martes, 10 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 7 YA PASAKA

JUMATANO WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo: Mdo 20:28-38
Zab: 68:29-30, 33-35a, 35bc-36ab
Injili: Yoh 17:11b-19
Nukuu:
Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe,” Mdo 20:28

Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa,” Mdo 20:32

Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami,” Mdo 20:33-34

Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea,” Mdo 20:35

Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo,” Yoh 17:11b

Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu,” Yoh 17:14

Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu,” Yoh 17:15

Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh 17:19

TAFAKARI: “Kujitoa kuliko kweli katika utume wetu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tulitafakari neno hili, “kujitoa kuliko kwa kweli katika utume wetu.” Mara nyingi tumesikia na hata kusoma sehemu mbalimbali kwamba, uongozi katika Kanisa ni utumishi. Bila shaka msingi huu unatoka kwa Kristo mwenyewe aliyejitoa bila kujibakiza. Kama kweli tu wafuasi wake hatunabudi kufuata nyayo zake kisawasawa. Kwa maana hiyo Kiongozi ni kutumika kwa ajili ya wale waliokupa dhamana uwaongoze, au uliopewa dhamana hiyo na Mamlaka husuka kuongoza. Naye Yesu anaseme, “mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Namna hii ya kujitoa haitazami maslahi binafsi. Utumishi wa aina hii siyo ajira.

Ni kwa mtazamo huu tunamwona Mtume Paulo akiwa Mileto anawaaga wazee wa Efeso kwa kutambua kazi yake na wito wake kwao. Huku ndiko kujitoa bila kujibakiza katika utume. Mtume Paulo anatoa wosia wake na kusema, jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha Kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe,” Mdo 20:28. Kadiri ya uzoefu na mang’amuzi ya kichungaji, mara nyingi tunapoondoka sehemu zile tulizotumika vyema, mwovu shetani huzinyemelea na kuziharibu. Hivyo ni vyema kuaga vyema na kutoa msisitizo maeneo yale ambayo yapaswa kulindwa kama mboni ya jicho. Tumenunuliwa kwa damu ya Yesu, hivyo tuilinde Imani yetu vizuri. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, analotuambia Mtume Paulo leo ndilo analotukumbusha Mtume Petro, yaani,  thamani ya Ukristo wetu na Imani hiyo ndani na katika Kristo Yesu, kwamba, Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Ndugu yangu, shikilia vyema utume wako. Hapo ndipo utakapokutana na Kristo.

Wapendwa pamoja na kutoa angalisho hili, ili tuendelee kuzichota neema kwa kazi yetu iliyotukuka kiutume, tusisahau kuunganika katika sala. Tusiache kukesha katika sala na kuyakabidhi yote mikoni mwa Mungu. Mtume Paulo anatambu umuhimu wa sala na kuyaweka yote mikono mwa Mungu. Yote tuyafanyayo yataendelea na kudumu tukiyaweka mikoni mwa Mungu. Hivyo, Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa,” Mdo 20:32. Kuyaweka yote mikoni mwa Mungu ni kutambua nafasi yetu kama binadamu, na nafasi ya Mungu ambaye ndiye mwezeshaji wa yote. Mtume Paulo anatambua jambo hili anaposema, “Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye,” 1Kor 3:5-7. Ufahamu huu ni muhimu sana katika utume wetu. Ndugu yangu usipojua kweli hii, na ukaona yote yawezekana kwa ufahamu na nguvu zako tu, hakika utume huo hautakuwa na matokeo mazuri. Shetani atakuinua mpaka kileleni na kukubwaga hadi chini bila huruma. Mradi wa mtindo huu ni kama ule Yesu aliyotuambia wa mtu yule aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. Naye anasema, “mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt 7:27. Huyu ni mtu yule asikiaye maneno ya Yesu asiyafanye. Mtu huyu ufananishwa na mpumbavu anayejiamini kwa nguvu zake mwenyewe na ufahamu wake. Hiki ndicho atuambiacho Mzaburi, “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wanafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1

Wapendwa wana wa Mungu, kuna hatari kubwa pale tunapojifananisha na matunda ya kazi zile tunazofanya na kutotambua tumeyafanya hayo yote kwa kuwezeshwa na Mungu. Hakuna sababu yoyote ya kujifananisha na kile ulichokifanya. Ukiona watu wanakusifia kuliko kweli, basi elewa umetumika vyema na Mungu. Hivyo sifa na shukrani zirudisha kwa Mungu. Kwa kufanya hivi, ni kutambua ubinadamu wako, na uwepo wa Mungu kwa kile ulichokifanya. Hapa ndipo tunapoomba tena kwa tendo hili la kushukuru. Mtume Paulo anafahamu ukweli huu anapotoa mapato na matumizi ya mahitaji yake ya kila siku mbele ya wale aliowatumikia kwa kusema, Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami,” Mdo 20:33-34. Katika utume wetu, yatupasa kutokuwa mizigo kwa watu. Jaribu kila siku kuwa mbunifu wa mambo yenye kujenga maisha ya watu na Imani dhabiti juu ya Mungu wanayemwamini. Huku ndiko kulenga juu alipo Kristo. “Basi mkiwa mmefufukiwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Kama hayo tuyafanyayo na kuyatafuta katika utume wetu hayalengi pale Kristo alipo basi tunapoteza Muda bure.

Wapendwa katika Kristo, yote tuyafanyayo yawalenge hasa wanyonge na wasiokuwa na fursa katika jamii tunayoishi. Huyu ndiye Kristo anayeteseka katikati yetu muda wote. Mtume Paulo anasema, katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea,” Mdo 20:35. Huu ndiyo umoja na mshikamano anaotutaka Kristo tuuishi na kila mmoja wetu bila kujali historia yake, familia yake, nafasi yake katika jamii, ukoo wake, kabila lake, na hata utaifa wake. Umoja huu na mshikamano katika Imani ndiyo aliotuombea Kristo kabla ya kifo, mateso, na kufufuka kwake. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo,” Yoh 17:11b. Umoja huu anaotuombea Kristo ni umoja wa Utatu Mtakatifu na usiogawanyika, yaani: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Tendo hili na hali hii tunapoiishi ndiyo furaha ya Mungu, na chukizo kwa yule Mwovu Shetani. Hivyo kwa namna nyingine yatupasa kuwa imara sana katika Imani. Ulimwengu utatuchukia kwa umoja wetu. Ulimwengu utatuchukia kwa sababu uraia wetu si wa hapa duniani, bali mbinguni. Hivyo Kristo analijua jambo hili na anatuombea katika sala hii maalum, Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu,” Yoh 17:14. Tumeumbwa ili tuishi milele. Mateso tutakayokutana nayo katika ulimwengu huu ni njia mojawapo ya utakaso wetu tukiuchuchumilia utakatifu huku tukiishi kwa uaminifu wote licha ya mahangaiko na majaribu. Hivyo Kristo hatuombei sisi kuondolewa katika ulimwengu huu, bali tuushinde na kujinyakulia taji la uzima wa milele. Tunaweza jambo hili tukiwa ndani na katika Yesu Kristo kwa sababu Kristo kesho tuombea kwa Baba yake atulinde na yule mwovu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu,” Yoh 17:15. Hakuna sababu ya kujiona kutengwa na Mungu wakati wa shida na dhiki kubwa. Tunaye mpiganaji wetu na Jemedari wetu aliyeyashinda yote, yaani, Yesu Kristo. Tushikamane naye hadi mwisho.

Wapendwa wana wa Mungu, vita hii dhidi ya mwovu shetani na uovu katika jumla wake tutaishinda tu tukiwa na Kristo kwa sababu amejiweka wakfu kwa ajili yetu. Kristo amejitenga na kufanya kazi hiyo tu ya kutukomboa kwa upendo wake wote. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh 17:19. Nasi tutatakaswa katika kweli. Utakataso huu katika kweli ni kuwa waaminifu katika ufuasi wetu kila siku tunapojitoa na kutumika bila kujibakiza kwa mpango wake Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh 17:19


Tusali:-Ee Yesu shujaa na Jemedari wetu, kwa mfano wa maisha yake, tuwezeshe nasi kujitoa bila kujibakiza katika utume wetu kila mmoja kadiri ya wito wake. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario