sábado, 9 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 15 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 15 YA MWAKA-C
Somo: Isa 1:11-17
Zab: 50:8-9, 16bc-17, 21, 23
Injili: Mt 10:34-11:1
Nukuu:
 “Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada,” Isa 1:13

Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu,” Isa 1:15

“Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane,” Isa 1:16-17

Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga,” Mt 10:34 

 “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona,” Mt 10:39 

TAFAKARI:Huu wingi wa sadaka zenu mnazonitolea una faida gani?”

Wapendwa wana wa Mungu,   maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine humpendeza Mungu. Lakini kujitoa huku kuwe sadaka inayosukumwa na upendo wa kweli, yaani, niwe mwenye kutoa zaidi ya kupokea. ‘Upendo sadaka’ una gharama yake. Mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo pale msalabani ni mfano hai wa ‘upendo sadaka.’ Kwa maelezo ya sadaka upendo hii, Yesu anasema, “hakuna upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Upendo sadaka huu uwe kielelezo cha sadaka zote zile tuzitoazo kwa ajili ya wengine. Tendo hili liakisi sadaka ile ya Yesu pale Msalabani. Ni “katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu,” 1Yoh 3:16. Kumbe wingi wa sadaka nizitoazo kwa lengo tu la kutoa sadaka bila kusukumwa na upendo wa kweli, tendo hilo halina thawabu wala faida yoyote mbele ya Mungu.

Ukavu huu wa utoaji wa sadaka kwa kuangalia wingi wake ndio anaoukataa Mungu kupita kinywa cha Mtumishi wake Nabii Isaya. Naye anasema, sadaka hizo, “zimejaa mafuta ya kafara za kondoo waume, na mafuta ya wanyama walionona; nami siifurahii damu ya ng'ombe wala ya wana-kondoo wala ya mbuzi waume,” Isa 1:11. Ndugu yangu, elewa kwamba hutoi sadaka kwa kumrubuni Mungu ili uyafikie matamanio yako binafsi. Hakika Mungu hataki wingi wa sadaka usio na chembe ya upendo ndani yake. Je, tunayomtolea Mungu ni mali ya nani? Hakika, Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Je, Mungu anahitaji nini basi tunapomtolea sadaka zetu? Mungu anachotaka kutoka kwetu ni fadhila, utayari wa tendo hilo la ‘upendo sadaka,’ yaani, ufahamu wa kweli wa kile nikitoacho na umaana wake, na siyo wiki wake usio na ufahamu wala maana. Naye Mungu anasema, “nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa,” Hos 6:6. Je, kile nikitoacho, yaani, sadaka, kinaniweka karibu na Mungu? Kinanifanya nimjue Mungu?

Ni katika wingi wa sadaka usiobeba ufahamu na maana, baadhi yetu wapo tayari kumtolea Mungu sadaka zilizo najisiwa, yaani, zisizo halali. Sadaka za mtindo huu Mungu anazikataa katu katu. Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada,” Isa 1:13. Bila shaka jamii yetu ya leo yenye kughubikwa na ufisadi kila kona, tumekuwa chukizo kwa kile tumtoleacho Mungu kama sadaka. Haya ni mateleo ya ubatili! Kwa upande mwingine hata wale wenye hofu ya Mungu wamekengeuka na kupokea sadaka hizi za kifisadi kukidhi hitaji la wakati na muda kwenye taasisi za kidini. Nia na maombi yetu tuyatoayo katika mazingira kama haya Mungu huficha macho yake asituone. Naye anasema, Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu,” Isa 1:15. Kama Mungu ataficha macho yake asione kile tufanyacho, basi tafsiri ya tendo hilo huwa “igizo.” Mungu apendi maigizo. Mungu anapenda tuwe kile tulicho, na kwa njia hiyo hapa kuna wokovu wako.

Dhuluma ni mbaya sana. Ni katika maigizo haya, wamdhulumu mnyonge leo, na kesho mbele za watu kwa kujitabanaisha na cheo na nafasi yako katika jamii wapanda madhabahuni ukiwa na kitita cha fedha kumtolea Mungu sadaka katika mtindo wa harambee. Hakika damu hii ya wanyonge Mungu hatoipokea, na badala yake itakulilia daima. Kuhusu wanyonge Mungu anasema, “heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu. Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake,” Zab 41:1-2. Kumbe kwa nafasi na vyeo nilichokuwa nacho katika jamii yanipasa kuwa sauti ya wasio na sauti, yaani, wanyonge.

Ndugu yangu, kama mkono wako huenda kinywani kila siku kwa mtindo huu wa kufinyanga haki za wanyonge, na kumlaghai Mungu mbele za watu kwa sadaka hizi za damu na jasho la wanyonge, Mungu anakupa nafasi ya kujiosha na kujitakasa. “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane,” Isa 1:16-17. Hakuna njia ya mkato katika hili ndugu yangu. Sakramenti ya upatanisho ndiyo njia ya kumrudia Mungu katika hali na mazingira kama haya.

Ndugu yangu, upendo wa Mungu kwetu na utayari wake wa kusamehe hauna mfano. Kinachotokea kwa upande wetu, ni kukubali kufa na tai shingoni, ni kwa sababu ya kiburi chetu. Chapa tulioyonayo ya sura na mfano wake Mungu, Mwa 1:27, ndiyo kivutia kikubwa cha hurama yake kwetu. Mungu wetu hapendi kuona tunaangamia bure. Anasema hata kama tungekuwa na dhambi nyekundu kama bendera, yupo tayari kusameha na kuzifanya nyeupe kama sufu, Isa 1:18

 Mpendwa katika Kristo, kwa nini unakubali kuumwa na mbwa aliyefungwa na mnyororo wa chuma kwenye mti? Dhambi, ni kujipeleka ukijua kabisaaa! Wokovu ni kumrudia Muumba wako ukijua uzuri na wema wake. Hata hivyo, pamoja na madhaifu yetu, Mungu bado hajakata tamaa nasi. Pamoja na watu kutokutambua wema wa Mungu, “ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha,” Neh 9:17

Ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, watu wengi hujihukumu wenyewe na kujifungia neema za kupatanishwa na Mungu. Ni kosa kubwa kuishi katika hatia fulani. “Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake,” Wal 5:17. Lakini Mungu wetu hakai na hasira yake milele. Kufanya hivyo ni kinyume cha uhalisia wake. Yeye hufurahia rehema. “Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18

Hata hivyo, kuiishi Imani ni changamoto kubwa sana. Yesu anaiona changamoto hii na anatupa angalizo. Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga,” Mt 10:34. Kuiishi Imani yetu ni kufanya vita dhidi ya utawala wa giza. Ni kuuishinda uovu kila siku. Mapambano haya lazima yazue sintofahamu nyingi; kifamilia, kiukoo, na hata kijamii.  Hivyo, Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili,” Mt 10:37. Ufuasi wetu katika Kristo, ni ufuasi wa kujikana nafsi kila siku. Mahangaiko yetu ya kila siku yasiwe ukuta wa kutokuishi imani yetu. Ni katika mateso pia tunakutana na Kristo kwani kwa njia hiyo ya mateso Kristo kaushinda msalaba kwa kujipatia utukufu. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona,” Mt 10:38-39. Hakuna utukufu pasipo msalaba.

Wapendwa wana wa Mungu, tuishi na kila mmoja wetu kwa upendo na amani. Tupokeane na kutabikiana kwa upendo. Tupokeane kwa upendo katika kweli. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki,” Mt 10:41. Tuyaone mazuri kwa wenzetu, na mazuri hayo yawe kielelezo cha kuuona uzuri wa Mungu kwa yule aliyeumbwa na sura na mfano wake.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona,” Mt 10:39


Tusali:-Ee Yesu tufanye vyombo vyako vya haki na amani. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario