JUMATATU
WIKI YA 16 YA MWAKA-C
Somo: Mik 6:1-4, 6-8
Zab: 50:5-6, 8-9, 16bc-17, 21, 23
Injili: Mt 12:38-42
Nukuu:
“Kwa
maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya
utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako,”
Mik 6:4
“Ee mwanadamu,
yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki,
na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!” Mik 6:8
“Kizazi
kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya
nabii Yona,” Mt 12:39
“Malkia wa kusini
atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa
wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie
hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani,” Mt 12:42
TAFAKARI: “Tenda haki, na kupenda rehema, na
enenda kwa unyenyekevu.”
Wapendwa wana wa Mungu, kwa upendeleo wa ajabu
Mungu alioufanya kwetu, yaani kwa kutuumba kwa sura na mfano wake, hatuna budi
kuwa watu wa haki na kupenda rehema, na kuenenda kwa unyenyekevu kama shukrani
kwa Mungu kwa tendo hili la ajabu. Ni kwa upendeleo huu Mungu haachi kwamwe
kukupigania licha ya uasi wako na njia zako mbaya. Naye Mungu asema, “Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa
utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu,
watangulie mbele yako,” Mik 6:4. Mungu apenda
kila mmoja wetu awe huru, na katika uhuru huo achague ni nani anayetaka
kumtumikia. Ni ndani ya uchaguzi huu ulio huru tunapojihukumu sisi wenyewe.
Siku ya mwisho, yaani, katika ukuhumu ile, Mungu atafanya hakikisho tu la
hukumu ambalo kwa kadiri tunavyoishi ndivyo tujihumivyo kwa uhuru ule tuliokuwa
nao. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka
nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na
Mungu wako!” Mik 6:8. Huu ndio wito wetu wa
kila siku kama wafuasi wake Kristo na wale wote wenye hofu ya Mungu.
Matumaini yetu mbele za
Mungu hayapaswi kusukumwa na ishara kama ndiyo msingi wa kumwamini Mungu. Ishara
au miujiza itusaidie kukoleza Imani yetu na wala sio msingi wa imani yetu. Yesu
anatoa angalizo na kusema, “kizazi
kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya
nabii Yona,” Mt 12:39. Ndugu yangu, hakuna ishara zaidi ya Yesu mwenyewe ambaye
ndiye yote katika yote. Fumbo zima la wokovu wetu limekamilishwa kwa
kumwilishwa neno, Yoh 1:14. Hivyo basi hakuna ishara kubwa zaidi ya hii. Naye
Yesu anasema, “Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa
kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka
pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu
kuliko Sulemani,” Mt 12:42. Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo kila kitu kwetu. Je,
bado waitafuta njia? Yesu ndiye njia. Je, bado wautafuta ukweli? Yesu ndiye
ukweli. Je, wautafuta uzima? Yesu ndiye uzima wa kweli. Ngoja nikujuze!
Naye Yesu anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Yesu Kristo ni njia
kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua Yesu
ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukuliana kindugu katika misalaba
yetu na ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu tunakutana naye Kristo katika
hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii tunakutana nayo
katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno, kulipokea neno,
kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi wa neno.
Na Yesu Kristo ni
uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika
mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi
ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu
yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu:
Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa
ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh
6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo
la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa
kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na
roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa kupitia Sakramenti ya kitubio tunapatanishwa tena na Kristo kutoka katika
hatia zote. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu
zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama
bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18. Hakuna sababu ya kufa moyo pale ambapo
mambo huenda ndivyo sivyo. Mungu aliye Upendo na Huruma uanza upya nasi pale
tunapokuwa tayari kufanya hivyo. Hivyo ndani na katika Kristo hakuna sababu ya
kuwa na hofu. Tumwamini Kristo na tuziamini kazi zake na hasa kupitia
Masakramenti yake. “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu,
niaminini na mimi,” Yoh 14:1.
Ndani na Katika
Kristo kunautulivu wa kweli, naye kesha tuandalia makao ya milele. Duniani hapa
ndugu yangu tunapita tu. Ulimwenguni hapa ni sehemu ya maandalizi ya huo
umilele. Mbinguni ndipo kwenye nafasi ya kila mmoja wetu, na ndiyo makao ya
milele. “Nyumbani mwa
Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda
kuwaandalia mahali,” Yoh 14:2. Lengo la Kristo ni kumpata kila mmoja wetu. Hili
ndilo pia lengo msingi la Kanisa. Lilipo Kanisa katika maana ya Mwili wa Kristo
nasi tukiwa viungo hai vyake, Kanisa huwa Sakramenti ya Wokovu kwa sababu
Kristo yu hai mahali hapo. “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali,
nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo,” Yoh 14:3.
Ndungu yangu, je, hu kiungo hai cha mwili wa Kristo, yaani Kanisa?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Akajibu,
akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa
ishara, ila ishara ya nabii Yona,” Mt 12:39
Tusali:-
Ee Yesu, Wewe watosha. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario