JUMAMOSI WIKI YA 17 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 26:11-16, 24
Zab: 69:15-16, 30-31, 33-34
Injili:
Mt 14:1-12
Nukuu:
“Ndipo
hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili
kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu,”
Yer 26:11
“Ndipo
Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma
kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia,”
Yer 26:12
“Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia
gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye,” Mt 14:3
“Kwa
sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye,” Mt 14:4
“Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake,
na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma
mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani,” Mt 14:9-10
TAFAKARI:
“Kuwa tayari na jiandae kwa kulipa gharama pale utakapo simama katika kweli na
haki.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo kwa namna ya pekee tunapotafakari ule ‘utayari wa kulipa gharama pale
utakapo simama katika kweli na haki,’ Nabii Yeremia na Yohane Mbatizaji ndiyo
dira na kielelezo cha kweli hiyo. Ipo vita kubwa sana kati ya giza na mwanga.
Popote pale kinapokuwepo kimoja, ni kwa namna hiyo hiyo kwamba kingine kipo
vitani kukipindua kile kinachoonekana. Hata kama hakionekani haimaanishi kwamba
hakipo.
Na sasa tuanze kwa
kumtazama Nabii Yeremia kwa kile alichokisimamia katika kweli na haki, na
madhara anayokumbana nayo. Utabiri ule wa Yeremia ambao ni ujumbe kutoka kwa
Mungu, Yer 26:4-6, unazua taharuki na kufikia hatua ya makuhani na manabii
kuitoa roho yake. Ukitaka urafiki na ulimwengu huu, waambie watu kile
wanachopenda kusikia. Hapa utapigiwa magoti na makofi kuanzia walevi hadi
wafalme wa ulimwengu huu. Kwa vile Yeremia alisimama katika kweli na haki ya
Mungu, mambo yalimwendea ndivyo sivyo katika mizania ya kibinadamu. “Ndipo hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na
watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji
huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu,” Yer 26:11. Kutokana na mtafaruku huu,
Yeremia haachi kuwaeleza chanzo na sababu ya ujumbe ule wa Mungu. “Ndipo
Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma
kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia,”
Yer 26:12. Mara nyingi hata baada ya kuujua ukweli kwa vile twapenda kuendelea
katika uovu, hutumia nguvu kubwa kuushikilia uovu, badala ya kubadilika na kuwa
mikono salama zaidi.
Ndugu
yangu, katika hali na mazingira kama haya, yakupasa kujiandaa vizuri kwani
vitisho huwa vingi sana ili tu kukukatisha tamaa na kurudi nyuma. Je, katika
hali na mazingira haya tujisalimishe na kuifunga midomo yetu? La hasha! Pamoja
na vitisho hivyo, Yeremia anasimamia maneno yake, na kuwaambia, “tengenezeni njia zenu, na matendo yenu,
mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya
aliyoyanena juu yenu,” Yer 26:13. Licha ya
kuyasimamia maneno yake, Yeremia anataka waone ukweli kama ulivyo kwa sababu
yote hayo ni kwa faida yao wenyewe. “Lakini
kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa
mema na haki mbele ya macho yenu,” Yer 26:12. Penye ukweli uongo hujitenga. Na
hivi ndiyo asemavyo Yeremia, kwamba, “Lakini
jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa
juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana
amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia,” Yer 26:15. Huu ni ujumbe mzito sana kwa wale
watesi wake Yeremia. Na walioguswa na neno lile waliuona ukweli na kusema, “Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema
nasi katika jina la Bwana Mungu wetu,” Yer 26:16b. Na pona ya Yeremia ilikuwa
hivi, “mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani,
alikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe,” Yer 26:24.
Mpendwa, katika Injili ya leo tunaona hathari za
matumizi mabaya ya madaraka yanayosababisha maafa makubwa kwa wale watetezi wa
haki katika jamii inayowazunguka. Ni jambo la hatari sana kuwa na kiongozi
anayeongozwa na mihehuko ya hisia zake, huku akitegemea sifa kutoka kwa watu.
Kiongozi mwenye misukumo hii ya kihisia ni rahisi sana kuzikanyaga haki za wale
anaowaongoza. Hii ni pamoja na kuwa kutokuwa makini katika ahadi azitoazo
kiongozi mbele za watu. Herode anamwahidia binti yake chochote apendacho baada
ya kucheza vizuri na kuufurahisha umati wa watu siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa
kwake. “Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote
atakaloliomba,” Mt 14:7. Mfalme Herode anajifunga kwa kauli yake mwenyewe.
Mfalme Herode hakuwa na lakusema binti yake alipokitaka kichwa na Yohane
Mbatizaji zaidi ya kutimiza ahadi yake na kulinda heshima yake kama kiongozi. “Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya
viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru
apewe,” Mt 14:9. Je, ni watu wangapi huwa kafara kunakotokana na utafutaji wa
sifa na umaarufu wa baadhi ya viongozi wetu?
Ni mbaya sana kutafuta
umaarufu kwa kukanyaka haki za watu, na hasa wale ambao wapo kinyume chetu
kutokana na matendo yetu yasiyo haki na hofu ya Mungu. Yohane Mbatizaji ni
mhanga wa viongozi wale wenye kupenda sifa na umaarufu. Kosa la Yohane
Mbatizaji ni kusimama katika kweli. Umauti unamfika Yohone Mbatizaji kwa sababu
alimwambi Mfalme Herode “Si
halali kwako kuwa naye,” Mt 14:4. Wapo wahanga wengi wa mtindo wa Yohane
Mbatizaji katika familia zetu, Jumuiya zetu ndogondogo za Kikristo, Jumuiya
zetu za kitawa, Makanisani mwetu, sehemu zetu za kazi, na mbaya zaidi leo
katika mfumo mzima wa utawala.
Herodia
ameitumia nafasi hii ipasavyo kumwangamiza mtesi wake ambaye alikuwa kero kubwa
hasa pale alipomsaliti mumewe na kuishi na Herode. Kamwe hatuwezi kuhalalisha
kosa kwa kutenda kosa. Tunachofanya ni kupata haueni ya muda mfupi tu, ila
dhambi na kusutwa kwa ndani hubaki na hata kuongezeka kwa sababu hapa tunacheza na haki ya mtu katika kweli, na kilio kisichokoma cha damu ya mwenye haki. Ni
vyema tukayatafakari kwa kina matendo yetu katika kupima faida na hasara zake.
Hakika hutobaki salama kwa kufanya dhuluma kwa mtu mwenye haki. Yohana
Mbatizaji anawawakilisha wengi leo katika jamii yetu. Wapo wengi leo
wamenyamazishwa hata kuuwawa kwa sababu tu za kisiasa na hasa pale waliposema
‘hii halili jambo hili kuwa kama lilivyo.’ Wapo pia wengi walionyamazishwa na
hata kuuwawa kwa vile tu walijaribu kuufichua uovu katika maana ya kugusa
maslahi ya watu fulani.
Wapendwa
tuutafute kwanza ufalme wa Mbinguni na mengine yote tutapewa kwa ziada.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Naye
mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale
walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe;
akatuma mtu, akamkata
kichwa Yohana mle gerezani,” Mt 14:9-10
Tusali:-Ee Mungu,
tujalie hekima na busara katika uongozi. AminaT
No hay comentarios:
Publicar un comentario