kwa muda tu na wakati ukifika watamilikishwa wengine, nasi tutaondoka kama tulivyokuja bila chochote kwa sababu,  Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Ndugu yangu, tunapojimilikisha yale ambayo kwa asili siyo yetu, mwisho wa siku huwa ni ubatili na masikitika makubwa.Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili,” Mhu 2:23.

Wapendwa Taifa la Mungu, Injili ya leo, inatutaka tutafakari kwa undani maisha yetu na uhusiano wake na mali. Ndugu moja anamwendea Yesu mbele ya mkutano na kumwamuru amwambie ndugu yake amgawie urithi wao, Lk 12:13. Badala yake, Yesu anamuuliza swali la msingi na la kushangaza. Akamwambia, Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Lk 12:14. Swali hili linatutaka kuweka bayana nini maana ya maisha yetu na mahusiano yake na mali. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa leo kwamba maisha yako ni dhamana hapa duniani, na mali tulizo nazo tumeazimwa tu kwa muda. Mali ni za Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, muda wetu hapa duniani na nguvu zetu, akili, nafsi, mahusiano, na mali zetu zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri. Sisi ni mawakili wa yale Mungu atupayo. Wazo hili la uwakili huanza na utambuzi wa kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu na kila mtu duniani. "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake." Zab 24:1. Hivyo Yesu anamtahadharisha kijana yule na sisi pia kwa kutuambia kwamba, “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo,” Lk 12:15. Uzima wako na furaha yako ya kweli haitokani na wingi wa mbali ulizokuwa nazo. Kwa maana nyingine, vitu hivyo kwa kuwa navyo kwa wingi havituhesabii haki mbele za Mungu. Ndugu yangu, kama humwamini yule aliyefufuliwa kutoka wafu yaani, Kristo Yesu, wingi wa utajiri wako ni bure kabisa kwa sababu mali zote ni za Bwana ukiwa na wewe mwenyewe. Mtume Paulo anasema, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu; ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki,” Rum 4:24b-25. Hivyo wingi wa mali zako bila Imani juu ya Kristo mfufuka ni bure.

Hakika "hatumiliki" chochote kwa wakati wetu mfupi wa kuishi duniani. Mungu "hutukopesha" dunia tunapoishi hapa. Ilikuwa mali ya Mungu kabla hujaja, na Mungu anamkopesha mtu mwingine ukifa. Je unabisha? Ndugu, ukweli ni kwamba unaifurahia dunia hii kwa muda mfupi tu. Injili ya leo inatuambia kwamba asiyefahamu ukweli huu ni MPUMBAVU kama mkulima yule tajiri aliyetaka kufurahisha nafsi yake kwa kusema, ‘pumzika basi, ule, unywe, ufurahi,” bila kujua ni nani aliye sababu ya uzima wake. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu,” Lk 12:20-21. Ndugu yangu bado furaha yako ipo kwenye mali?

Mungu alipowaumba Adamu na Hawa, aliwakabidhi uangalizi wa uumbaji wake na akawaweka kuwa wadhamini wa uumbaji wa mali yake. "Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi," Mwa 1:28

Kazi ya kwanza ambayo Mungu aliwapa wanadamu ni kuangalia na kutunza "vitu" vya Mungu duniani. Wajibu huu haujaondolewa kamwe. Ni sehemu ya malengo yetu leo. Kila kitu tunachokifurahia yapasa tukione kama dhamana ambayo Mungu ameiweka mikononi mwetu. "Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu." 1Kor 4:2

Yesu mara kwa mara anaonyesha kuwa maisha ni dhamana na anatoa mfano wa talanta, mfanya biashara alikabidhi watumishi utajiri wake alipo safiri. Aliporudi alitathmini kazi ya kila mtumishi na kumpa ujira sawasawa na kazi yake. Yule tajiri anasema,  "vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako," Mt 25:21.

Ndugu, mwisho wa maisha yako duniani utatathminiwa kulingana na ulivyotumia yale Mungu aliyokukabidhi. Hii inamaana kwamba mambo yote unayofanya, hata yale mambo madogo madogo ya kila siku, yana matokeo ya umilele.

Kama utaona mambo yote kuwa dhamana, Mungu anaahidi zawadi tatu katika maisha ya milele. Kwanza, utapewa "uthibitisho". Atasema, "kazi nzuri! umefanya vyema." Kisha "utapandishwa" daraja na utapewa jukumu kubwa katika umilele: "nitakuweka uwe mwangalizi wa vitu vingi." Na mwisho utakaribishwa katika "karamu." "Njoo ushiriki katika furaha ya Bwana wako.

Watu wengi wanashindwa kufahamu kuwa pesa ni jaribu na dhamana toka kwa Mungu. Mungu anatumia pesa kutufundisha kumtegemea; na kwa watu wengi fedha ni jaribu kuu kupita yote.Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi,” 1Tim 6:10. Mungu anaangalia jinsi tunavyotumia pesa ili kupima jinsi gani tunaaminika. "Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?" Lk 16:11. Huu ni ukweli wa muhimu sana. Mungu anasema kuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya ninavyotumia pesa zangu na hali yangu ya kiroho. Jinsi ninavyotawala pesa zangu "utajiri wa dunia" ni kigezo cha kiasi gani Mungu anaweza kunikabidhi baraka za kiroho, "utajiri wa kweli".

Hebu jiulize ndugu yangu, Je, namna ninavyotumia fedha zangu yaweza kumzuia Mungu kufanya mambo zaidi maishani mwangu? Je, ninaweza kuaminiwa katika utajiri wa kiroho? Wapo watu wachache katika mazingira na maisha yetu, waliweza kuthibitisha uhusiano wa moja kwa moja baina ya walivyotumia pesa zao na hali ya kiroho ya maisha yao. Pesa au utajiri wao havikuwa kipao mbele katika maisha yao. Watu na maisha yao ya dhiki ilikuwa kero zake na mara zote alijitahidi kutafuta suluhu ya kero hizo za watu. Mtu wa namna hii ndiye tunayeweza kuumpa dhamana ya kusimamia mali ya umma. Alilolisema ndilo alilolifanya. Dhima hii ndiyo iliyompa nguvu ya Kimaadili. Mfano wa mtu huyu ni Baba yetu wa Taifa; Julius Kambarage Nyerere, aliyetutangulia katika haki. Apate rehema kwa Mungu apumzike kwa amani. Sina shaka katika maisha yake. Ipo siku atapewa uangalizi mkubwa zaidi na Mama Kanisa na kuwa Mwombezi wetu-Mtakatifu.

Yesu Kristo anasema, "na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi." Lk 16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka uwajibike zaidi.

Ndugu yangu, pamoja na kuishi leo na sasa na changamoto zake, yanipasa kujua shabaha ya maisha yangu ipo wapi. Kama Mkristo na mfuasi wa Kristo, Kristo ndiye shabaha maisha yangu. ‘Na jina lake Mataifa watalitumainia. Kristo ni yote, na katika yote.’

Kwa nini Kristo ndiye shabaha ya maisha yako kama Mkristo na mfuasi wake? Ndugu yangu, wakati fulani wanafunzi wa Yohana Mbatizaji walimwona Yesu akiwa anabatiza, nao walimwendea Yohana Mbatizaji ili kujua juu ya kile afanyacho Yesu, na nafasi yake katika ufahamu na umaana wake. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni,” Yoh 3:27. Kwa jibu hili la Yohana ilithibitisha Kristo ndiyo njia sahihi na hapana shaka juu yake. Pamoja na ukweli kwamba vyote vilifanyika kwa huyo (NENO-CHRISTO); wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3, kwa kinywa chake Yesu Kristo analithibitisha hili na kusema, hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu,” Yoh 14:65. Ni ndani na katika Kristo kuna njia, kweli, na uzima. Naye Yesu anasema,Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, nje ya Kristo una nini kilichochako zaidi ya dhambi zako?

Kristo ndiye shabaha ya maisha yako unapotazama fumbo zima la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Tendo hili la UFUFUKO wa Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo fursa ya pekee kwa wale wote wamuaminio Kristo, ambaye ndiye mwisho wa shaka yote. Naye Mtume Petro analisema tukio hili katika undani na upana wake. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:12. Ndugu yangu hapo ulipo Kristo yupo? Hapo ulipo usalama upo bila Kristo? Ndugu yangu hata nikipoteza vyote katika ulimwengu huu kama ninaye Kristo ndani ya maisha yangu sitokuwa nimepungukiwa na chochote.

Na hivi ndivyo asemavyo Mtume Paulo hasa kwa wale wanaaminio ufufuo wa Kristo, na upya wa maisha yao ndani na katika Kristo; Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Tendo la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo linatusukuma toka ndani ya mioyo yetu na imani yetu kuyatafuta yaliyo juu kule Kristo aliko. Kwa Mkristo yeyote hapa duniani asipolifanya jambo hili kuwa kielelezo cha maisha yake, basi ajue kwake ufufuko hauna maana ye yote. Mtume Paulo anasema hivi kuhusu ufufuko, “tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure,” 1Kor 15:14. Ufufuko wa Kristo ndiyo kiini cha Imani yetu.

Ndugu yangu, mambo yaliyo juu aliko Kristo ni yale yote yanayotuongoza huko aliko, yaani ufalme wa mbinguni na umilele wake. Kwa maneno mengine ni kuvaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba,” Kol 3:10. Utu huu upya ni tendo la kupiga vita aina zote za dhambi kwa sababu dhambi ufifisha na kuzorotesha utu wetu wa ndani ambao ni nafsi na roho.

Jambo la pili na lenye maana kabisa katika maisha ya kiroho ni kufikiri muda wote yale yaliyo juu na siyo yaliyo katika nchi. Hapa Mtume Paulo anaongelea sana swala la nafsi ya mtu. Nafsi inapoegemea zaidi katika mwili matokea yake ni anguko kuu na mwisho wa matumaini yote ya kuurithi ufalme wa Mungu. Hapa ndipo binadamu anapoonekana mara zote kufikiri yaliyo katika nchi na yasiyo na umilele. Kuepukana na kadhia hii, Mtume Paulo anatoa angalizo kwa kusema,  Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu,” Kol 3:5-6. Ghadhabu ya Mungu hapa ni kuukosa ufalme wake na kuangamia milele pasipo kuwa na nuru yake.

 Ndugu yangu, pale nafsi inapoegemea roho, ndipo tunapojazwa tumaini jipya na kufanywa upya siku kwa siku.Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Kuishi ukweli huu ndani na katika Kristo ni kuchuchumilia cheo chetu halisi, yaani UTAKATIFU WAKO! Cheo hiki kila mmoja wetu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ndiyo stahili yake, na anaipata kwa kuishi kweli kwa mafundisho ya Kristo, na kutimiza ukweli huo kwa uaminifu. Hivyo hasili zetu katika maana ya mila na desturi zetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu hazina uhalalisho wowote katika cheo hiki kama hatunaye Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Ni kwa sababu hii Mtume Paulo anawapa angalizo watu wa nyakati zake, na sisi pia kwa kusema, hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11.

Wapendwa katika Kristo, angalizo la mtindo huo alilotoa Mtume Paulo na lenye kutuweka katika mstari sahihi kuelekea urithi tulioandaliwa na wenye hadhi ya cheo chetu, ndiyo changamoto kubwa kama wafuasi wake Kristo. Na changamoto ya Mkristo ni kupenda hata pale pasipopendeka, ikiwa kipimo cha upendo huo ni kupenda bila kipimo. Kwa kupenda kwa mtindo huu, mimi na wewe tuwe tayari kuyapokea yale aliyoyapokea Kristo Yesu, ila kwa sasa na kwa tumaini kubwa ni kwamba, Kristo kesha yashinda mateso hayo, Kristo kesha ushinda Msalaba.

Ni katika pendo hilo Kristo anapomponya mtu yule aliyepooza mkono, Mt 12:13, Mafarisayo wanafanya shauri la kumwangamiza, Mt 12:14. Ila kwa mbinu hizi hawatafanikiwa kama ulivyokuwa utabiri wa Nabii Isaya, akisema,Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu,” Mt 12:17-18. Kumbe usalama wangu na wako upo kwa Kristo mwenyewe, na huu ndio ule  “Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda,” Mt 12:20. Naam, Na jina lake Mataifa watalitumainia,” Mt 12:21. Je, bado una mashaka na Kristo Yesu?

Upendo Katete, binti aliyetoka familia masikini sana ya Bwana na Bibi Lazaro Katete, alisoma kwa shinda sana hadi kufikia kiwango cha kuwa Daktari bingwa wa magonjwa ya akina Mama na Watoto. Kuhitimu masomo yake hayo ilikuwa mwanzo mpya wa maisha mapya katika familia yao. Baada ya miezi sita ya kuajiriwa kwake, ulilipuka ugonjwa wa Ebola katika nchi yake na hivyo aliona ni wakati wa kuitumia elimu na utaalamu wake, na kama sadaka katika nchi yake.

Baada ya mwenzi mmoja akiwa anatoa huduma hiyo katika kambi rasmi ya wagonjwa wa Ebola, hali ilibadilika ghafla kwani naye alionekana ana dalili za kuambukizwa ugonjwa huo. Kambi nzima iliingiwa na hofu, si kwa sababu ya ugonjwa ule ambao kwa wakati ule ulikuwa si kitu cha kuepukika, bali waliingiwa hofu kumwana mtu ambaye alikuwa karibu nao na kujitoa bila kujibakiza kuwahudumia hawezi tena kufanya hivyo.

Na baada ya wiki mbili, Upendo Katete alifariki. Hakika lilikuwa pigo kubwa sana kwa jamii ile na hasa wazazi wake na familia yake kwa sababu nuru ile iliyokuwa inang’aa ilizimika ghafla. Familia yake haikupata hata nafasi ya kumwona na hata kumpa heshima ya mwisho kwa kuuaga mwili wake, kutokana na hathari za wao pia kuambukizwa.

Baada ya miaka mitano, na kwa kutambua mchango wake na historia ya maisha yake, jamii yake na msaada kutoka nje ya nchi ile, waliamua kujenga hospitali kubwa sana kwa heshima yake yenye kutoa huduma kwa akina mama na watoto. Kumbe tukio hili linatukumbusha maneno haya ya Yesu,  Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Ndugu yangu, ni wazi leo Upendo Katete hayupo tena katika hali ya kushikika, ila bado na kwa kiasi kikubwa anaendelea kuishi na kutoa hudumu kwa jamii yake kupitia hospitali hii; “Upendo Katete Hospital.”

Tumsifu Yesu Kristo

Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11


Tusali:-Ee Yesu, maisha yetu yana maana ndani na katika wewe. Tupe ujasiri wa kuyatafuta katika maisha yetu kila siku yale ya juu pale ulipo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario