miércoles, 13 de julio de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 15 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 15 YA MWAKA-C
Somo: Isa 38:1-6, 21-22, 7-8
Zab: 38: 10, 11, 12abcd, 16
Injili: Mt 12:1-8
Nukuu:
 “Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona,” Isa 38:1b 

Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu,” Isa 38:5-6 

 “Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao?” Mt 12:3-4 

 “Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia,” Mt 12:7 

Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,” Mt 12:8 

TAFAKARI: “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunapoongelea ufunua wa wazi na wa kweli wa Mungu, kigoto chake au hitimisho lake ni  ‘Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu,’ Yoh 1:14. Tendo hili limebebwa katika upendo wa kweli wa Mungu, na dhumuni na malengo ya uumbaji wake. Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18. Ndugu yangu unayesafiri nami sasa katika tafakari hii, upendo huu wa Mungu ikiwa ni pamoja na nia na kusudi lake, haukufifishwa licha ya maanguko ya mwanadamu. Na huu ndiyo uthibitisho wa upendo wa Mungu kwetu kwamba,  kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Ni kwa upendo wake Mungu na siyo mastahili yetu kwamba Mungu alituumba kwa sura na mfano wake mwenyewe, Mwa 1:27. Hivyo wokovu wetu katika mantiki hii ilikuwa ni swala la wakati tu kwa upande wetu. Mungu hakufungwa na hajafungwa na wakati kwa nyakati zote zote kwa sababu yeye ni alfa na omega, Ufu 1:8; 21:6; 22:13. Hakika, ‘Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato,’ Mt 12:8

Ni katika maana hiyo ya Mungu kutokufungwa na wakati, na ilipompendeza na kusadifu, alisema ‘sasa inatosha na nitafanya kitu na kutimiza lengo langu.’ Hivyo, “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Tendo hili la ajabu na la Kimungu linamwinua mwanadamu katika maana ya kumshirikisha, yaani, Mungu kuchukua umbo la mwanadamu ili kuwezesha na kufikia kile kilicho cha Kimungu. Hii ndiyo maana halisi ya Neno kufanyika mwili na kukaa mwetu. Mtume Paulo anaelezea kweli hii kwa maneno haya: Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Ni upendo gani huu wa ajabu wa Mungu ambao mimi na wewe tukae kimya bila kumshukuru Mungu? Kwa maana nyingine tendo hili la Mungu lamaanisha hivi; ‘Mungu aliye tajiri wa kila kitu amekubali kujishusha ili mimi na wewe tuwe tajiri kwa umasikini wake.’ Hakika Mungu anakupenda na ananipenda sanaaaaaaa! Katika kweli hii ya Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Mungu katika umasikini wake ili tuwe matajiri,  Mtume Paulo anasema, maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ndugu yangu una sababu yoyote ya kujiona mnyonge ilihali unapumua pumzi ya Mungu bila tozo lolote?

Ndugu yangu, ni katika hali na mazingira hayo niliyoyasema kama utangulizi wa tafakari yetu ya leo, Nabii Isaya ana mwakilisha Mungu mbele ya Mfalme Hezekia katika hali yake ya kufa. Katika hali hii, Nabii Isaya anaenda kwa Mfalme Hezekia na kumwambia,  “Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona,” Isa 38:1b. Ndugu yangu, kufa ni lazima, ila kuzaliwa siyo lazima. Kama kufa ni lazima, umejiandaaje na tukio hili la lazima? Kwa kutambua kweli hii juu ya maisha na kifo ambacho ni lazima, Mfalme Hezekia anakiri haya mbele ya Mungu,Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana,” Isa 38:3. Hatuna sababu ya kuwa na hofu na mashaka mbele ya Mungu kama twaenenda mbele zake Mungu katika kweli na haki. Pasipo shaka yoyote, Mungu anamjibu Mfalme Hezekia kwa kinywa cha Nabii Isaya;Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu,” Isa 38:5-6. Na maneno haya ya Mungu yalithibitishwa kwa ishara hii, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona,” Isa 38:21. Hakika Mungu ni mwaminifu nyakati zote! Hivyo kama Mungu ni mwaminifu nyakati zote, huo ndio mwito wetu mbele ya Mungu, yaani, kuwa waaminifu kwake, Mt 5:48. Na kwa mantiki hiyo, yote tuyafanyayo lazima yawe na uhusiano na Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu hapendi sadaka zetu zisizo na uhusiano wa maisha yetu na thamani mbele zake. Mungu wetu hupenda rehema na neema anazotujalia pale tunapoziishi kuliko kile tumtoleacho kama sadaka. Yote tumtoleayo ni mali yake, Zab 24:1. Vyote vipo chini ya mamlaka yake. Hivyo Yesu anasema, Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia,” Mt 12:7. Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka kutokana na mila na desturi zetu, wakati fulani tulilazimika kufanya mitambiko na hata kutolea sadaka za kuteketezwa zisizo na uhusiano na imani yetu. Kwa kufanya hivi tunapoteza dira na mwelekeo wa Kimungu katika maisha yetu. Je, naweza kuwa huru hata kama naishi katika mila na desturi hizi? Jibu ni HAPANA! Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24 

Tumsifu Yesu Kristo.

“Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona,” Isa 38:1b


Tusali:-Ee Yesu ujuaye siri ya maisha yangu, nasema asante kwa sababu kwangu wewe watosha. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario