IJUMAA
WIKI YA 14 YA MWAKA-C
Somo: Hos 14:2-9
Zab: 51:1-2, 6-7, 10-11, 15
Injili: Mt 10:16-23
Nukuu:
“Nitakuwa
kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi
yake kama Lebanoni,” Hos 10:5
“Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye
haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake,” Hos 10:9b
“Angalieni,
mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka,
na kuwa watu wapole kama hua,” Mt 10:16
“Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina
langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22
TAFAKARI: “Kwa maana njia za Bwana zimenyoka,
nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake,”
Hos 10:9b
Wapendwa wana wa Mungu, hakuna kati yetu aishiye kwa nafsi yake
mwenyewe, wala hakuna afaye kwa nafsi yake, Rum 14:7. Ni katika kweli hii
kwamba yupo aliye na mamlaka yote kuhusu hali na maisha yetu. Na huyu ndiye
Mungu anayejifunua kwetu kwa namna mbalimbali katika maisha yetu. Kabla ya yote
Mungu amejifunua katika uumbaji wa vyote tuvionavyo na tusivyoviona. Na wakati
ulipotimia, Yoh 3:16, Gal 4:4-5, na Ebr 1:1-2, Mungu alijifunua katika tendo la
Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Katika tendo hili Mungu
ametuangazia mwanga wake, ameuonyesha Umungu wake, na ametuhesabia haki. Mungu
ameendelea kuufunua upendo wake kwa kifo kile cha Msalaba cha Kristo. Katika
tendo hili tumeona ubora na ukamilifu wa tendo la sadaka, wokovu na ushindi.
Mungu ameendelea kujifunua kwetu kwa tendo la ufufuko. Hapa tunaona ushindi wa
Msalaba na maisha ya Milele. Mungu anaendelea kujifunua kwetu kupitia Roho wake
Mtakatifu na kutupa ufahamu wa kujua siri ya Mbinguni ikiwa ni pamoja na yale
yote aliyotufundisha Yesu Kristo.
Ni katika safari hii yote ya historia ya wokovu wetu tangu kuumbwa kwa
ulimwengu hadi leo Mungu hubaki kuwa Emanueli, yangu, Mungu pamoja nasi, Isa
7:14, 8:8, na Mt 1:23. Na hivi ndivyo alivyojidhihisha kwa kwana wa Israeli; “Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama
nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni,” Hos 10:5. Ni Mungu aliye sababu ya uhai wetu na mwenye
kuulinda na kuuneemesha. Mungu ndiye hitimisho letu. Uhai huu unafananishwa na
mti na matawi yake. “Matawi yake
yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama
Lebanoni,” Hos 10:6. Ni chini ya uvuli wa Mtu huu, yaani, uzima ndani na katika
Mungu kuna ufufuko na uzima wa milele. “Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama
ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai
ya Lebanoni,” Hos 10:7. Anayetupatia uzima na kuuchukua tena ndiye mwenye nguvu
na yapaswa kuabudiwa milele. Huyu ndiye mwenye njia ya kweli na iliyonyooka
licha ya fumbo katika njia yake. Naye anasema, “mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,” Isa 55:8. Ni fumbo kwa sababu licha ya kuishi
katika nafasi na muda, hakuna kati ajuaye kikomo chake. Yeye ndiye
ashikiliaye hayo mawili (muda na nafasi)
katika umilele wake. “Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda
katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake,” Hos 10:9b. Hivyo salama yangu na yako ni kuishi katika
haki. Ni katika haki hii tunapoufurahia uwepo wa Mungu kwa sababu usalama upo
licha ya ugumu wa kulielewa fumbo zima la maisha. Haki hii ndiyo hofu ya Mungu.
Hivyo,
kadiri ya Injili ya leo, kila mmoja wetu hufurahia matunda ya kazi yake. Kwa
upande mwingine tunapokuwa tayari kutumika kwa ajili ya Kristo yatupasa kuwa
tayari kutaabika kwa ajili ya Kristo. Kuishi maisha yanayompendeza Kristo ni
kutangaza vita dhidi ya ufalme wa giza. Hivyo, “Angalieni,
mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka,
na kuwa watu wapole kama hua,” Mt 10:16. Ni katika upole tunajifunza mambo
mengi. Huu ndio upole wa hua. Ni katika busara hufunuliwa yake yaliyojificha.
Huku ni kuwa kama nyoka.
Kumfuata
Yesu, kwatutaka kuikana nafsi, na hata wakati mwingine kwenda kinyume na
utaratibu tuliojijengea kutokana na mila na desturi zetu.
“Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana,
na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha,” Mt 10:21. Kusalitiana huku kwa weza kutokea tunapoyaishi
yale Kristo anayotuwasa. Tunapofuata njia yake, kuishi ukweli wake, na kulishwa
uhai wake, wengi watatutenga. “Nanyi
mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye
kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22
Kufaulu katika
mtihani huu wa maisha ndani na katika Kristo kwa tutaka kuvumilia hadi mwisho.
Ni katika kuvumilia twafikia tumaini lile la uzima wa milele.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nanyi mtakuwa
mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata
mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22
Tusali:-Ee Yesu tujalie
uvumilivu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario