ALHAMISI WIKI YA 17 YA MWAKA-C
Somo:
Yer 18:1-6
Zab: 146:1b-2, 3-4, 5-6
Injili:
Mt 13:47-53
Nukuu:
“Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika
mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama
alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya,” Yer 18:4
“Ee
nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi
huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa
mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli,” Yer
18:6
“Tena
ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki
wa kila namna,” Mt 13:47
“Akawaambia, Kwa
sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu
mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale,” Mt 13:52
TAFAKARI:
“Mungu yupo tayari kuanza upya nawe. Ni utayari wako tu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
bila shaka kuna wakati unafika nakujiona hufai mbele ya Mungu, na hasa pale
unapoitazama historia yako iliyo mbaya. Kama binadamu wakati mwingine
tunajiangalia katika maana ya kujihukumu kwa sababu hatuna tumaini tena katika
maisha. Mungu wetu aliye Upendo na Huruma tazama yake kwetu ni ile yenye kubeba
uhasili wake, yaani, Upendo na Huruma. Mungu daima yupo tayari kuanza upya nasi
tunapojirudi na kuacha njia zetu mbaya. Kumbe hapa yategemea utayari wangu, na
kuona upendo na huruma hii ya Mungu isiyo na mipaka.
Taswira hii ya Mungu
aliye Upendo na Huruma inajidhihirisha kwa Nabii Yeremia kwa mfano wa nyumba ya mfinyanzi, aliye kuwa akifanya kazi yake kwa
magurudumu, Yer 18:2. Mungu katika mfano huu anapenda kuufunua upendo na huruma
yake. Haijalishi historia yako mbaya wala kuanguka kwako, bali utayari wako wa
kuamka na kuanza upya na Mungu. Naye Mungu anamwambia Yeremia, “Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na
huko nitakusikizisha maneno yangu,” Yer 18:2. Na hivi ndivyo Yeremia alivyoona
akifanya yule Mfinyanzi; “Na chombo kile,
alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi,
alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi
kukifanya,” Yer 18:4. Ndugu yangu, hivi ndivyo Mungu huyabadili maisha yako
pale unampomrejea. Na katika tendo hili, Mungu anaufunua upendo na huruma yake
na kusema akitumia kinywa cha Nabii Yeremia, “Ee
nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi
huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa
mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli,” Yer
18:6. Hakuna limshindalo Mungu kama tutakuwa
tayari kumrejea katika hali ya toba na majuto ya kweli. Mungu hawezi kuumba
jiwe kubwa kiasi kwamba Yeye mwenyewe akashindwa kulibeba.
Mungu wetu huyu ambaye
ni Huruma na hukumu yake ni ya haki, hayupo katika hali ya kutuvizia tunapotenda
kosa au dhambi na kutuadhibu. La hasha! Mungu wetu ambaye taswira na uhalisia
wake ni UPENDO NA HURUMA, utuvumilia hadi mwisho akiwa na matumaini makubwa
kubadilika kwetu kutoka katika njia mbaya na kumrudia yeye. Hivyo, licha ya
anguko la wazazi wetu wa kwanza, Mungu hakuondoa uhuru ndani yetu wa kumrudia
baada ya kutambua mienendo yetu mibaya. Ni kwa uhuru huo huo twaweza kurudi
kwake au kuendelea katika hali ya uasi na dhambi.
Ndugu yangu, kuishi
katika kweli na haki ya Mungu ni kuishi katika ufalme wake. “Tena
ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki
wa kila namna; hata lilipojaa,
walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya
wakawatupa,” Mt 13:47-48. Hivyo ni katika kweli na haki hii tunapokutana na
hukumu ya haki ya Mungu. Mungu hutupa hali na uwezekano wa kuziacha njia zetu
mbaya na kumrudia ili mwisho wa siku tusipate nafasi yoyote ya kumtupia lawama.
Mungu anaheshimu sana uhuru wa kila mmoja wetu, kwa sababu ndiye Yeye aliyetuumba
kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Mungu hapendi kutuburuza kama nyapara
gerezani.
Elimu ya ufalme wa
Mbinguni ni kujifunza kweli na haki ya Mungu. Ni katika kweli tunakuwa huru,
Yoh 8:32, na ni katika kutimiza mapenzi ya Mungu kadiri ya maagizo yake
tunahesabiwa haki. Tunapotimiza jambo hili kwa ufasaha wake, twatwaliwa haki ya
mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni. Naye Yesu anasema, “Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya
ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake
vitu vipya na vya kale,” Mt 13:52. Huku ndiko kuwa wapya katika Kristo na ndani
ya Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Asema Bwana.
Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi
katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli,” Yer 18:6b
Tusali:-Ee Mungu uliye Upendo
na Huruma yetu, tuongoze daima katika kweli na haki. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario