SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA
BWANA WETU YESU KRISTO-C
Somo:
Mwa 14:18-20
Zab: 110:1-4 (K) 4
Somo
II: 1Kor 11:23-26
Injili:
Lk 9:11-17
Nukuu:
“Na
Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa
Mungu Aliye juu sana,” Mwa 14:18
“Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi
mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote,” Mwa 14:20
“naye
akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni
hivi kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:24
“Na
vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya
katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:25
“Maana
kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana
hata ajapo,” 1Kor 11:26
“Akawaambia,
Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki
wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula,” Lk 9:13
“Wakala,
wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi
na viwili,” Lk 9:17
TAFAKARI: “Wapeni ninyi chakula.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu
Yesu Kristo. Hiki ndicho kiini na uwepo halisi wa Kristo katikati yetu. Kwa
uwepo wa Mwili na Damu ya Yesu, mimi na wewe tulio wafuasi wake waaminifu
tunaunganishwa na kufungamanishwa na Upendo huu wa ajabu wa Bwana wetu Yesu
Kristo. “Sasa, basi, hakuna hukumu ya
adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa
sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali
na sheria ya dhambi na mauti,” Rum 8:1-2. Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu
Kristo ni chakula na Uzima wetu. Hii ndiyo Sakrameti Kuu ya Ekaristi Takatifu.
Sherehe hii ya leo inaturudisha nyuma na kutafakari kwa undani siku ile ya
Alhamisi Kuu ambayo ndiyo iliyokuwa siku rasmi kwa kusimikwa Sakramenti hii ya
Ekaristi Takatifu.
Kwa maumbo haya ya
Mkate na Divai, Mwili na Damu ya Yesu, Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni
uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu
anatuambia, “Mimi ndimi chakula
cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu
kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni
ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa
ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh
6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo
la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa
kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na
roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.
Wapendwa katika Kristo,
jibu la Yesu kwa wanafunzi wake, “Wapeni ninyi chakula, Yoh 9:13,” kwenye
Injili ya leo pale wanafunzi wake walipomwendea ili awaage makutano nao wapate
muda wa kujitafutia chakula, liliakisi kile kilicho tokea siku ile ya Alhamisi
Kuu, yaani wajibu (Mkleri) na kiini cha Sakramenti ya Daraja Takatifu. Hivyo
ili kuwe na mwendelezo wa chakula hicho-Ekaristi Takatifu, Yesu aliisimika
rasmi Sakramenti ya Daraja Takatifu siku hiyo ya Alhamisi Kuu na kuwaonyesha
kiini chake, yaani, kuwa watumishi na kutumika vilivyo kwa upendo wa kimungu,
kwa tendo lile la kuwaosha miguu wanafunzi wake. Yesu kwa jibu lake hili
anaonyesha utashi wake ikiwa na kukubali kwamba kwa hitaji hilo walilokuwa nalo
wanastahili chakula. Pili, anawataka kwanza Mitume wake watoe kile walichokuwa
nacho na kukishirikisha kwa upendo.
Leo Mama Kanisa
anaposheherekea Sikukuu hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo,
tunakumbushwa pia wajibu na kiini cha Sakramenti ya Daraja Takatifu, vile vile
bila kusahau ushiriki wetu katika ukuhani wa kawaida kwa kila Mbatizwa kwa
Sakramenti ile ya Ubatizo (kupakwa mafuta Matakatifu ya Krisma, na kuunganishwa
na taifa lake Mungu, kuendelea kuwa kiungo cha Kristo, kuhani, nabii na mfalme,
hadi uzima wa milele Mbinguni). Kwa mantiki hiyo, Kanisa kama mwili wa Kristo
uliojengwa na Wabatizwa wote, na Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, linawajibu
wa kuwalisha chakula waamini wake, wale wote wenye hofu ya Mungu, na wale ambao
bado hawajamjua Kristo.
Jamii inayotuzunguka
licha ya itikadi zao za kidini, siasa, utamaduni na desturi, wana njaa ya mwili
na roho. Kama Kanisa linalosafiri-Kanisa la hija, lililosheni watakatifu na
wadhambi, ni wakati wa kutafakari kwa makini zile heri nane kama zilivyoandikwa
na Mwinjili Mathayo 5:3-11, na kwa namna ya pekee mstari ule wa sita na tisa. “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao
watashibishwa. Heri wapatanishi;
Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:6,9. Jamii yetu ya leo ina njaa na kiu
ya haki. Mtu katika ukamilifu wake ni mwili na roho. Mtu huyatamani yaliyo ya
roho kama haya ya kimwili yapo sehemu yake na katika umaana wake. Hivyo, mtu na
utu wake lazima uheshimiwe na kupewa stahili zake. Haki ya mtu kama tokeo la
kuwajibika kwake lazima ilindwe na kutetewa kwa nguvu zote bila kupepesa macho.
Ni kazi ya kila Mbatizwa kama Kanisa, na Kanisa kama Chombo na Sakramenti ya
Wokovu, ‘kuwapa chakula’ katika maana ya kuamsha dhamiri zilizo lala, kuzijenga
dhamiri zilizoharibiwa na kudumaa, na kuzifufua dhamiri zile zilizokwisha kufa,
ile duniani hapa tunapoishi pale mahali salama kama sehemu pekee ya kujiandaa
kwa maisha ya umilele.
Kila
kukicha ulimwengu huu wa leo unapoteza usalama wake kwa sababu tu wapo watu
wachache kwa ubinafsi wao (uroho wa madaraka) wanatumia vibaya uhuru na
madaraka yao na kuzalisha machafuko. Katika eneo hili kila Mbatizwa anaalikwa
kuulisha ulimwengu kuanzia pale alipo kwa kuwa mpatanishi. Kabla ya yote
yakupasa kujipatanisha nafsi yako mwenyewe, wewe na jirani yako, wewe na
mazingira yako, na wewe na Mungu. Upatanisho huu utuepusha na dhambi ya
kijamii. Kwa kuishi na kufanya hivyo tunautendea haki ukuhani wetu wa kawaida,
na unabii wetu. Nafasi uliyonayo leo kama Mkristo ni taa na nuru pale ulipo.
Kristo ni kielelezo cha Nuru halisi kwetu licha ya kwamba walio wake, yaani,
mimi na wewe kila siku tunamkataa.
“Alikuwako
ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu
haukumtambua,” Yoh 1:10. Hivyo ndiyo maana ukuhani wa Kristo unafananishwa na
ule wa Melkizedeki Mfalme wa Salemu. Historia yake haijulikani sana zaidi ya
kile alichokifanya kama kuhani na Mfalme. Kumbe kwa muono huo mimi na wewe
tunashirikishwa ukuhani wa Kristo bila kujali historia zetu wala makabila yetu.
Sote tunaitwa kuhudumu na kuwa wahudumu ndani na katika Kristo. “Na
Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa
Mungu Aliye juu sana,” Mwa 14:18. Kwa nafasi yake kama kuhani anamlisha Abramu
kwa kumbariki. “Akambariki,
akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi,”
Mwa 14:19. Na mwisho kwa uwepo wa Abramu
anamsifu Mungu na kuwa mpatanishi kati ya Abram una maaduni zake kwa kuitafuta
amani. “Ahimidiwe
Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu
la kumi la vitu vyote,” Mwa 14:20.
Leo
Kanisa linaposheherekea Sikukuu hii ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu
Yesu Kristo, tunakumbushwa kuwa wakarimu. Yakupasa kuwa mkarimu ukitambua
thamani ya kukombelewa kwako. “Nanyi
mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu;
mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa
damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya
Kristo,” 1Pet 1:18-19. Kwa kutambua thamani hiyo, niwe mkarimu kuanzia pale
nilipo ikiwa ni kwa wote wanaonizunguka. Niwe mkarimu na kujitoa katika Kanisa
kwa vipaji vyangu na mali alizonijalia Mungu ili shughuli zake za kimisionari
zisonge mbele na Kristo afikiwe kwa wate wote wenye njaa na kiu ya haki. Hivyo
nikumbuke kuishi katika kiasi na kuwajali wengine.
Niepuke mara zote matumizi
mabaya ya mali na kutapanya kile kilichozidi au baki baada ya kupata hitaji
langu. “Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande
vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili,” Lk 9:17. Vikapu kumi na viwili, ni idadi ile ya jumla ya
makabila yale kumi na mbili ya Wayahudi, yaani wana wa Yakobo. “Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili. Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa
kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni. Wana wa Raheli, ni Yusufu na
Benyamini. Wana wa Bilha,
kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali. Wana
wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo
aliozaliwa katika Padan-aramu,” Mwa 35:22b-26. Kumbe tukiwa wakarimu na
kushirikishana kwa upendo yale tuliyojaliwa kwa ukarimu na Mungu, hakuna
atakayekosa.
Tujifunze kutoka mshumaa. Mshumaa upiga
vita giza (njaa na kiu ya haki), na wakati huo huo kutoa bila kujibakiza
(kuepuka ubinafsi, uroho wa madaraka, kujilimbikizia na kuwa sababu ya
machafuko). Kumbe mimi na wewe haitoshi kulalamika tu bila kufanya chochote ili
hali twaweza kubadili hali pale ulipo na kwa nafasi uliyo nayo. Kama si umeme
uwe mshumaa, na kama si ushumaa ule kijinga cha moto. Hakuna sababu ya kupiga
kelele chumbani kuna giza tororo ilhali umeushika mshumaa. Washa mshumaa huo,
na ingia chumbani. Kuwa nuru na mwanga pale ulipo. “Wapeni ninyi chakula.”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wakala,
wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi
na viwili,” Lk 9:17
Tusali:-Ee
Yesu, nifundishe ukarimu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario