domingo, 1 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 6 YA PASAKA

JUMATATU WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo: Mdo 16:11-15
Zab: 149: 1b-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Yoh 15:26-16:4
Nukuu:
Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo,” Mdo 16:14

Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha,” Mdo 16:15

Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26

Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada,” Yoh 16:2

Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi,” Yoh 16:4

TAFAKARI: “Uwepo wako kama Mkristo hai ni kutangaza vita dhidi ya uovu na shetani.”

Wapendwa wana wa Mungu, jana yaani dominika ya sita ya Pasaka tumeanza wiki ya sita ya Pasaka, na baada ya dominika ya Kupaa kwake Bwana wetu Yesu Kristo, tutasherekea Sikukuu ya Pentekoste. Ni tukio kubwa sana Kikanisa tunapompokea Roho Mtakatifu tuliyeahidiwa na Bwana wetu Yesu Kristo. Pamoja na Karama zake na Mapawa yake katika Kanisa, Roho Mtakatifu hufanya kazi  kubwa sana ya kutufanya kitu kimoja ndani na katika Kristo. Sifa mojawapo kubwa ya Roho Mtakatifu ni kutufanya wamoja, ikiwa ndiyo sala kuu ya Yesu Kristo kabla ya mateso na kifo chake, aliposali, Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.  Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja,” Yoh 17:19-22. Bila umoja huu, na mwongozo wa Roho Mtakatifu, maisha yetu kama Wakristo yapo hatarini kabisa. Hivyo, leo natulitafakari neno hili, “Uwepo wetu kama Wakristo hai ni kutangaza vita dhidi ya uovu na shetani.” Vita hivi vinaushindi pale tu tunapoishi na Kristo na kuongozwa na Roho Mtakatifu ambaye anatufunulia yote tusiyoyajua bado na kutufundisha njia sahihi ya kufuata.

Roho huyu Mtakatifu tunapewa pale tunapoyapokea Sakramenti yake Matakatifu, naye hutujaza neema na kutufanya kuwa wapya. Haya yote hufanyika kwetu si kwa juhudi zetu, wala kazi zetu, bali kwa mastahili yake Mungu mwenyewe. Hivyo, “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyotenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.” Tit 3:5-7.

Ni roho huyu kwa namna ya pekee huwaongoza walioridhiwa naye kuisha maisha yanayompendeza Mungu kama ilivyotokea kwa mwanamke yule, Lidia wa Filipi. Na mambo yalikuwa hivi, Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo,” Mdo 16:14. Mtume Paulo alitumika vizuri kwa jumuiya hii iliyoko Filipi, na hivyo anaacha kitu cha kuigwa. Ukweli ni kwamba, tunapoisha hapa duniani mwisho wa siku ya maisha yetu moja ya mambo haya mawili lazima litokee; kuwa MUHENGA au LIHOKA! Muhenga ni mtu yule anayeacha kitu cha kuigwa na wengine baada ya maisha yake, kama mchango katika jamii hiyo aliyoisha na kutoa maisha yake kama ushuhuda wa kiroho ma kimaadili. Lihoka ni mtu yule ambaye hakuacha chochote kama somo la kuigwa, na watu kujifunza kiroho na kimaadili. Hivyo mtu huyu anakuwa roho mbaya/ovu kwa jamii ile aliyoiacha, “bad spirit!” Kwa ushuhuda huu wa Mtume Paulo uko Filipi, anabakia kuwa Muhenga. Ndugu yangu, jambo hili linasema nini kuhusu utume wako na wito wako hapo ulipo?

Wapendwa, nimeanza kwa kusema moja ya kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ni kutufanya wamoja. Hivyo Roho huyu hakumpendelea tu Lidia kufanya kama alivyofanya baada ya kumpokea kupitia Sakramenti ya ubatizo, ila nyumba yake yote walijazwa neema ya Mungu, na kuishi katika hofu hiyo ya Mungu, na kuleta taswiri nzima ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Hivyo, Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha,” Mdo 16:15. Shurutisho hili wanalopata Mtume Paulo na mwenzake Barnaba, ni shurutisho la upendo uliotukuka. Yeyote anayeongozwa na Roho wa Bwana hakwishi kuwa na upendo wa kujitoa kwa wengine. Roho huyu huwa sehemu ya kwanza katika kuanzisha joto hilo la upendo kwa jirani, Roho huyu humwezesha mtu husika kujitoa bila kujibakiza, na mwisho Roho huyu humfanya mtu huyo kuwa na huruma.

Hakika kwa matendo haya ya Roho Mtakatifu kwa Mkristo ni sababu tosha ya kuwa na vita vya kudumu dhidi ya uovu, na hasa yule mwovu shetani. Katika hili Yesu anatuambia, Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada,” Yoh 16:2. Matendo hayo mema yafanywayo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwetu, ni Ibada tosha ya Mungu, kwani Mungu ni MWEMA. Hivyo mwovu shetani katika uovu wake, hatafurahiwa na jambo hili. Hata katika hali hii Yesu anatutumia Msaidizi wa kutufanya kubaki katika upendo na wema huu wa Kimungu. Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26. Roho huyu licha ya kutushuhudia kweli ya Kristo katika maisha yetu, anatufunulia yale yaliyo nje ya uwezo wetu wa Kibinadamu. Hivyo tendo hili linamfanya Mungu wetu kuitwa Mungu, na Waajabu muda wote kwa wale wenye hofu juu yake.

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu anatuambia haya yote ili itakapofika saa ile, yaani wakati ule wa kujaribiwa kwetu, na wakati ule wa kuutoa ushuhuda wetu mbele ya watu juu ya Kristo, tujue kwamba hatupo wenyewe, bali yupo nasi na haachi kutupigania. Hivyo, nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi,” Yoh 16:4. Hali hii inatukumbusha msimamo wetu kiimani hasa pale tunapokumbana na sintofahamu kwenye maisha yetu. Mkristo aliyeiva katika imani hii, mara zote Mganga yake Mkuu ni Kristo. Ndugu yangu, mara ngapi umemsaliti mganga huyu Mkuu Yesu Kristo na kwenda kwa akina “nsonganzingwe”? Embu tazama kifua chako, kiuno chako, shingo yako, paja lako la uso na sehemu nyingine ujuazo zilivyo chanjwa na kukufanya kama umevaa mkanda wa Rambo! Usicheke! “Jesus is the master key.” Mrushusu naye atatenda. Amina

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia,” Yoh 15:26


Tusali:-Ee Yesu, usinitoe katika kweli hii; wewe tu baki kwangu kuwa Njia, Kweli na Uzima. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario