JUMAPILI YA 17 YA MWAKA-C
Somo
I: Mwa 18:20-32
Zab: 138:1-2, 2-3, 6-7, 7-8
Somo
II: Kol 2:12-14
Injili:
Lk 11:1-13
Nukuu:
“Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki
pamoja na mwovu?” Mwa 18:23
Akasema,
Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b
“Mkazikwa
pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa
kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu,” Kol 2:12
“akiisha kuifuta
ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu;
akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani,” Kol 2:14
“Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni],
Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani
kama huko mbinguni.]” Lk 11:2
“Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila
tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu],” Lk 11:4
TAFAKARI: “Wokovu si tendo tu lenye kubeba maana ya
mtu mmoja aliye mwema, bali kwa yule mwema mmoja katikati ya waovu Mungu huwa
na huruma kwa kundi HILO.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa
anaadhimisha Dominika ya 17 ya Mwaka “C” wa Kanisa. Wana wa Taifa la Mungu, ni
kweli kwamba hatupo ulimwenguni humu kwa bahati mbaya. Tupo ulimwenguni humu
kwa malengo ya Mungu kila mmoja kadiri ya wito wake. Pamoja na malengo hayo
mazuri ya Mungu, uwepo wetu hapa duniani ni mwendelezo wa ukombozi wa kila
mmoja wetu kwa nafasi yake binafsi, na kwa upande wa pili kila mmoja wetu kwa
ukombozi wa wingine. Hivyo kwa lengo hili la pili, Mtume Paulo anasema, “Kila
mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine,”
Flp 2:4. Somo letu la kwanza la leo linatuelekeza kuyatafakari makuu haya.
‘Wokovu si tendo tu lenye kubeba maana ya mtu mmoja aliye mwema, bali kwa yule
mwema mmoja katikati ya waovu Mungu huwa na huruma kwa kundi HILO.’ Hapa ndipo kulipobeba maana ya swali ya
Ibrahimu na jibu la Mungu. “Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye
haki pamoja na mwovu?” Mwa 18:23. Mungu anamjibu Ibrahimu na kusema, “Nikiona
katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao,”
Mwa 18:26.
Ukweli
ni kwamba Mungu hututakia mema kila siku na hapendi tuangamie kwa jambo lolote.
Tumepewa uhuru wa kufanya lililo jema, na hata kwenda kinyume cha yale
yasiyompendeza Mungu. Ni kwa uhuru huo huo tunaweza kumrudia Mungu kwa toba na
majuto. Mungu anatujua jinsi tulivyo na yupo tayari kutupokea jinsi tulivyo.
Ibrahimu anazidi kumdadisi Mungu na kupima uwezo wake wa kusamehe. Mungu
anaonyesha hana kigezo chochote cha kusamehe zaidi ya utayari wa muhusika
kuiacha njia yake mabaya na kumfuata. Ibrahimu hachoki kumdadisi Mungu kuhusu
huruma yake. Naye “akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema
mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi?” Mwa 18:32a. Mungu anaweka msimamo
wake wazi na kumjibu Ibrahimu, “Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi,” Mwa 18:32b.
Je, tunasababu yoyote kupata adhabu ya Mungu kwa mwelekeo huu wa Mungu kuwa
tayari kusamehe makosa yetu?
Sodoma
na Gomora ni miji iliyosikika kwa kutokuishi maadili mema. Kulikuwa na kila
aina ya dhambi. Ukimya wa Mungu siyo kwamba hakuona maovu hayo, bali Mungu anatuamini
kwamba ukweli utatuweka huru tunapogundua na kuacha njia zetu mbaya. "Tena
mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Yoh 8:32. Kweli hii ndiyo
tunayoitafuta kila siku ya maisha yetu, na kila mmoja kadiri ya wito wake. Kwa
“Kuwa” utawani, au maisha ya ndoa kama yalivyo haitoshi, ila kuuishi ukweli wa
maisha hayo kama yalivyo ndio kunakoleta utofauti. Wapo tulioingia mifumo hiyo
ya maisha kama yalivyo na mwisho wa siku tumejikuta ni watupu kabisa. Kumbe
yanipasa kila siku kuutafuta ukweli juu ya maisha hayo na kuuishi ukweli huo
kila siku, na kwa majira yote.
Ndugu
yangu, mfano hai wa wazo letu kuu la leo, yaani, ‘Wokovu si tendo
tu lenye kubeba maana ya mtu mmoja aliye mwema, bali kwa yule mwema mmoja
katikati ya waovu Mungu huwa na huruma kwa kundi HILO,’ ni Yesu Kristo mwenyewe
na kile alichokufanyia wewe na mimi pale Msalabani. Ni kwa tendo hilo tulizikwa
‘pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa
kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu,’Kol 2:12. Ni kwa ajili ya
mwenye haki mmoja kundi zima la wenye dhambi, yaani, mimi na wewe tunakuwa huru
na kuhesabiwa haki mbele za Mungu. “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa
yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe
makosa yote,” Kol 2:13. Na hivi ndivyo tulivyo wana wa Mungu, na warithi wa
Ufalme wa Mungu kwa sadaka hii ya Yesu pale Msalabani.
Na alichokutendea Yesu pale Msalabani wewe na mimi ni hiki, “akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya
kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,
akaigongomea msalabani,” Kol 2:14. Ndugu yangu, mimi na wewe tumekombolewa kwa
thamani kubwa sana. Na hivi
ndivyo asemavyo Mtume Petro, “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si
kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu
usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya
mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19.
Hakika sina budi kusema asante kwa Yesu Kristo kila niivutapo punzi yangu.
Asante Yesu!
Ndugu
yangu, na huu ni ukweli kwamba pamoja na hatia alizokuwa nazo mtu, Mungu hubaki
kuwa HURUMA, MSAMAHA, UPENDO NA AMANI yetu. Huruma hii na upendo huu wa Mungu,
tunauona katika sala ya Baba yetu ambayo leo mmoja wa wanafunzi wa Yesu
anamwomba Yesu awafundishe namna ya kusali. Sala hii ya ‘Baba Yetu’
inatufundisha na kuweka wazi ni nani aliyekimbilio letu la pekee, na mapaswa
yetu tungali hapa duniani. “Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni],
Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani
kama huko mbinguni.]” Lk 11:2. Jambo lingine la msingi ni huruma ya Mungu kwa msamaha wa makosa yetu inayotokana na
kiwango kile kile cha sisi kuwasamehe wale waliotukosea. “Utusamehe dhambi
zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni
[lakini tuokoe na yule mwovu],” Lk 11:4. Wapendwa wana wa Mungu, kama kipimo
cha kupenda ni kupenda bila kipimo kama asemavyo Mt. Agustino, basi ni hivyo
hivyo masharti ya kusamehe ni kusamehe bila masharti.
Pamoja
na kusamehe huku bila masharti kama tulivyokwisha kuona katika somo la kwanza
kwa upande wa Mungu kumwelekea mdhambi, somo letu la Injili linafafanua pia
vizuri dhana nzima ya ‘wanyofu wa moyo na kuhesabiwa haki mbele za Mungu.’ Hawa
ndio waliomfanya Mungu kuwa kimbilio lao. Hawa ndio wale wasiokuwa na mbadala
wa maisha yao zaidi ya Mungu katika shida zao. Hawa ndio Yesu anaowaambia, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni,
nanyi mtafunguliwa,” Lk 11:9. Huu ndio uhusiano wa Mungu na aliyemnyofu wa
moyo. Mungu kamwe hatosita kutokumhesabia haki katika kweli. “Kwa
kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,”
Lk 11:10. Ni kweli hata aliyekatili aweza kutoa bila upendo kwa yule
anayemsumbua, lakini mwenye kupenda hawezi kuacha kutoa. Mungu wetu ni upendo
na anajua mahitaji yetu yote. Naye Yesu anaufunua upendo huu wa Mungu kwetu kwa
kusema, “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu
vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao
wamwombao?” Lk 11:13. Ndugu yangu tuliosafiri wote katika tafakari hii, jisalimishe kwake aliye Mungu wa kweli,
upendo, haki na amani.
Onesmo
Chilambi aliyelelewa na Bibi yake tangu akiwa na umri wa miaka mitatu baada ya
wazazi wake wote wawili kufariki kwa ugonjwa wa Ukimwi; akiwa na umri wa miaka
12 Onesmo alibaatika kupata kibarua cha kubangua korosho kwenye kiwanda kidogo
cha Mzee Kasumuni, kwani Bibi yake hakuwa na uwezi wa kumsomesha.
Onesmo
Chilambi alifanya kazi ile kwa uaminifu mkubwa sana kwa muda wa miaka 30. Na
kwa kazi ile aliweza kujijengea kajumba kazuri ka kuishi, kuoa na kuwa na
familia ya watoto watatu, ingawa mkewe alikuwa mjamzito pia. Kwa wakati huu,
mtoto wake wa kwanza alikuwa shule ya ufundi, wa pili sekondari kidato cha
kwanza, na huyo wa tatu alikuwa shule ya msingi darasa la tano.
Siku
mmoja Ijumaa, akiwa kesha maliza kubangua korosho, alishawishika kuchukua
sadolini moja ya korosho ili auze na kuongeza ada ya mwanaye aliyerudishwa nyumbani
kwa sababu ya ada kutoka chuo kile cha ufundi. Kwa vile hakuwahi kuwa mwizi,
alipita getini kwa mashaka sana, kiasi kwamba mlizi aligundua kuna kitu ambacho
si cha kawaida kwa Bwana Onesmo Chilambi. Baada ya kupekuliwa, alikutwa na
sadolini moja ya korosho.
Onesmo
alipelekwa moja kwa moja kwa Mzee Kasumuni. Onesmo alikiri kufanya kosa lile
kwa mara ya kwanza kwa miaka yake 30 ya kazi. Hata hivyo Mzee Kasumuni
hakusadiki na hakuwa tayari kumsamehe. “Nakuomba Mzee wangu usinifukuze kazi.
Nipo tayari unikate kiasi cha mshahara wangu nilipe kiasi hiki cha korosho,”
Onesmo Chilambi alisema kwa majonzi na huzuni kubwa. “Sinto kukukata chochote,
na fedha yako yote ya mwezi huu sintokupa, na wala hutopata kiinua mgongo chako
kwa miaka hiyo 30 uliyofanya kazi hapa. Siwezi kulea wezi hata kidogo na iwe
fundisho kwa wengine,” Mzee Kasumuni alifoka kwa hasira.
Kurudi
nyumbani, Bwana Onesmo alieleza yote yaliyojiri kwa familia yake, na sababu ya
kufanya hivyo. Mara presha ilimpanda mke wake na kujifungua kabla ya wakati na
kusababisha kifo cha kichanga kile na Mama baada ya kukosa huduma ya haraka na
kupoteza damu nyingi. Baada ya wiki moja kupita, watoto walishangaa kuona Baba
yao kuchelewa kuamka kitu ambacho hakikuwa cha kawaida. Kufungua mlango wa
chumba cha wazazi wao, walimkuta Baba yao kajitundika juu ya paa la nyumba.
Hakika ilikuwa uzuni kubwa na simanzi.
Ndugu
yangu, kilichokosekana hapa ni MSAMAHA tu. Embu ona madhara ya kutokusamehe
hasa pale anayehitaji kusamehewa anapojifunua hadi tone la mwisho.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa kuwa kila
aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa,” Lk 11:10
Tusali:-Ee
Yesu kila mara niutazamapo Msalaba wako Mtakatifu, nikumbushe upendo wako na
wajibu wangu wa kusamehe. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario