JUMATATU
WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo:
Yak 3:13-18
Zab:
19:8, 9, 10, 15
Injili:
Mk 9:13-28
Nukuu:
“Lakini,
mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme
uongo juu ya kweli,” Yak 3:14
“Hekima
hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na
Shetani,” Yak 3:15
“Maana
hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak
3:16
“Lakini
hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari
kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina
unafiki,” Yak 3:17
“Na
tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18
“Akawajibu,
akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi
hata lini? Mleteni kwangu,” Mk 9:19
“Yesu
akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye,” Mk 9:23
“Mara
babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini
kwangu,” Mk 9:24
“Lakini
Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama,” Mk 9:27
“Hata
alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi
hatukuweza kumtoa?” Mk 9:28
TAFAKARI:
“Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.”
Wapendwa wana wa Mungu,
si jambo la ajabu leo kusikia kila kona kelele za watu wenye hofu ya Mungu
kukemea uvunjwaji wa haki za binadamu ulio waziwazi, na wa mchana kweupe.
Uvunjwaji wa haki huu unanzia pale ulipo, familia unayoishi, tamaduni ikiwa ni
pamoja na mila, desturi, na mazingira unayoyaishi, mfumo wa siasa unaouishi au
kurisishwa, uchumi unaotawala maisha yako kila siku, na Imani unayoishi
kutokana na yale unayoyaamini. Ndugu tunayesafiri sote katika tafakari hii, ni
vema ukajua kwamba huwezi kuongelea haki bila wajibu.
Haki ni tunda la wajibu
wako. Hivyo kama umewajibika vyema unayohaki na mastahili ya kile
ulichokiwajibikia. Ni kwa namna na mtazamo huu tunaongelea uvunjifu wa haki
pale mmoja wetu licha ya kuwajibika kama impasavyo haki yake inaporwa waziwazi
mchana kweupe. Uporaji wa haki hizi mara nyingi hufanywa na wale wenye “NGUVU”
katika sehemu husika. Jambo la ajabu ni hili; katika jamii yoyote ile wenye
“nguvu” hupewa dhamana hiyo na kundi hili linalohujumiwa na wenye “nguvu” hawa.
Kinachosikitisha ni kwamba, badala ya waliodhaminishwa kuwa watetesi, wao
wanakuwa wahujumu. Hawa ni wale wasiokuwa na hofu ya Mungu ndani yao, na
kipauwa mbele chao ni ubinafsi wao. Katika hali hii, amani kamwe haiwezi
ikatawala. Jamii ya mtindo huu huwa na utulivu wa kukubaliana kwa
kutokubaliana. Ni hali lenye kujionyesha kwa matumizi makubwa ya mabavu na
nguvu.
Ila jambo la kukumbuka
ni kwamba palipo na mgandamizo mkubwa wa nguvu pasipo nafasi ya kutokea, tokeo
lake ni mpasuko usiokifani. Hivyo tunahitaji amani katika maana ya kutambua utu
wa watu na tofauti zao katika kutenda na kufikiri. Tunahitaji amani kwa
kuheshimu matakwa ya wengi na yenye mwelekeo chanya wa namna watakavyo
kutawaliwa, kuwajibika, na kuuwajibisha utawala ule uliopewa dhamana na umma
wao. Ni katika amani hii tunaweza kuona matunda yake, yaani, haki ikitendeka
pasipo ghiliba. Hivyo, “tunda la haki
hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18. Na wale waitafutao na
kuifanya amani ni wale wasiyotanguliza mbele ubinafsi wao, wala falsafa za
makundi yao (vyama vya siasi), bali umoja wa wote katika utofauti wao, wakijali
uhalisi na Utaifa wao.
Wapendwa katika Kristo,
tunapopindisha kweli hii katika jamii, tuwe tayari kwa machafuko ya kila aina.
Na mwenye kujisifia katika mambo haya ni mpanda matatizo katika jamii husika na
matunda yake ni machafuko yasiyokwisha. “Maana
hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya,” Yak
3:16. Mtume Yakobo anasema, “Lakini, mkiwa
na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo
juu ya kweli,” Yak 3:14. Kweli ya kitu chochote kile haiwezwi pindishwa kwa
maslahi binafsi au ya kikundi cha walio wachache. Na kama ikiwezekana mafanikio
yake ni ya muda mfupi tu. Na hivi ndivyo Yesu asemavyo kuhusu kweli; “tena
mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:32. Tunapoipindisha
kweli ili tupate kuungwa mkono na wasio na ufahamu juu ya kweli, tutayapata ya
dunia hii kwa muda mfupi na kujeuka kuwa mashetani, yaani, wapinga kweli. “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu,
bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani,” Yak 3:15. Hekima
ishukayo kutoka mbinguni ni kweli ile ya Neno aliyemwilishwa na kukaa kwetu,
Yoh 1:14. Na huyu ndiye Kristo. “Basi Mwana
akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli,” Yoh 8:36. Mgandamizo wowote ule wa haki za watu hauwezi kamwe kuzika
kweli ya kile kilicho haki yao. Hivyo katika hali yoyote ile katika mwono huu,
amani haitakuwepo.
Yesu Kristo ndiyo
kielelezo cha haki kama tunda la amani. Kristo Yesu hakuja kuyatafuta yalio
yake binafsi, bali kutuweka huru katika utumwa wa dhambi. Hii ndiyo hekima
itokayo juu. “Hekima itokayo juu, kwanza ni
safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa
rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki,” Yak 3:17. Huu ndio wito
wa kila mmoja wetu mwenye hofu ya Mungu ambao mwisho wake ni kuwa wakamilifu
kama Baba wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Yesu anatukumbusha mwito huu na kusema,
“Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Ndugu yangu, pale ulipo simama katika
kweli, na kuwa mtetezi wa haki za watu wote, na kwa namna ya pekee wanyonge kwa
maana, “heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab 41:1.
Yote haya yanawezekana tu kama tunamwamini Yesu Kristo, na kile alichokijia
katika ulimwengu huu. Katika kweli hii, Yesu anawakemea wale wasiokuwa na imani
naye hasa katika Injili ya leo tunapoona wanafunzi wake wanashindwa kumtoa pepo
kijana yule aliyefikwa na mkasa ule. “Akawajibu,
akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi
hata lini? Mleteni kwangu,” Mk 9:19. Kumbe palipo na mashana na pasipo njia,
tuyapeleke mahangaiko yote hayo kwa Kristo kwa Imani thabiti na ya kweli.
Katika tendo hili la
Imani Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye,” Mk
9:23. Je, ukiweza nini? Ukiweza katika maana ilivyotumika hapa, inatukumbusha
kuwa na ufahamu pasipo shaka juu ya Yeye, yaani, Kristo ni nani kwetu. Naye
anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu yangu, bila Kristo hatuwezi
kufanya lolote lile, liwe dogo au kubwa, “maana
pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5b. Je, wewe na mimi
tuna jeuri katika kweli hii? Kwa nini basi kujifanya miungu watu?
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa kutambua ukweli huu, “mara
babaye yule kijana (aliyekuwa na pepo) akapaza sauti, akasema, Naamini,
nisaidie kutokuamini kwangu,” Mk 9:24. Kumbe tunapopotoka kutokana na hekima hizi
za dunia, ubinadamu, na ushetani, si vibaya tukajirudi na kutambua ubinadamu
wetu unaohitaji neema na huruma ya Mungu. Kristo yupo tayari muda wote
kutushika mkono tunapotambua pale tulipojikwaa na hasa kuzikuza nafsi zetu na
kutokumpa Mungu nafasi. Hivyo kwa neema na huruma hii ya Mungu, “Yesu akamshika mkono akamwinua naye
akasimama,” Mk 9:27. Tendo hili linakuwa
fundisho kubwa kwa wanafunzi wake Yesu. “Hata
alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi
hatukuweza kumtoa?” Mk 9:28. Kushindwa kwa wanafunzi wa Yesu ni moja na kuwa na
Imani haba ingawa Yesu anawaambia, “namna
hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba,” Mk 9:29. Kwa namna
nyingine ni kuwa na Imani thabiti.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini
hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari
kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina
unafiki,” Yak 3:17
Tusali:-Ee
Yesu, nitumie vyema kama chombo chako haki na amani katika hofu ya kweli ya
Mungu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario