SHEREHE
YA PENTEKOSTE
Somo:
Mdo 2:1-11
Zab: 104:1, 24, 29-30, 31, 34
Somo
II: 1Kor 12:3b-7, 12-13
Injili:
Yoh 20:19-23
Nukuu:
“Kukawatokea
ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao,” Mdo
2:3
“Wote
wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho
alivyowajalia kutamka,” Mdo 2:4
“Basi
sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa
kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe,” Mdo 2:6
“Wakrete
na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu,”
Mdo 2:11
“Wala hawezi mtu
kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu,” 1Kor 12:3b
“Basi
pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni
yeye yule. Kisha pana tofauti za
kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote,” 1Kor
12:4-6
“Maana
kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule,
navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12
“Basi
Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami
nawapeleka ninyi,” Yoh 20:21
“Naye
akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu,” Yoh 20:22
“Wo
wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa,” Yoh 20:23
TAFAKARI:
“Na tutende kadiri ya Roho wa Bwana na si kadri ya mazoea yetu, familia zetu,
koo zetu, makabila yetu, mazingira yetu, tamaduni zetu, mitazamo yetu, itikadi
zetu na utaifa wetu. Pokea Roho Mtakatifu, na uanze safari mpya ya ubatizo
katika Roho Mtakatifu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo Mama Kanisa anasherehekea Sikukuu ya Pentekoste. Ni sikukuu ya
kuvuviwa kwa Kanisa na wana wake. Pentekoste ni sikukuu ya kuzaliwa Kanisa.
Pentekoste kama ilivyo katika mila na desturi ya Kiyahudi, huadhimishwa baada
ya majuma saba, yaani siku 49 baada ya jumapili ya Pasaka. Kwa maana nyingine
Pentekoste ni siku hamsini takea tukio kubwa la Ufufuko wa Bwana yetu Yesu
Kristo. Masomo yetu yote matatu ya siku ya leo yanalenga tukio hili kubwa baada
ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu. Ni siku ya kufanywa upya vyote katika
Yesu Kristu yaani Upyausho. Ni siku ya furaha kubwa kwa kila mbatizwa,
tunapoalikwa kama wana Kanisa na familia ya Mungu kutenda kadiri ya Roho wa
Bwana na si kadiri ya mazoea yetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu,
mazingira yetu, tamaduni zetu, mitazamo yetu, itikadi zetu na utaifa wetu. Roho
Mtakatifu anasukuma na kutuwezesha kuwaza, kusema, na kutenda zaidi ya mipaka
yetu ya kibinadamu. Huku ndiko tunapoalikwa kama wana wa Mungu.
Mitazamo hii
imeshavunjwa na Roho Mtakatifu ambaye sifa yake moja kuu ni ‘Umoja katika
utofauti wetu.’ Kwa hiyo Roho Mtakatifu leo anatualika wote kuanza yote katika
yeye-Roho Mtakatifu na kuyatakatifuza yote katika Kristo.
Somo la kwanza linatupa
taswira nzima ya maisha ya kijumuiya na namno walivyokuwa wanaishi kwa hofu na
sintokujua nyingi. Roho Mtakatifu anavunja ukimya huu na kuwa furaha na ujasiri
mkubwa wa kuishi na kuyaneno mambo makuu ya Mungu. Somo la pili linatupa
mwangaza wa maana halisi ya maisha ya Mkristo, ikiwa ni pamoja na kuishi kadiri
ya Roho wa Bwana tukisaidiana na kutabikiana katika shida na raha. Umuhimu huu
wa maisha ya Mkristu huambana na matumizi mazuri ya karama, utoaji wa huduma,
na utendaji. Na mwisho somo la Injili linatufundisha mambo makuu mawili; zawadi
kubwa ya ufufuko wa bwana wetu Yesu Kristo ikiwa ni amani ya kweli, na
kusimikwa rasmi kwa Sakramenti ya Upatanisho.
Wapendwa wana wa Mungu
katika Kristo mtazame mwenzako uliyekaa naye na umshike mkono umwambie mateno
haya; “Pokea Roho Mtakatifu, na uanze safari mpya ya ubatizo katika Roho
Mtakatifu.” Umoja katika maisha ya kijumuiya, Roho Mtakatifu anavunja
sintofahamu zake, hofu, mashaka na kutujaza nguvu mpya na mtazamo mpya na FURAHA
ya kweli kama tulivyosikia kutoka somo la matendo ya Mitume. Kila mmoja
anapigwa mshangao kwa tukio la ujio wa Roho Mtakatifu. Wasiojua siri hiyo
wanaulizana kama Wayahudi walivyofanya, “Tazama, hawa wote wasemao si
Wagalilaya? Imekuaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?”
Mdo 2:7. Hilo ndilo bomu la pili la FURAHA katika Kanisa ikiwa la kwanza ni
Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Jambo hili
linanikumbusha familia mbili za jirani ambapo familia moja kulisikika sauti za
furaha na wimbo ulisikika kwa lugha ya kiingereza ukisema, “Happy birthday to
you.” Familia ya pili ya jirani yake, yaani kwa Mzee Haijalishi, mwanaye Maria
alimuuliza baba yake, “kulikoni hapo kwa jirahi muda huu wanafurahi na kuimba
happy birthday to you; ni nani huyo wanayemsherekea?” Mzee Haijalishi bila
kusita alimjibu mwanaye Maria na kumwambia, “nafikiri huyo atakuwa anaitwa, ‘to
you.” Wapendwa katika Kristo leo ni sikukuu kubwa ya “to you” wetu yaani, Roho
Mtakatifu. Huu ndio mshangao wanaopigwa wasio fahamu siri hii. Hata leo katika
Kanisa bado wapo watu tunaoshangazwa na mkusanyiko wa sala wa Wanakarismatiki.
Hatuachi kuwanenea visivyo na kusema hawa ni wapenda kelele na kulia muda wote.
Je, tumeenda kusali nao na kuona sababu za kelele zao? Je, yawezekana umati huu
wote wa watu ni wendawazimu? Na
nani basi kawatia wendawazimu
huo?
Tunapozidi kutafakari
matendo haya makuu ya Mungu, Mtume Paulo katika somo la pili anatutabanaisha
taswira halisi ya maisha ya wale wote waliobatizwa katika ubatizo huu wa Roho
Mtakatifu. Wazo kuu la Mtume Paulo ni kututafakarisha uzuri wa umoja katika
utofauti wetu. Uzuri na umoja huu katika utofauti unajionyesha katika karama,
utoaji wa huduma na utendaji. Umoja ni tunda la Roho Mtakatifu katika maisha ya
Kanisa na wana wake. Kwa hiyo, kielelezo cha karama ni Roho Mtakatifu.
Kielelezo cha huduma ni Kristo mwenyewe, na kielelezo cha utendaji ni Mungu
mwenyewe. Haya yote ni kwaajili ya kufaidiana, (IKor 12:7). Kila mmoja wetu kwa
kile alicho si kwa manufaa yake tu, bali ni kwa ajili ya wengine pia. Jambo
hili huenda sambamba na maisha halisi ya kila siku. Iwe furaha au mateso
kwangu, mwenzangu na jirani yangu vyote vinanihusu kama mwana Kanisa na
mbatizwa.
Uhalisia huu wa maisha unanikumbusha hadithi hii. Mzee
Fungamali na mkewe Mama Matumizi walikuwa wakulima na wafugaji maarifu sana
katika kijiji cha Changamkeni. Kwa muda mrefu walisumbuliwa sana na panya kwani
waliharibu sana nafaka walizokuwa wakivuna kama mahindi na ngano. Baada
ya kutafakari jambo hili, waliazimia kununua mtego wa pacha. Basi siku ya
jumatano kila wiki huwa kuna gulio katika kijiji chao cha Changamkeni. Mzee
fungamali alikwenda na kununua mtengo wa panya ikiwa ni pamoja na kipande cha
samaki kama chambo.
Akiwa sebuleni Mzee
Fungamali aliutoa mtego huo ndani ya mfuko huku panya mmoja akiwa anaangalia
kwa makini kinachoendelea kupitia kati ya moja ya nyufa za nyumba ile. Hakika
panya yule alijua mtego huo ni kwa ajili yake na familia yake kwa kile walichokuwa
wanakifanya. Ila kwa upendo aliokuwanao panya mchana ule ule aliona ni jambo la
busara kutoa angalisho kwa wengine kama; kuku, mbuzi, nguruwe, na ng’omba.
Safari ilianza kwa
wanafamilia kuku, “jamani, jamani kuna mtego wa panya ndani ya nyumba ya Mzee Fungamali,”
panya alisikika akisema. “Hilo halituhusu sisi. Toa uwendawazimu wako hapa,”
Kuku walimjibu kwa dharau. Mguu wa pili ulifika katika familia ya mbuzi.
“Waheshimiwa mbuzi, jamani kuna mtego wa wanya katika nyumba ya Mzee Fungamali
kuweni waangalifu,” panya alisema kwa msisitizo. “Mtengo wa panya, aaaaha!
Mtego huo na mbuzi wapi na wapi bwana? Ondoka zako unatupotezea muda hapa!”
Mbuzi walijibu kwa kujiamini na kuona ni kituko cha mwaka.
Basi panya hakuchoka. Aliondoka mara ile hadi
katika familia ya ng’ombe. “Waheshimiwa wakubwa zangu ninajambo mahususi la
kuwaambia. Nyumbani kwa Mzee Fungamali kuna mtego wa panya. Kuweni waangalifu
sana,” panya aliyasema hayo kwa msisitizo mkubwa. “Hivi hujatambua kuwa mtego
huo ni kwa ajili yako? Tazama miguu yetu, je hako kamtego kanaweza kubana kwato
zetu? Tafakari kwa kina,” ng’ombe walisema huku wakimsikitikia panya. Hata
hivyo panya hakukata tamaa na badala yake aliimaliza safari yake kwenye familia
ya nguruwe. “Wapendwa mnaopendwa na wengi naomba niwape ujumbe huu muhimu.
Kwenye nyumba ya Mzee Fungamali kuna mtego wa panya. Hivyo nawaomba muwe
waangalifu sana.” Panya aliyasema hayo kwa unyenyekevu mkubwa huku koo likiwa
limemkauka kwa kauli mbiu yake ile. “Ebo! Embu tuondolee giza hapa. Kiguru na
njia kote huko ni kutuletea ujumbe wa kipuuzi namna hii? Umekosa la kufanya?
Nguruwe walijibu kwa majigambo makubwa na uelewa mpana kadri ya uzoefu wao.
Basi panya alijirudisha taratibu katika nyumba ile ya Mzee Fungamali na kuwa
makini na mtego ule.
Usiku ule kulikuwa na
mvua kubwa sana. Hivyo chatu mmoja mkubwa alijipenyeza na kuingia katika nyumba
ya Mzee Fungamali kujisitiri kutokana na mafuriko yaliyotokea kwenye shimo
lake. Kutokana na harufu ile ya samaki, chatu huyu alitafuta chanzo cha harusu
ile. Mwishowe ilisikika sauti ya kufyatuka mtego. Panya wote walishtuka na
kutaka kujua kulikoni. Mama wa familia pia alisikia sauti ya mfyatuko huo wa
mtego. Alijua hakika panya keshanaswa. Basi, Mama mwenye Nyumba aliamka na
kwenda kutazama mtego. Mara alisikia maumivu kwenye mguu wake wa kushoto. Chatu
yule alimng’ata kwani mtego ulimpana mkiani tu. Kelele za Mama wa nyumba
zilimwamsha Mzee Fungamali. Mzee Fungamali alipambana na kuweza kumwua chatu
yule, ili hali ya mkewe ikiwa mbaya sana. Alimkimbiza mkewe hospitalini usiku
ule ule kwa baiskeli. Alipewe huduma ya kwanza na kulazwa. Asubuhi yake, mama
Matumizi aliomba aandaliwe supu ya kuku. Basi kuku alichinjwa na supu
ilipelekwa hospitalini. Baada ya siku tatu mama akiwa anapelekewa supu ya kuku,
hali yake ilibadilika na jioni yake alifariki. Kijiji kizima kilisikitishwa na
msiba ule. Kutokana na umaarifu wa familia ile, Mzee Fungamali alilazimika
kuanda chakula cha kutosha kwa kijiji kizima na wageni kutoka nje ya kijiji
kile. Hapa kuku, mbuzi, ngombe walichinjwa kuwezesha kitoweo kwa kundi kubwa
lile la watu. TUWE WAANGALIFU KUNA MTEGO WA PANYA!
Wapendwa wana wa Mungu,
mambo yote yanayomuhusu mwenzangu ni yangu pia na yananihusu licha ya utofauti
wa kimaumbile, hali, na nafasi tulizo nazo katika jamii. Huku ndiko kufaidiana
katika shida na raha. Karama, huduma, na utendaji vilenge katika maisha ya kila
siku katika jamii tunayoishi na hasa kwa wana Kanisa katika kufaidiana. Mtego
wa panya jamani!
Somo la Injili
linatufundisha mambo makuu mawili; Amani kama tunda kuu na zawadi nzito ya
Kristu mfufuka anapowatokea mitume wake na kusema, ‘Amani kwenu.’ Yoh 20:19-20.
Jambo la pili ni kuwekwa rasmi kwa Sakramenti ya Upatanisho au Kitubio.
Sakramenti hii ni tiba ya majeraha yetu kiroho na kimwili. Ni upendo wa Mungu
katika ukengeufu wetu katika kuuishi Upendo na Huruma ya Mungu. Kwetu sisi
waamini, Sakramenti ya kitubio ni heshima kubwa kwa kurudishiwa tena hadhi yetu
ya kuwa wana wa Mungu baada ya kuasi. Rejea Mwana mpotevu (Lk 15:11-32). Ni
daraja ambalo linatuwezesha kupita pamoja bila kujali uzito wa dhambi zetu, kwa
sababu Huruma na Neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Muhumili wake ni
Kristu mwenyewe katika Padre ambeye ni Kristu mwingine. Ni heshima kubwa kupita
katika daraja hili. Kuna usalama zaidi kwa sababu daraja hili halikujengwa kwa
mbao, chuma, wala zege bali ni Kristo mwenyewe. Halinepi wala kutikisika.
Hatupaswi kuogopa kupita katika daraja hili. Padre ni nani katika Sakramenti
hii ya upatanisho?
Wapendwa wana wa Mungu, niwakumbushe tena nafasi ya Padre katika
Kanisa, na katika adhimisho hili la Sakramenti ya Upatanisho. Padre ufahamika
kwa kile afanyacho. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana, (Yoh
14:6). Padre ni Mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa watu
wa Mungu, “Kila Padre ni Kristo
mwingine” {“Alter Christus”}. Ni mwanadamu kama wanadamu wengine, aliyetwaliwa
kati ya watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu, “Maana kila kuhani mkuu
aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo
yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao
wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa
ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa
ajili ya dhambi,” Ebr 5:1-3. Kama Kristo mwingine hakuna mtu
anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Lakini Padre ni chumvi na mwanga
wa dunia. Kwa hiyo padre hata baada ya upadrisho wake anaendelea kuwa binadamu.
Na hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata
tama.
Kumbe si halali: Watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge
kama wao. Kuwadai mapadre kuwa na akili kama malaika. Kutaka upendo wao
unyeyushe ugumu wa kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya
maisha.
Padre ni upendo kwa Mungu: palipo na huzuni Padre huleta
furaha. Pasipo na haki Padre hutetea haki. Kwa vijana huwatia moyo na
kuwafundisha fadhila mbalimbali. Padre utii
na uaminifu kwa watu wote. Padre ni moyo wa uwajibikaji na heshima kwa
watu. Wanaoteuliwa kuwa mapadri ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa
ndugu zao. Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Padre ni
zawadi kwa Mungu ya watu kwa Mungu. Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi
hulipwa chuki na minong’ono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni
mtu anayemwakilisha Kristo. Kama Mt. Fransisko alivyosea, “kama ningekutana na
malaika pamoja na Padri, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni
rafiki wa Mungu na Padri ni Mhudumu wa Mungu.” Malaika hufuata pale Mungu
alipo, lakini Mungu ufuata pale padre alipo. Mt. Yohana Maria Viane alisema: “Acha eneo na
sehemu yoyote bila Padre kwa miaka ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu
wanyama.” Padre kwa Kanisa ni zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo.
Wakristu wenzangu, Sakramenti ya Kitubio ni upatanisho (1Yoh
4:10), uliotukuka kati ya Mungu na mwanadamu. Jamani nani kati yetu asiyependa
kupatanishwa na Mungu ikiwa yeye tu ndiye hatma ya kila kitu kwetu? Mbona
hatupendi upatanisho huu? Mbona tunafurahia ufundo wa mizoga ya dhambi zetu?
Kwa nini hatutaki uturi huu kutoka Sakramenti hii ya Upatanisho? Leo Sakramenti
hii ya Upatanisho imekuwa kama kituo cha polisi. Hatuendi kwa hiari yetu bali
kwa pingu na ni pale tu tunapokamatwa. Hii siyo taswira ya Sakramenti ya
Upatanisho. Tutafakari mfano huu wa upendo katika Sakramenti ya Upatanisho.
Mzee Mchepuko alijipeleka katika saduku la maungamo na mambo
yalikuwa kama hivi. “Habari zako Padre,” Mzee Mchepuko alianza kwa salamu hiyo.
“Milele amina mwanangu na karibu katika upatanisho na Mungu,” Padre Mapendo
alijibu kwa utulivu. Muda ulipita ukitawaliwa na ukimya. “Mbona kimya
mwanangu?” Padre Mapendo aliuliza kwa upole. “Sijui nianzeje Padre, ni muda
mrefu sijakanyaga mahali hapa,” alijibu Mzee Mchepuko kwa hofu. “Usiwe na hofu
wala woga. Anza tu kusema yote kwa moyo wa toba uliyoyatenda kinyume cha Upendo
wa Mungu,” Padre Mapendo alimjibu kwa sauti ya upole. Mzee Mchepuko akayasema
yote yaliyokuwa moyoni mwake. Padre Mapendo akamwombea na kumalizia kwa maneno
haya; “nami kwa niaba ya kanisa nakuondolea dhambi zako kwa jina la Baba na la
Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.” Yoh 20:23. Kisha Padre Mapendo akampa
malipizi ya kusali sala ya Baba Yetu. Muda ukapita ukitawaliwa na ukimya. “Mbona
kimya mwanagu,” Padre Mapendo alimuuliza kwa upole. “Sikumbuki tena sala hii
Padre,” Mzee Mchepuko alijibu kwa unyenyekevu mkubwa. “Sali sala yoyote
unayokumbuka mwanangu,” Padre Mapendo alimjibu wa utulivu. Muda tena ulipita na
baadaye ilisikika sauti, ‘ngo, ngooo, ngooooo!’ “Ndicho ninachokumbuka katika
Kanisa Padre,” Mzee Mchepuko alijibu kwa upole (akimaanisha KENGELE). “Nenda na
amani na furaha kwa kusamehewa dhambi zako,” Padre Mapendo alimalizia. “Asante
Padre,” Mzee Mchepuko kwa furaha na tabasamu alijibu.
Hitimisho
Wapendwa katika Kristo, pamoja na michepuko yetu (hali ya
dhambi) na kusahau kwetu, Mungu hubaki kuwa UPENDO, HURUMA NA MSAMAHA. Jamani
kwendeni kupatanishwa naye!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Naye
akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote
mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa,” Yoh 20:22-23
Tusali:-Ee
Yesu na yangu yote, nijalie fadhila ya unyenyekevu katika kutumia karama na
vipaji vyangu vyema na kuvishirikisha kwa wengine pasipo choyo, ili katika hayo
wewe uonekane. Amina
Tusome TAFAKARI nyingine hapa >> https://wingulamashahidi.org/2019/08/12/hata-ilipotimia-siku-ya-pentekoste/
ResponderEliminar