lunes, 2 de mayo de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA WATAKATIFU FILIPO NA YAKOBO MITUME

SIKUKUU YA WATAKATIFU FILIPO NA YAKOBO MITUME
3/5
Somo: 1Kor 15:1-8
Zab: 19:2-3, 4-5
Injili: Yoh 14:6-14
Nukuu:
 “ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko,” 1Kor 14:3b 

na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko,” 1Kor 15:4 

baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote,” 1Kor 15:7

 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6 

Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha,” Yoh 14:8 

 “Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh 14:10 

Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11 

Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12 

Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13

Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya,” Yoh 14:14 

TAFAKARI: Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Naam ninaamini.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Watakatifu Pilipo na Yakobo Mitume. Kadiri ya mapokeo ya Kanisa, Mtume Filipo alizaliwa Bethaida na alikuwa mwanafunzi wa kwanza wa Yohana Mbatizaji na baadaye alimfuata Yesu Kristo. Yakobo mwana wa Alfayo, mtumwa wa Mungu, na wa Bwana Yesu Kristo Yak 1:1, alichaguliwa na kuliongoza Kanisa la Yerusalemu. Mtume Yakobo aliandika moja ya waraka wa Kanisa kwa watu wote, “Barua ya Yakobo.” Kama kiongozi wa Kanisa la Yerusalemu, Yakobo Mtume aliishi maisha kamili na ya mateso mengi kwa ajili ya Imani, na kwa tendo hilo aliwaongoa Wayahudi wengi katika Imani na kumfuata Kristo. Alikufa kifo shahidi mwaka 62 baada ya Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Paulo Mtume na wengine, msingi wa Imani kwa Wakristo upo kwenye kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kifo cha Kristo ambacho ni tokeo la dhambi zetu, kimetufanya sote tuhesabiwe haki mbele ya Mungu na kupata mastahili ya kuwa watoto wake Mungu na warithi Ufalme wake, 1Kor 14:13. Hapa ndipo ulipo uhai wetu kwa sababu, alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona,” Isa 53:5.  Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo uliamsha hari mpya na maisha mapya katika ufuasi wake. Huu ni wito wa kila mmoja wetu kuishi maisha mapya na Kristo, yaani, maisha ya ufufuko. Maisha haya ya ufufuko yanatudai kila siku kulenga katika ukamilifu licha ya kwamba udhaifu upo. Kwa maana nyingine, kama mfuasi wa Kristo na kama ilivyokuwa kwa Filipo na Yakobo Mitume, tusijiridhishe hata mara moja katika hali ya udhaifu wetu na kumsaliti Yesu kwa matendo yetu maovu na dhambi.

Maisha haya ya ufufuko na mapya kwa kila mfuasi wa Kristo ni maisha ya ushuhuda kwa yale aliyotufundisha Kristo na kuyaona kila siku ya maisha yetu. Hata hivyo hatuwezi kuwa mashahidi wa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo kama hatupo tayari kushirikishana habari njema ya wokovu wetu. Pili, hatutaweza kushirikishana habari hii njema ya wokovu kama hatupo tayari kulitafakari neno lake. Tatu, hatutaweza kulitafakari neno lake kama hatupo tayari kulipokea neno hilo na habari njema hiyo ya wokovu. Na nne, hatutaweza kulipokea neno hili la wokovu kama hatupo tayari kulisika. Hivyo, mwito wa kuwa mashahidi wa ushuhuda wa ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na habari njema ya wokovu wetu, kwatutaka kufanya haya yafuatayo: Kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, na kulishirikisha neno. Hivi ndivyo walivyofanya Mitume hawa Filipo na Yakobo, na Mitume wote wa Kristo, na wale wote waliomfuata hasa tunapolitazama Kanisa hili la Mwanzo. Kwa ushuhuda wao, na kifo dini chao kwa kumwaga damu zao kwa ajili ya Mwana-Kondoo wa Mungu, Kanisa limekuwa na msingi Imara na Imani hadi leo.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, maisha na ufuasi wako kama Mkristo lazima yaongozwe na malengo hayo niliyoyasema kama kweli wataka kuwa ndani na katika Kristo Yesu. Naye Yesu anakuambia wewe na mimi hivi; Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11. Ndugu yangu, hapa ni Imani ya kweli katika Kristo Yesu! Na msingi Imara ni kumwona Kristo pasipo shaka yoyote katika mambo haya matatu anayotuambia, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Maana ya maneno haya ni nini? Ndugu yangu kama nilivyokwisha kusema mahali pengine, si vibaya nikakukumbusha na leo pia. Yesu Kristo ni njia kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua Yesu ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukuliana kindugu katika misalaba ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu, tunakutana naye Kristo katika hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii tunakutana nayo katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi wa neno.

Na Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake,  Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa ndani yetu. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.

Kwa uelewa huo, Yesu Kristo anamtoa mashaka Filipo pale alipomtaka Yesu awaonyeshe kwa Baba nayo inatosha, Yoh 14:8. Kuthibitisha kwamba Yeye, yaani, Kristo ndiye Njia, Kweli, na Uzima, na ndiyo mlango sahihi wa kumfika Baba, na Ufalme wa mbinguni, anasema, Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Ndugu yangu, kwa kumwishi Kristo na kumwamini una kitu cha kupoteza? Maneno haya ya Yesu kwamba yeye ni njia, kweli, na uzima si maneno ya kufikirika bali ndio kweli yenyewe na jibu sahihi alilolitaka Mtume Filipo. Je, bado unamashaka? Kama bado upo kwenye mashaka, Yesu anakuambia,  Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13. Hatupaswi kuwa na mashaka kama kweli twataka kuishi maisha mapya, yaani, maisha ya ufufuko.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya,” Yoh 14:14

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, wewe kwetu watosha. Amina
Watakatifu Filipo na Yakobo, Mtuombee.


No hay comentarios:

Publicar un comentario