JUMANNE
WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo:
Yak 4:1-10
Zab:
55:7-8, 9-10a, 10b-11a, 23
Injili:
Mk 9:29-36
Nukuu:
“Mwatamani,
wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na
kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!” Yak 4:2
“Hata
mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,”
Yak 4:3
“Enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila
atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu,” Yak 4:4
“Lakini
hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao,
bali huwapa neema wanyenyekevu,” Yak 4:6
“Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia,” Yak 4:7
“Mkaribieni
Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na
kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili,” Yak 4:8
“Huzunikeni
na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha
yenu kuwa hamu,” Yak 4:9
“Kwa sababu
alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa
katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu
atafufuka,” Mk 9:31
“Akaketi chini,
akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa
mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35
TAFAKARI:
“Hofu ya Mungu, maisha ya sala na maombi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kufanikiwa katika maisha yanayoongozwa na malengo, ni kuishi maisha
yanayosukumwa au kuongozwa wakati wowote na hofu ya Mungu, sala na maombi.
Maisha yenye mtazamo huu kwa ujumla wake utufikisha kwenye kusudio la maisha ya
kiroho. Kuongozwa au kusukumwa na hofu ya Mungu uturejesha kwenye kusudio la
uumbaji wetu, na hali yetu halisi, yaani, ubinadamu wetu. Hofu hii ya Mungu
umulika na kutukumbusha kila mara kusudi la kuumbwa kwetu, yaani, tumjue Mungu,
Kumb 6:5, tumpende Mungu na majirani zetu, Mt 22:29, kumtumikia Mungu na wale
tuliopewa dhamana juu yao, Gal 5:13, na mwisho tuupate uzima wa milele. Hii ni
hatua ya mwisho kama asemavyo Mtume Paulo katika kuvipiga vita vile vya imani
hapa dunia, yaani, “mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa
watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa
milele,” Rum 2:22. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, hayo ndiyo
maisha yanayoongozwa au kusukumwa na hofu ya Mungu.
Ndugu yangu, hatutaweza
kuifikia hali hiyo kama tutabebwa na wimbi la dunia tunaloishi leo kama
litakavyo. Tunaishi katika ulimwengu wa ushindani, na wakati mwingine pasipo
washindani au washindaniwa. Ni ulimwengu wa vitu, na utafutaji wa vitu kila siku hata kama havina tija leo na
kwa sasa. Mtindo na mtazamo huu wa maisha huaribu na upoteza lengo na sababu ya
kuumbwa kwetu. Hofu ya Mungu hutoweka, na maisha ya sala na maombi hukosa ladha
yake, kama Mtume Yakobo asemavyo, “Mwatamani,
wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na
kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!” Yak 4:2. Maisha yenye msukumo huu
kamwe mbele ya safari hayana ushindi. Ni kushindwa tu! Ni maisha yaliyokosa
malengo. Na ndiyo maana kama asemavyo Mtume Yakobo, “hata
mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,”
Yak 4:3. Tunaomba vibaya na kuvitumia vibaya
kwa sababu maisha yamepoteza shabaha yake, yaani uzima wa milele. Ni maisha
bila hitimisho ambalo kwa uhakika lipo, yaani, maisha ya umilele.
Ndugu yangu, ni kweli pasipo shaka
kabisa kwamba usipo thamini umilele kama hitimisho la maisha yako, nguvu na
akili zako zote zitajikita kwa haya ya leo na kesho ambayo kwa uhakika kama
yalivyo hayana umilele. Katika kweli hii Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na
wevi huvunja na kuiba; bali
jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi
hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa
hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:19-21. Ndugu yangu,
chunguza kile kinachochukua muda wako mwingi hapa duniani na ujiulize kama kina
uhusiano na umilele wako mara baada ya maisha haya hapa duniani.
Wapendwa
wana wa Mungu, Yakobo Mtume anatupa karipio zito pale tunapokosa mwelekeo
sahihi wa maisha ya hapa duniani, na uhusiano wake, yaani, maisha ya milele. Na
kwa sababu hiyo anasema, “enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila
atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu,” Yak 4:4. Ndugu
yangu, tukiwa na uadui na Mungu kuna kushinda kweli vita hiyo? Hakika hakuna
kushinda! Hivyo pamoja na raha na anasa zake mwisho wa siku hakuna faida
yoyote. Basi kila mmoja na haihoji dhamiri yake kwa swali hili la Yesu kama
anavyotuuliza, “Kwa kuwa itamfaidia mtu
nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi
yake?” Mk 8:36-37. Ndugu yangu, pasipo shaka sindano hiyo imekuingia vizuri.
Tafakari!
Wapendwa wana wa Mungu,
ili tufikie lengo la maisha ya kiroho twahitaji kuishi na kukumbatia muda wote
fadhila ya unyenyekevu. Unyenyekevu uturudisha katika hali ya ubinadamu wetu
pale tunapotaka kujiumba na kuvaa taswira nyingine kama tokeo la majivuno yetu,
mafanikio yetu kimaisha, na hata ufahamu wetu. Ndugu yangu, chochote kile
kitakachojiumba kama tokeo la kujikuza zaidi na kuipoteza ile hofu ya Mungu ndani
yako, mwisho wake ni kupoteza dira ya hitimisho la maisha yako, yaani, umilele
wake. Hofu hii ya Mungu, na kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, “hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema,
Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu,” Yak 4:6. Ndugu
zangu, tusipokuwa na hofu hii ya Mungu hatutaweza kumtii Mungu na wala
kumkaribia kwa sababu Mungu hatakuwa na nafasi ndani ya moyo wako. “Basi
mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia,” Yak 4:7. Na kwa namna hiyo
hiyo Yakobo Mtume anatuambia, “mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.
Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye
nia mbili,” Yak 4:8. Hili litawezekana tu pale tutakapokuwa tayari
kujinyenyekesha na kuiishi hofu ya Mungu.
Wapendwa katika Kristo,
maisha ya unyenyekevu na hofu ya Mungu hayatupeleki tu karibu na Mungu, bali
utufanya kuwa tayari kutahabikiana katika hali zote za maisha na mahangaiko
yake. Hivyo, huu ni mwaliko kwako na kwangu wa kufanya toba ya kweli na
kumrudia Mungu. “Huzunikeni na kuomboleza
na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu,”
Yak 4:9. Kujishusha huku ndiko kujidhili
mbele za Mungu, naye atatukuza, Yak 4:10. Pasipo kujishusha ni vigumu kuyaona
mahangaiko ya wengine na kuyabeba kama moja ya changamoto na misalaba yenye
nuru ya Utukufu. Yesu anataka tulione jambo hili vizuri ikiwa yeye ndiye
kielelezo chetu. Hivyo ni “kwa sababu alikuwa akiwafundisha
wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu,
nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka,” Mk 9:31. Hata
hivyo Mwinjili Marko anatuambia hawakulifahamu neno lile kwa sababu walijawa na
uoga na hivyo walishindwa kumuuliza Yesu, Mk 9:32
Ndugu yangu, kutokujishusha
hakutatuandaa na kuwa tayari kutumika kwa ajili ya wengine. Je, kila mmoja wetu
akiupenda ukubwa bila kutumika tutaepuka machafuko? Wanafunzi wa Yesu, yaani
wale Thenashara, wanapatwa na ushindani huu wakiwa njiani wakipita katikati ya
Galilaya na Yesu, Mk 9:34. Yesu anawaambia kiini cha ukubwa huo wanaoutamani. “Akaketi
chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa
wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35. Ukubwa ni utumishi, na
kutumika kweli kwa ajili ya wote pasipo kuweka mbele faida au maslahi binafsi.
Huu ndio ule utumishi usio na faida kama anavyotuambia Yesu; “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote
mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa
kufanya,” Lk 17:10. Hakika sote leo tuliopewa dhamana ya uongozi katika nyanja mbalimbali katika Taifa letu-
Tanzania, tungaliishi hofu hii ya Mungu na kweli katika hali ya kutumika,
Kristo angeonekana kwa kila mtu.
Tusifu
Yesu Kristo!
“Mtu
atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk
9:35b
Tusali:
Ee Yesu Mwema, tujalie fadhila ya unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario