martes, 10 de mayo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 7 YA PASAKA

ALHAMISI WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo: Mdo 22:30, 23:6-11
Zab 16:1-2a, 5, 7-8, 9-10, 11
Injili: Yoh 17:20-26
Nukuu:
Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?” Mdo 23:3

Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako,” Mdo 23:5

“Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu,” Mdo 23:6b

Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21

Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24

Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26

TAFAKARI: “Furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, ipo “furaha kuishi katika dhamiri safi, na kupokea mateso yote kwa ajili ya Kristo.” Kuishi katika dhamira safi ni kuishi maisha yasiyo na hatia, yaani maisha yanayompendeza Mungu. Ni kuishi bila dhambi, ingawa twaweza kudondoka tena na tena katika dhambi. Tuapodondoka katika dhambi tuijongee neema na huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho. Ndugu yangu, neema na huruma ya Mungu kupitia Sakramenti hii ya Upatanisho ni kubwa kuliko dhambi zetu. Kuishi katika dhamiri safi kunatufanya kuwa tayari kwa jambo lolote wakati wote wote. Mt. Aloyce wa Zonzaga ni mfano wa mtu aliyeishi katika dhamiri safi muda wote. Wakati fulani alipokuwa anacheza mchezo fulani, mlezi wake alimjia na kumwuliza hivi, “endapo umebakia muda mfupi tu na iwe mwisho wa dunia hii ungefanyaje? “Nitaendelea kucheza mchezo huu,” Mt. Aloyce alimjibu mlezi wake bila wasiwasi. Jibu la Mt. Aloyce wa Gonzaga linaonyesha jinsi gani alivyokuwa tayari katika yote.

Mtume Paulo kwa dhamiri safi aliyokuwa nayo haogopi kuyapokea mateso yote kwa ajili ya Kristo. Paulo anapigwa na kudhalilishwa bila kulijua kosa lake. Wapo pia wengi kati yetu bila kujua makosa yao wanajikuta wakikabiliwa na mateso hata wengine wanapoteza maisha yao.

Kristo anatuombea umoja na amani, akijua ulimwenguni humu tutapatwa na matatizo mengi. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma,” Yoh 17:21. Sala hii ya Bwana wetu Yesu Kristo inaonyesha dhamiri safi aliyokuwa nayo. Dhamiri hii safi ndiyo inayomsukuma pasipo shaka kujongea mateso, na kifo kile cha msalaba.

Tunapoyapokea mateso kwa dhamiri safi tunauhakika wa kuwa pale alipo yeye, yaani, Yesu Kristo baada ya maisha haya ya hapa duniani. Uhakika huu anatupa Yesu anaposali, Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24

Wapendwa wana wa Mungu, yatupasa kuisha ndani ya pendo la Mungu nyakati zote na majira yote. Kuuishi upendo huu wa Mungu ni kutambua pia jina lake ambalo Mwana amefanya bidii zote kutufundisha. Hivyo Yesu anasema, Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26. Ndugu yangu, kuishi upendo wa Mungu na kutenda yaliyomema huijenga na kuikuza dhamiri safi ndani mwetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu,” Yoh 17:24


Tusali:-Ee Mungu Mwenyezi, uniumbie moyo safi uifanye upya roho iliyotulia ndani mwangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario