JUMANNE
WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Mik 7:14-15, 18-20
Zab: 85:2-4, 5-6, 7-8
Injili: Mt 12:46-50
Nukuu:
“Alipokuwa
katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama
nje, wataka kusema naye,” Mt 12:46
“Akajibu,
akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina
nani?” Mt 12:48
“Kwa
maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye
ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu,” Mt 12:50
“Ni
nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu
wa urithi wake waliosalia?” Mik 7:18a
“Hashiki
hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18b
TAFAKARI: Ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye
mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.”
Wapendwa wana wana
Mungu, Somo la kwanza, kutoka kitabu cha Nabii Mika linatuelezea uhasili wa
Mungu. Mungu kwa asili ni Upendo, Huruma, na Msamaha. Ni Mungu anayetutakia
mema muda wote sisi viumbe na wana wake. “Ni
nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu
wa urithi wake waliosalia?” Mik 7:18a. Ni Mungu anayejifunua kwetu
kupitia historia na vile alivyoviumba. Ni Mungu ambaye yupo na alikuwepo na
atakuwepo milele yote.
Kwa upande wetu, tunayokazi moja tu, yaani kumtafuta kwa maana
anapatika. Nabii Isaya anatuambia hivi, “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana,
Mwiteni, maadamu yu baribu; Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki
aache mawazo yake; na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu,
Naye atamsamehe kabisa.” Isa 55:6-7
Ndugu yangu, kumwasi
Mungu ni tendo ambalo lipo chini ya uwezo wetu. Kumrudia Mungu ni tendo la toba
na kufanya maamuzi ya msingi kabisa. Mungu “hashiki
hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18b. Unapofanya
maamuzi haya ni wazi itakulazimu
kuachilia mengi ambayo kwayo yalikupa furaha na hata kujulikana na
kujikweza. Ila tukitambua umuhimu wa umilele wa maisha yetu, hatuna budi
kuachilia yote haya ambayo ni ya kupita na ya muda mfupi. Mungu “atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe
utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya baharí,” Mik 7:19
Ufanyapo toba ya kweli
na kumrudia Mungu, anakupokea kama tulivyo. Mungu katika mapokezi haya hatazamani
historia yako iliyo mbaya. Mungu huanza mradi mpya nawe na kukufanya mpya tena
katika yale mazuri anayokufikiria. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi,
asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku
zenu za mwisho,” Yer 29:11. Ndugu yangu, kwa nini hubadiliki? Waitaji malaika
washuke na kukuambia jambo hili? Kwa nini unakuwa kero kwa ndugu na jirani
zako? Kwa nini unakuwa kero kwa wanajumuiya wako na viongozi wako? Je, unapenda
kuishi hivyo hadi lini?
Ndugu yangu elewa jambo
hili; sote tumefanywa wana na ndugu kwa upendo wa Mungu kwa njia ya Mwanaye
Mpenzi Yesu Kristo. Na hapa ndipo tunapoiona asili ya Mungu, yaani, Upendo,
Huruma, na Msamaha. Maandika Matakatifu yanatufundisha hivi: “Hakuna
aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki
zake,” Yoh 15:13. Kwa tendo hili la upendo wa Mungu kwa kumtoa mwanaye Yesu
Kristo, leo hii sote tumefanywa ndugu katika Kristo. Hivyo Yesu haoni haya
kuwaambia wazazi wake ukweli huu. “Akajibu,
akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina
nani? Akawanyoshea mkono
wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote
atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na
umbu langu, na mama yangu. ” Mt 12:48-50
Kuyafanya mapenzi ya Mungu ni kutambua
ukweli huu wa kumwilishwa Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ambaye alikuwa mbali
sana na viumbe vyake sasa yupo karibu, yaani: “Tazama,
bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli;
Yaani, Mungu pamoja nasi,” Mt 1:23. Huyu ndiye Mungu anayetuunganisha na kuwa
watoto wake bila kujali familia zetu, koo zetu na kabila zetu. Yeyote yule
mwenye kujinadi kwa koo au kabila lake na kujiona bora kuliko wengine, na huku
akijiita mfuasi wa Kristo na Mkristo, bado hayajitambua.
Tumsifu Yesu Kristo
“Hashiki hasira
yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema,” Mik 7:18b
Tusali:- Ee Mungu, twasema
asante kwa kutupenda kama tulivyo, na upo tayari kutusamehe. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario