lunes, 25 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 17 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI  YA 17 YA MWAKA-C
Somo: Yer 15:10, 16-21
Zab: 59:2-3, 4-5a, 10-11, 17
Injili: Mt 13:44-45
Nukuu:
Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi,” Yer 15:16

Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao,” Yer 15:19

 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile,” Mt 13:44

Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri,” Mt 13:45.

TAFAKARI:Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, ujasiri wa Nabii Yeremia umejengwa katika neno la Mungu. Ujasiri huu siyo tukio litokealo mara moja, bali lina hatua zake, na kila hatua huanzisha hatua nyingine. Kwa maana nyingine, kila hatua mpya huwa tokea la hatua iliyotangulia. Hivyo kwa ufupi ujasiri wa Nabii Yeremia unaonekana katika haya ayasemayo, Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi,” Yer 15:16. Ni muhimu kutambua mabadiliko ndani yako yenye mwelekeo wa kweli na haki ya Kimungu. Hii ni hatua ya kwanza katika Neno la Mungu. Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani,” Yer 15:10.

Na sasa tuzame ndani ya ujasiri ule wa Nabii Yeremia kama tokeo la neno la Mungu lililo yabadilisha maisha yake. “Maneno yako yalionekana,” inamaanisha, ‘kulisikia neno. Kulisikia neno ni hatua ya utofautishaji wa jumbe tuzisikiazo na kuchota maana, na tumaini la kweli la kule tuendapo tusipokujua. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu,” Yer 15:17. Hi ni hatua ya upembuzi wa kile tukisikiacho.

“Nami nikayala,” inamaanisha, ‘kulipokea neno,’ kwani huwezi kufanya hivyo kama hujalisikia neno. Kuyala maneno ya Mungu ni ‘neno la Mungu kama mwanga huanza kulifukuza giza ndani yetu na kuangaza nuru ile ya Mungu ambao ndio uhai na uzima halisi. Hivyo Mtume Petro katika hili anasema, Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing'aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu,” 2Pet 1:19

 “Na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu,” kunamaanisha ‘kulitafakari neno.’ Na unaweza tu kulitafakari neno kama ‘umelipokea neno’ hilo. Neno hili husababisha mitikisiko ndani ya nafsi yako.  Hapa ndipo unapotambua kwamba, mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?” Yer 15:18. Kumbe tunapozama katika tafakari ya neno la Mungu ambalo ndilo uzima ndani yetu, tunaanza kutambua ndani yetu mambo hayako salama.

Tunatambua yapo mambo ya kurekebisha ili neno liendelee kuwa uzima na uhai ndani yetu. Tunatambua pia vyanzo vya mashaka na wasiwasi wetu ambavyo kwa kiasi fulani ndiyo sababu ya kutokuwa na furaha. Hapa ndipo ninatambua nguvu na udhaifu wangu. Hapa ndipo ninapoanza safari mpya na kuelekea kule liliko tumaini la kweli. Hapa ndipo tunapomwamsha roho yule ndani yetu tukitambua mwili wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu. Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu,” 2Pet 1:20-21

 Hapa ndipo ninapotambua bila Mungu mimi si lolote wala chochote. Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao,” Yer 15:19

 “Shangwe ya moyo wangu,” yamaanisha, ‘utayari ule wa kulishirikisha neno la Mungu kwa wengine, na  furaha ya Mungu iliyopo ndani yangu. Furaha ni kama kikohozi huwezi kukizuia. Unaweza kushirikisha furaha hii kama tunda la tafakari ya kina. Hivyo ushirikishwaji wa neno la Mungu kwa wengine ni tokeo la tafakari ya kina. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana,” Yer 15:20. Kulishirikisha neno la Mungu kwa wengine ni tokea la kulitafakari neno la Mungu vyema ambalo wakati huu limeyabadili maisha yako. Hivyo tunalishirikisha neno la Mungu tunavyokomazwa na neno hilo na kuwa sehemu ya neno hilo kama ulivyo uhusiano wa maji na samaki. Bila maji hakuna uhai wa samaki. Hii ndiyo furaha tuishirikishayo kwa wengine. Uhai na uzima huu tuupatao mara baada ya kuzama katika tafakari ya kina, na kushirikisha uhai na uzima huo kwa wengine, ndiyo sababu ya ujasiri wetu na kuwa tayari kuwa mashahidi na washuhuda wa neno bila woga.

 “Maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi,” maneno haya yamaanisha ‘kuwa shahidi na shuhuda wa neno la Mungu hata ikibidi kufa.’ Hatua hii haitazami nafsi na ubinafsi wako, bali kweli na uzima ule wa neno ndani yetu, 2Pet 1:20-21. Kuwa shahidi wa neno bila woga ni kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yako, na kumwachia Mungu usukani wa maisha yako. Ni kuamini pasipo shaka maneno haya ya Mungu kwamba, Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha,” Yer 15:21.

Na hii ndiyo maana halisi ya maneno haya ya Yesu kuhusu ufalme wa mbinguni, yaani,Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile,” Mt 13:44. Hapa hatuna woga tena kwa sababu neno la Mungu lina mizizi imara ndani yetu na kutufanya sehema ya uimara na uhai huo. Hii ndiyo lulu ndani ya maisha yetu. Hakuna wakutunyang’anya kwani ndiyo uzima ndani yetu. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri,” Mt 13:45. Je, ni nani aliye tayari kuipoteza lulu hii nzuri ndani ya maisha yake? Kuipata lulu hii, na iwe sehemu ya thamani ya urithi wako, yaani, uzima na uhai ule niutamanio, sina budi kuzipitia hatua hizi tano muhimu, yaani; kusikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kwisho kuwa sehemu ya neno hilo kama shahidi na shuhuda.

Tumsifu Yesu Kristo!

Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha,” Yer 15:21


Tusali:-Ee Yesu Mwema, tuimarisha katika neno lako siku zote na tufanye mashahidi na mashuhuda wa neno hili katika kweli na haki. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario