miércoles, 18 de mayo de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 7 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo: Yak 5:1-6
Zab: 49:14-15ab, 15cd, 16-17, 18, 19-20
Injili: Mk 9:40-49 
Nukuu:
 “Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho,” Yak 1:3 

Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi,” Yak 5:4 

Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo,” Yak 5:5 

 “Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41

Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini,” Mk 9:42 

 “Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto,” Mk 9:49 

TAFAKARI: “Mwanadamu hawezi kudumu katika fahari yake bila Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kama tulivyokwisha kuona kwamba maisha yetu hapa duniani ni jukumu la muda mfupi, masomo yetu ya leo yanatutaka tuyaone maisha kama dhamana. Maisha ni dhamana tukijua tunaowajibu wa kufanya kwa muda na siku tutakazokuwa hapa duniani. Ulimwengu huu ukiwa kama kiganja cha mkono, nasi wanadamu kama vidole vya mkono huo, kwa pamoja na hasa tukijali umoja katika utofauti wetu, tunao wajibu wa kupafanya mahali hapa-dunia, kuwa sehemu nzuri ya kuishi kwa kila moja, huku tukiutamani ule umilele. Hivyo, “mwanadamu hawezi kudumu katika fahari yake bila Mungu.” Dhana hii katika maisha inatukumbusha kuwa hakuna masikini asiyekuwa na kitu cha kutoa, na hakuna tajiri asiyekuwa muhitaji. Ndugu yangu, tonge la ugali upata umbo lake zuri la mviringo kwa sababu vidole vyote vitano vya mkono vimeshiriki katika uumbaji huo vikijali umoja katika utofauti wao.

Jamii isiyojali umoja katika utofauti ili wote kwa pamoja walifikie lile lengo na haki ya kuishi bila kubughudhiwa, hakika jamii hiyo kudongoka katika machafuko ni swala la kufikia tu. Maisha ya mtindo huo hayawezi kamwe yakaepuka hofu, yaani kwa matajiri kwa utajiri wao, na masikini kwa umasikini wao. Hali ya unyonyaji na kutokuwa na fursa sawa kwa wote, ni tatizo kuwa sana leo katika jamii yetu. Mazingira na hali kama hii ndiyo anayoikemea leo Yakobo Mtume na kusema, Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia,” Yak 5:1. Ni wazi kwa mashaka haya wenyenazo-matajiri, huanza kwanza kujenga wigo katika eneo la ujenzi kabla ujenzi wenyewe. Na hata baada ya ujenzi kukamilika, wigo huo uzungushiwa nyaya za umeme na makaripio mengi. Hii yote ni hofu na dalili za kutokuwa na usawa na fursa kwa wote katika jamii tunayoishi leo. Mwisho wa siku Mtume Yakobo anaonya juu ya tabaka hili lisilojali kwa kujilimbikizia mali. Naye anasema, Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo,” Yak 1:2. Leo kati yetu wapo watu wanaosali kila kukicha Mungu awape maisha marefu ili waendelee kuvitumbua na kuvitafuna walivyojikusanyia hata kwa njia zisizo halali. Vile vile kati yetu wapo, tena walio wengi wanaosali kila siku Mungu awapunguzie ugumu wa maisha. Hawa ni wale wasio na uhakika wa mlo wa asubuhi na mchana, na jioni pale tu wakibahatika.

Wapendwa wana wa Mungu, aliyenacho tena cha ziada na kuona jirani yake akitaabika bila kumnyooshea mkono wa heri, ajue anajikolezea jehenam angali hapa hapa duniani. Hakika, dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho,” Yak 1:3. Pasipo shaka, siku ya mwisho ya tabaka hili ni mateso yasiyo kifani. Kuepuka kadhaa na mateso hayo, Yesu anatuasa, Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41. Embu tazama maisha ya wakulima yalivyo ya taabu na gharama kubwa katika uzalishaji! Embu tazama wanavyonyongwa katika bei za mazoa yao! Tazama kelele za wakulima hao zinavyopotea hewani bila kusikilizwa! Ndugu zangu na wote wale msiowasikia kelele za wakulima hawa, na ninyi wenye mamlaka,  angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi,” Yak 5:4. Ni Mungu huyu aliyetajiri kwa kumwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14, sote katika utofauti wetu kwa vile ndivyo inavyompendeza kutuumba, Mwa 1:27, na kuufunua utukufu wake, katufanya sote matajiri.  Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Je mimi niliye Mkristo na tajiri-katika mali, najua ukweli huu na kuwajibika kadiri na uwezo na utajiri aliyonipatia Mungu?

Leo kuishi maisha ya anasa ndiyo fahari na kujulikana na wengi toka Misikitini, Makanisani, na Serikalini. Saratani hii imeingia hata katika siasa zetu na hatma ya uongozi. Uongozi umekuwa wa kuhudumiwa na siyo kuhudumu. Kila mmoja nataka kuwa mkubwa. Hali na mtazamo huu kijamii ubinya kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki kwa wote, na mbaya zaidi kwa wale wasionacho. Hii ni kwa sababu kama asemavyo Yakobo Mtume,  mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo,” Yak 5:5. Kwa mtindo huu, duara la umasikini linaendelea kutanuka na kuwa kubwa zaidi, huku watu wachache wakijineemesha jasho la walio wengi. Mnyonge hana pa kushika kwa sababu kote kuna kaa la moto. Wale wachache wanaojitokeza na kukemea unyonyaji huu uliokidhiri wanachukuliwa kama waalifu wa kivita na kufichwa kusikojulikana na hata kupoteza uhai wao. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi,” Yak 5:6. Ndugu yangu, kama tujuavyo maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda mfupi, na kwa upande mwingine kuwa ni dhamana, basi tujue hata mahangaiko haya ya wengi wanyonge ni ya muda tu. Jambo la muhimu la kuondokana na hali hii ni kila mmoja kujali na kuwajibika kwa nafasi yake, na kuuchukia uovu kwa nguvu zake zote.

Wapendwa wana wa Mungu, tutende haki kwa usawa tukimwogopa Mungu. La sivyo tuwe tayari kwa haya ayasemayo Kristo Yesu juu ya wadogo na wanyonge katika jamii.Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini,” Mk 9:42. Kufungwa jiwe na kutupwa baharí kulimaanisha kupotea kabisa na kutokuonekana machoni mwa watu. Tunajua mwili uliozama kwenye maji baada ya muda huelea. Hivyo kwa kufungiwa jiwe na kutupwa baharini hakuna tena uwezekana wa kuelea juu. Basi ni vyema tukavichambua kwa makini viashiria (vilema) vyote vile vinavyotuweka mbali na upendo wa Mungu na watu wake. Naye Yesu katika hili anatushauri kwamba,  Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki,” Mk 9:43-44. Baadhi yetu tumekuwa watu wa kujilimbikizia mali tu kila kukicha hata kama hatuzihitaji. Basi ni vyema ukautazama vizuri mkono wako na kupunguza kasi hiyo ya kujilimbikizia mali na nyingi zikiwa za dhuluma.

Wapo pia kati yetu kazi yao ni kuvuruka utarajibu wa kweli na haki uliopo ili wengi wakose na wachache akiwemo na yeye wafaidike na kuneemeka. Hivyo mienendo hiyo siyo sahihi na wala haimpendezi Mungu. Hii ni kama miguu. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki,” Mk 9:46. Basi tutazame mienendo yetu na kujali zaidi faida ya wengi. Jicho likiwa mfano wa ufahamu wetu katika kuona, kuchambua (mema na mabaya), na kufanya kwa weledi, ufahamu huu wapaswa kujali uzalendo wa kweli katika vita dhidi ya uovu kwenye jamii yetu leo. Hivyo, Yesu anatushauri pia, Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki,” Mk 9:47-48. Ni jambo la kusikitisha sana tunapoona mtu msomi na aliyejaliwa ufahamu wa kutosha wa mambo mengi anakuwa ndiye kichokoo cha kwanza cha maovu katika jamii. Ndugu yangu, elewa umepewa dhamana kubwa sana mbele ya watu wa Mungu na Taifa yako.

Wapendwa wana wa Mungu, Nabii Isaya anasema maneno haya mazito kwa kila mmoja wetu, “wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?” Isa 33:14. Mungu mwenye haki na mwenye kutuhesabia haki atampa kila mmoja kadiri ya matendo yake pale tunapotimiza wajibu na sababu ya kuumbwa kwetu. Hii ndiyo ‘chumvi ya moto’ anayoisema Yesu, akiimaanisha kwamba tusipo vishinda vilema vyetu vyenye kutupeleka katika kutenda dhambi, basi tuwe na uhakika wa mateso yasiyo na mwisho. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto,” Mk 9:49. Ndugu yangu, maisha ni dhamana.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41


Tusali:-Ee Yesu, niwezeshe kila siku kuvishinda vilema vyangu, na niwe tayari kuyafanya mapenzi yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario