jueves, 7 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 14 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 14 YA MWAKA-C
Somo: Isa 6:1-8
Zab: 93:1ab, 1cd-2, 5
Injili: Mt 10:24-33
Nukuu:              
Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi,” Isa 6:5 

Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa,” Isa 6:6-7 

Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi,” Isa 6:8 

 “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 10:32-33

TAFAKARI:Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, wito wa Nabii Isaya unaonyesha mtazamo wa Mungu na jinsi tunavyojitazama kama watu tusiostahili kwa yale Mungu anayotufikiria. Hakika upendo, huruma, msamaha, haki, na upole wa Mungu hatuwezi kuufananisha na kitu chochote. Mungu atabaki kuwa Mungu kwa milele yote! Isaya anapotazama mwaliko wa Mungu na kile alicho anaona ni vitu viwili tofauti. Naye anasema, “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi,” Isa 6:5. Pamoja na historia zetu zilizombaya, kushindwa kwetu katika maisha, na kudharauliwa kwetu, bado Mungu anasema, Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba,” Mt 10:27. Tuitazamapo historia ya wokovu wetu, ipo mifano mingi na mazingira mbalimbali ambapo Mungu ukiinua kile kilicho dhaifu na kunyenyekeza kile kinachojikuza.

Mungu hutumia watu wa kawaida kabisa kulifikia lengo lake Takatifu. Nabii Isaya ni mmoja wapo, hasa anapojitazama mazuri na mabaya yake. Bila shaka mimi na wewe tunajisikia kama Nabii Isaya. Mapungufu na udhaifu wewe visiwa ukuta wa kuona nuru ya Mungu. Tusimame katika kweli na haki hata kama udhaifu upo. Huku ni kuishi maisha ya ufufuko, yaani, “mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Hivyo, udhaifu wangu uwe changamoto na nguvu ya kunisukuma kufanya vizuri zaidi siku kwa siku. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Mtume Paulo kwamba, “napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10. Kumbe katika hali zote na udhaifu wangu, Kristo awe kielelezo changu cha kufanya vizuri zaidi. Yeye kesha ushinda Msalaba.

Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, ‘tuambiwalo katika giza, tuliseme katika nuru; na tusikialo kwa siri, tulihubiri juu ya nyumba.’ Neno hili la maanisha hivi; pamoja na ‘shindwa yako bado una kitu cha kufanya na kubadili historia yako mbaya. Hivyo kitumie kitu hicho katika ukamilifu wake na hadi mwisho wake, na yote yatakuwa mapya.’ Huu ndiyo ujumbe mahususi.

Mpendwa katika Kristo, unapojiachia kwa Mungu bila kujibakiza katika maana ya kuona kweli kama ilivyo na siyo kama ulivyo, ndipo utakaso unapokujilia na kufanywa upya mbele ya Mungu, na kuhesabiwa haki kwa mastahili ya Mungu mwenyewe. Isaya anayaendea mabadiliko haya katika maisha yake kwa sababu Mungu kesha pendezwa naye. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa,” Isa 6:6-7. Ni mara ngapi tunajiona watu tusiofaa mbele za watu na kujipoteza kabisa? Ndugu yangu, hata kama ulimwengu wote utakuchukia, Mungu hubaki na upendo wake kwako wa ajabu. Embu itazame mikono ya Yesu pale msalabani. Yesu anakuambia, ‘tazama nimeyakubali haya yote na hata kufa kifo cha aibu msalabani kwa sababu nakupenda kupita vyote.’ Hakika Mungu anatupenda upeo, Yoh 13:1.

Wapendwa wana wa Mungu, utaisikia sauti ya Mungu ndani yako unapo utafakari upendo huu wa Mungu ulio wa ajabu. Isaya anaisikia sauti ya Mungu ndani yake, na kusema, Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi,” Isa 6:8. Isaya anazaliwa upya mwili na roho na sasa yupo tayari kuyafanya mapenzi ya Mungu. Huwezi kukutana na Mungu katika maisha yako naye akakuacha kama ulivyokuwa mwanzo.

Ndugu yangu, unapomfuata Kristo kwa ukaribu, unakumbushwa kuishinda hofu na woga. Unayepaswa kumwogopa ni Mungu mwenyewe. Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana,” Mt 10:26. Ndugu yangu, hata kama leo tutafinywa uhuru wetu tunapoishi imani yetu, kweli hiyo ipo siku itajulikana wazi kwa watesi wetu. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28

Tunapolishinda giza kwa matendo yetu ya mwanga, kutatutaka kila mara kusimama katika kweli na kumshuhudia Kristo pasipo haya. “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 10:32-33. Maisha yetu na ukiri wetu mbele za watu kuhusu Kristo ndiyo kweli hiyo itakayo jidhihirisha mbele za Mungu siku ya hukumu ya mwisho.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi,” Isa 6:8b


Tusali:-Ee Yesu Mwema, nitazama na kunipa nguvu hata katika udhaifu wangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario