sábado, 9 de julio de 2016

JUMAPILI YA 15 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 15 YA MWAKA-C
Somo I: Kumb 30:10-14
Zab: 69:13, 16, 29-30, 32-33, 35-36,
Somo II: Kol 1:15-20
Injili: Lk 10:25-37
Nukuu:
ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali,” Kumb 30:10-11 

"Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16

 “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni,” Kol 1:19-20

Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27

TAFAKARI:Fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28b 

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 15 ya mwaka “C” wa Kanisa. Mama Kanisa leo anatutafakarisha juu ya matendo ya uzima. Ikiwa ilimpendeza Mungu kutuumba kwa sura na mfano wake kama tokeo la pendo lake, Mungu wetu huyu aliye mwanzo na mwisho, na mwenye kuishi milele yote, lengo la kuumbwa kwetu ni kuishi milele. Kuishi kwetu leo na sasa katika ulimwengu huu kusukumwe na upendo. Na ‘fanya hivi nawe utaishi.’ Ni katika kupenda tunaishi kwa sababu tunajua lengo la kuubwa kwetu katika maana ya kumpenda Mungu na jirani, Mt 22:37-39. Na katika amri hivi mbili hutegemea torati yote na manabii, Mt 22:40. Ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali,” Kumb 30:10-11. 

Kuishi tena na tena ni ‘kupenda bila kipimo kama kipimo cha upendo,’ na ndivyo atufundishavyo Mtakatifu Augustino wa Hippo. Kielelezo cha upendo huu ni Kristo mwenyewe. Naye Yesu anasema, Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Kumbe nisipokuwa tayari kwa ‘upendo sadaka,’ ishi yangu inaulakini mkubwa. Kristo kwa kutupenda upeo, Yoh 13:1, aliutoa uhai wake ili mimi na wewe tuishi na kuhesabiwa haki kama wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake wa milele. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni,” Kol 1:19-20. Ndugu yangu, huyu ndiye Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na mbwembwe zote za mwanadamu hapa duniani, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujiuliza swali hili la msingi alilouliza mwana-sheria mmoja wa Kiyahudi kwa Yesu kuhusu uhai. Mwana-sheria huyu anamuuliza Yesu hivi; “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Lk 10:25. Msingi wa swali hili haupo kwenye uhai tu wa leo na kesho, bali uhai katika umilele wake. Tuelewe kwamba mwanadamu ameumbwa kuishi milele, na hayo ndiyo makusudi ya Mungu katika uumbaji wa mwanadamu. Tatizo kubwa la mwanadamu ni mbwembwe nyingi alizonazo akisahau kuwa muda aliopewa hapa duniani hausimami kumsubiri. Mhubiri anatuwasa na kusema, “mwanadamu hadumu katika heshima, bali amefanana na wanyama wapoteao,” Zab 49:12. Fahari ya mwanadamu ni yule aliyemuumba, yaani Mungu wake. Mengine yote ni mbwembwe tu! Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake. Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako,” Kumb 10:20-21. Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa kwamba utajiri wako, ufahamu wako (kiwango cha elimu ulicho nacho), umaarufu wako, nk, bila Mungu ni bure kabisa.

Yesu kabla ya kumjibu vizuri mwana-sheria yule wa kiyahudi alitaka kujua uelewa wake wa Maandiko Matakatifu (Torati) yanasema nini kuhusu uhai wa Milele. Mwana-sheria yule akamjibu kwa staha, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27. Yesu anaridhika na jibu hili na amamwambia hivi; “Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi,” Lk 10:28. Kuishi kwetu hapa duniani ambapo kunatupelekea kuishi milele baada ya kifo, kama wanadamu kwatuwajibisha kufanya kwa weledi mkubwa mambo makuu mawili.

Moja, mpende Mungu wako kwa moyo wako wote, roho yako yote, na nguvu zako zote. Kwa maana nyingine ni kutumia vyote Mungu alivyokujalia ili umpende na ubaki kumpenda daima. Afya yako njema, akili yako ya pekee, utajiri wako, na umaarufu wako hapa nduniani isiwe sababu ya kujitenga na upendo huu wa Mungu. Hayo Mungu aliyokujalia kwa namna ya pekee isiwe sababu ya kuwakejeli wenzako ambao kwa mtazamo wako wa kibinadamu waona hawastahili mema yoyote mbele ya uso wa Mungu. Ndugu yangu, hata yale tunayoyaona kwa macho yetu kama udhaifu wa mtu na wengine, Mungu wakati mwingine utumia udhaifu huo kutufundisha siri ya maisha na uhai tuliopewa na Mungu mwenyewe. Maisha  na uhai tuliyonayo ni mali na zawadi yake Mungu. Mimi na wewe tumepewa uhai huu na kuazimwa kwa muda tu hapa duniani kama sababu ya kuutumia vyema uhai huu ili tuishi milele baada ya muda ambao kila mmoja wetu kapewa kadiri ya mapenzi yake Mungu. “Maana siku zangu zinatoweka kama moshi, Na mifupa yangu inateketea kama kinga,” Zab 102:3.

Pili, nimpende jirani yangu kama nafsi yangu. Jirani yangu ni yeyote yule ninayekutana naye na wale wote wanaonizunguka, yaani, wahitaji na wasio wahitaji. Jirani yangu ni kama kioo cha kujitazama ukamilifu wangu mbele ya Mungu. Je, udhaifu wa jirani yangu unasema nini kuhusu maisha yangu mimi niliyejiinua na kujiona safi na mwema kuliko wengine? Yesu, anakemea hali hii kwa Mafarisayo na Waandishi, na kwetu pia. Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Mtazamo huu wa ugeugeu na kujiinua mbele za Mungu pasipo mastahili yoyote ndio sababu ya mfano wa Msamaria mwema. Wafarisayo ambao kwa kiasi kikubwa walijiinua na kuwa wepesi kuwahukumu wengine, wanashindwa kuokoa uhai ambao ni mali na zawadi ya Mungu kwa vile tu muhitaji huyu na mhusika huyu hakuwa Myahudi. Wakati mwingine tunashindwa kusimama katika kweli kwa vile tu mhusika siyo kutoka familia yetu, ukoo wetu, kabila letu, au kutoka Kanda yetu. Wenye mitazamo kama hii ilihali wanajiita wafuasi wa Kristo, basi Kristo huyo huendelea kusulubiwa kwa matendo yao. Kristo huyo siyo fahari ya maisha yao. Mimi na wewe kama wafuasi wa Kristo hatuna kitu kingine cha kujivunia zaidi ya Msalaba wa Kristo.  Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Je, tusikemee maovu? La hasha! Mkemeapo Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa,” 1Pet 2:1, 21, 23-24. Je, nauona udhaifu wangu ninapoutazama udhaifu wa mwingine?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anapomwambia mwana-sheria yule afanye tathimini kati ya wale wayahudi na yule Msamaria aliyetoa msaada kwa mhitaji yule aliyepata kipigo na wanyang’anyi, mwana-sheria anaelewa soma lile na kumjibu Yesu, “Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo,” Lk 10:37. Wapendwa katika Kristo, yatupasa kusimama katika kweli na haki, hivyo tutende yote kwa upendo na huruma ya kweli. Tusipolifanya jambo hilo basi tujiandae kusutwa na dhamiri zetu katika umiele wote.

Wapendwa wana wa Mungu, mamlaka aliyokuwa nayo Yesu ni vita dhidi ya uovu hapa duniani. Ni ukweli usiopingika kwa kupitia jina lake tunapata uponyaji wa kweli. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6.  Mamlaka ya Yesu yamejengwa chini ya mamlaka ya Mungu. Hivyo hakuna jambo lolote alifanyalo Yesu Lisilo kuwa na uhusiano na Mungu, huku jambo lile likifunua siri ya Mungu kila kukichwa. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake,” Kol 1:16. Kwa nini basi nakuwa na mashaka juu ya utendaji wa Kristo katika maisha yangu?

Wapendwa katika Kristo, Yesu anapotoa mfano wa vazi kuukuu na jipya, na kwa upande mwingine divai ya zamani na kiriba  kipya anataka kutufundisha jambo hili; “kwanza kabisa lazima tujue sababu na malengo ya maisha yetu hapa duniani. Hatupo hapa duniani kwa bahati mbaya hata kidogo. Tupo katika ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu ambao ni dhahiri na mathubuti. Hivyo lolote lile lililo jema mbele ya Mungu huwiishwa na kufanya upya.

Ndugu yangu, maisha ya hapa duniani ni safari. Na katika safari hiyo kila siku tunapimwa kwa upendo. John na Maria walipendana sana tangu walipokutana kwa mara ya kwanza Chuo Kikuu. Baada ya miaka mitatu walifika lengo la kuishi kama mume na mke. Hivyo likizo ya mwaka ule wa mwisho wa masomo yao, John aliafikiana na Maria kwenda kwao na kujitambulisha ikiwa ni pamoja na kuzungumza swala zima la mahari.

Wiki moja kabla, Maria alitangulia nyumbani ili kuweka mazingira vizuri juu ya ujio wa John Mchuma wake. Safari ya kuelekea kijiji kwa Maria haikuwa rahisi kwa John kutokana na usafiri kuwa wa shida na barabara kuwa mbovu. Hata hivyo kwa vile alikwisha penda, John alijitahidi na kupata usafiri ingawa ulikuwa wa kugombania sana. Baba mmoja mwenye umri wa mtu mzima aliyekuwa nyuma yake John katika kurupushani ile ya kugombania usafiri, shati lake lilichanika kiasi kwamba kifua na tumbo lake vilikuwa wazi.

John na Baba yule walikaa pamoja kwenye basi lile ingawa hali ile ya Baba kuwa kifua wazi ilimsikitisha sana John. Ndipo John alipolivua sueta lake na kumpa Mzee yule ajisitiri. Mzee yule alifurahi sana na kumwambia John, “asante sana mwanangu kwa kuusitiri mwili wa Baba yako. Ubarikiwa popote uendapo na utakapokuwa.” Basi John ndipo alipoanza kumwelezea ugeni wake na huko anapokwenda kwa lengo la kujitambulisha kwa mchumba wake aliyekuwa anaitwa Maria Majaliwa. Kadiri ya maelezo yale, Mzee yule alimwambia, “usihofu chochote. Mimi naifahamu vizuri sana familia hiyo na binti huyo. Usijali nitakufikisha mguu kwa mguu.”

Walipofika kituoni, wote wawili waliongozana kuelekea kwenye familia ile ya Maria. Jambo la ajabu walipokaribia tu kwenye nyumba ile Maria na ndugu zake walifika kwa furaha kumpokea Baba yule na John, na mizigo yao yote kwa pamoja  kuiingiza ndani. Hapa ndipo John aliposhtuka na kumuuliza, “kumbe Baba wewe ndiye Mzee Majaliwa Baba ya mchumba wangu Maria?” Naye akajibu, “ndiyo kijana wangu. Na kwa ukarimu na upendo wako kwangu leo, sina shaka na ishi ya binti yangu nawe. Baraka zangu zote nawapa, na yote yaliyo ndani ya mioyo yetu yawe kama Mungu apendavyo.” Hakika ilikuwa furaha sana.

Ndugu yangu, upendo wa kweli ni pale tunapomwona Kristo kwa kila tunayekutana naye bila kujali historia yake, hali yake, familia yake, kufahamiana kwetu, na hata kabila lake.
Tumsifu Yesu Kristo!

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27


Tusali:-Ee Yesu wangu mwema, nifanye nuru na mwanga wako popote pale nitakapokuwa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario