JUMATANO
WIKI YA 14 YA MWAKA-C
Somo: Hos 10:1-3, 7-8, 12
Zab: 105:2-3, 4-5, 6-7
Injili: Mt 10:1-7
Nukuu:
“Israeli
ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri
iyo hiyo ameongeza madhabahu zake,” Hos 10:1ab
“kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri
iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri,” Hos 10:1cd
“Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya
pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt
10:1
“Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa
mbinguni umekaribia,” Mt 10:7
TAFAKARI: “Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili,” Hos 10:12a
Wapendwa wana wa Mungu, Mungu akiwa ndiye udongo na nchi yenye rutuba,
wana wa Israeli wanafananishwa na
mzabibu. Hivyo, “Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi
wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake,” Hos 10:1ab. Ni
kweli isiyo shaka kwamba, mmea hukua na kuzaa kadiri ya kipimo na uwezo wake
pale unapostawi kwenye udongo mzuri na wenye rutuba. Itakuwa kituko cha hali ya
juu kama mahitaji yote ya mmea yamekidhiwa, na mmea huo mwisho wa siku
kutokufikia lengo lake la kuzaa matunda mengi na mazuri. Ni “kwa kadiri ya wema
wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri,” Hos 10:1cd. Kwa hali ya kawaida tunategemea wewe na mimi
uliye na hofu ya Mungu kutenda kadiri ya sifa ya Mungu, yaani, haki, amani,
upendo, huruma, na msamaha. Kinyume chake ni kuasi kuliko wazi katika maana ya
kutokuzaa matunda mema kulingana na yale Mungu aliyokukirimia bure na kwa upendo.
Ni kutokumcha Bwana kuliko kwa wazi, na mfalme au mwenye dhamana katika umma
katika kweli hii hata hesabiwa haki. “Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi Bwana,” Hos 10:3a. Mfalme
au kiongozi yeyote yule na kwa nafasi yoyote ile pamoja na mambo yake mengi, ni
alama ya ‘umoja na mshikamano kwa umma ule anaoungoza.’ Kiongozi mbaguzi na
mwenye makundi hamwakilishi Mungu.
Hathari
za kiongozi mwenye ghiliba kama hii huonekana mara. Miiba na mbigili huonekana
kwenye himaya yake kwa sababu ndivyo visukumavyo fikra na utendaji wake. Hapa
ndipo kwenye kulia na kusaga meno, na ‘tungejua nyingi’ zisizo na idadi kwa
sababu, “mwiba
na mbigili imemea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na
vilima, Tuangukieni,” Hos 10:8b. Kiongozi asiyejifunza kupanda katika haki na
badala yake kupanda katika chuki na visasi, mavuno yake ni uharibifu. Hivyo
ndugu zangu ‘tupande katika haki, ili tuvune kwa fadhili,’ Hos 10:12a.
Kwa
mantiki hiyo, ni vizuri kutambua pale tulipowaumiza wenzetu, au mwenzako na kujaribu
kwa namna yoyote ile kupaponyesha. Hili ni jambo la muhimu sana tunapoishi kama
familia, au jumuiya yoyote ile ya Kikristo. Kutambua kosa na kufanya juhudi ya
kuleta uponyaji, kitendo hicho hutuponya pia. Agizo la Yesu kwenye injili ya
leo linatupa fursa ya kupambana na uovu bila kushindwa. Yesu “akawaita
wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na
kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt 10:1. Hapa pia tunaalikwa
kuushinda uovu kwa kutenda mema. Kama asemavyo Mt. Agustino; “ovu ni kutokuwa
na mafaa,” kushinda lililo ovu ni kutenda lililo jema.
Ndugu
yangu unayesafiri nami sasa, ‘misioni’ yetu hapa duniani kama watu wenye hofu
ya Mungu ni kuwarudisha kundini wale waopotea au kukwazika kutoka na utendaji wetu
wa awali au sasa. Ni mwaliko pia wa kujisahihisha pale tunapokosea. Yatupasa
sana kuepuka kishawishi kile cha kusema ‘mkubwa na mwenye madaraka au cheo
hakosei.’ Kasumba hii ni saratani mbaya sana katika utume wetu kama Kanisa
mahalia na taasisi yoyote ile ya kiraia. Kama sisi ni binadamu, na ndivyo
tulivyo, basi kukosea kupo. Kama kukosea kupo, kutambua na kujirekebisha ndipo
kunakotuhesabia haki mbele ya Mungu juu ya utendaji wetu na dhamana tuliyopewa
na Mungu mbele za watu na kondoo wa malisho yake. Hivyo Yesu anawatuma, na kuwaagiza, akisema, “Katika njia ya
Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia
kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli,” Mt 10:5-6. Yesu analifanya
hili kwa Thenashara wote ili hali akijua mmoja wao atamsaliti. Hivyo, “Simoni
Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti,” Mt 10:4. Je,
twaweza kuushinda uovu kwa kuzidi kutenda lililo jema na hata kuendelea kuona
uzuri kwa wenzetu hata kama tumegundua njama na hila zao? Katika jambo hili
bila shaka Yesu anatukumbusha thamani ya mtu na utu wake. Mt. Agustino anasema
hivi: “usimchukie mtu, bali zichukie tabia zake mbaya.”
Mwisho
kauli mbiu yetu: jana, leo, na kesho na iwe kuhubiri kusiko kikomo kwamba
ufalme wa mbinguni umekaribia. Tunalisema hili iliwa ndiyo kauli mbiu ya Kanisa
kama sakramenti ya wokovu wetu. Tunalihubiri hili kwa wengine tukijua kwamba
ndani yetu na nafsini mwetu twauona na kuuonja ufalme huo wau pendo, haki,
amani, upole, unyenyekevu, huruma na msamaha. “Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa
mbinguni umekaribia,” Mt 10:7
Tumsifu Yesu Kristo!
“Akawaita
wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na
kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt 10:1
Tusali:- Ee
Yesu Mwema, tujalie nguvu na neema ya kushinda uovu kwa wema. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario