lunes, 30 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 9 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Tim 1:1-3, 6-12
Zab: 123:1b-2ab, 2cdef
Injili: Mk 12:18-27
Nukuu:
Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3

Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9

 “Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao,” Mk 12:18-19

Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni,” Mk 12:25 

TAFAKARI: “Kuna furaha ya kweli na heshima kuifia ‘kweli na haki’ kwa wajinga ili waijue kweli na haki, kuliko kufa kama mfalme kwa pongezi na makofi ya wapumbavu wadhanio kuijua ‘kweli na haki ilhali hawaijui na wao wenyewe hawajijui.’”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kuwa Mkristo kwa kubatizwa tu haitoshi. Leo kuwa Mkristo kwakuitaji kuwa mpiganaji halisi wa Kristo kama Mfalme wa haki, kweli, upendo, unyenyekevu, huruma, msamaha, na uwazi. Ulimwengu uliojaa dhuluma, ufisadi, na matendo ya uvunjifu wa haki za binadamu, hauwezi kamwe kuukubali Ufalme wa Yesu Kristo kama nilivyosema. Leo tulio wengi, yaani Wakristo, tumewekwa katika kikaangio cha kukubaliana na mtazamo huo (dhuluma, ufisadi, na uvunjifu wa haki za binadamu) au kuukataa kwa gharama kubwa sana hata kuutoa uhai wako. Hakika njia iliyo rahisi na isiyo na mawaa ni kuusaliti Ukristo (kumkana Kristo) wako kwa gharama nafuu kama alivyofanya Yuda Eskariote kwa vipande thelathini vya fedha. Ndiyo maana leo wale tuliotegemea waseme na kuukemea uovu wapo kimya, na wale waliojaliwa ufahamu wa kupembua mema na mabaya wamekuwa wasaliti wa iliyo kweli na haki.

Ndugu yangu unayesafari nami katika tafakari hii, kuwa Mkristo leo ni changamoto kubwa sana, kama ilivyokuwa kwake Yesu Kristo kuutangaza Ufalme wa  Mungu kwa Wayahudi kwa kauli mbiu yake ile, yaani,  “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Jamii ya Yesu wakati ule ilikuwa kama ndoto kuupokea ujumbe huu-kutubu na kuiamini Injili. Je, katika hali hii, Yesu alirudi nyuma katika hili kwa vigezo vya kutokukubalika? La hasha!

Kwa kuushindilia msumari wa moto katika kusisitiza na kumaanisha asemacho, Yesu aliwapa wapinzani wake silabasi ya utendaji wake kwa miaka ile mitatu. Naye anasema juu ya utendaji wake kama ifuatavyo na itakavyokuwa: Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Silabasi hii ndiyo iliyokuwa hatma ya kifo chake kila cha aibu, yaani, kifo cha Msalaba. Msukumo wa kifo hiki ni Upendo na furaha ya kweli katika haki, kwa kujua kile akifiacho siyo kitu cha kubumba bali ndio ukweli wenyewe. Yesu anakuwambia wewe na mimi,  Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Bwana wetu Yesu Kristo amelifanya hili, nasi kama wafuasi wake ni changamoto kubwa kwetu leo. Hakika Kristo amekupenda wewe na mimi upeo, na kwa sababu hiyo alikuwa tayari na yupo tayari hadi sasa kufa kwa ajili yako na mimi. Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Kwa nini basi Mkristo mwenzangu unakuwa na imani ya mwono wa chura? Hivi leo nikikuuliza uniambia ukweli kuhusu Chura ‘kama amesimama au kachuchumaa waweze nipa jibu sahihi? Kigugumizi hiki cha kujua mkao wa Chura, ndicho kigugumizi juu ya imani ya Wakristo wengi wa leo.

Wapendwa wana wa Mungu, yote niliyoyasema ni kukuandaa ili uzame vizuri katika tafakari ya leo na kadiri ya masomo yake. Mtume Paulo licha ya changamoto alizozikuta baada ya kuongoka kwake, hakuwa tayari kubadilishwa na mtazamo wa wakati wake na kujivika koti la uovu. Haki na kweli ndani na katika Kristo Yesu ilibaki kuwa msingi wa imani yake. Hivyo Barua yake ya pili kwa Timotheo anapenda wafahamu, na tufahamu kiini na msimamo wa imani yake. Naye anasema, Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana,” 2Tim 1:3. Anaye kumbukwa hapa bila shaka ni Timotheo mwenyewe aliye mfano halisi wa kweli na haki katika jumuiya yake. Leo mambo hayako hivyo hata kidogo. Baadhi yetu kama viongozi wa dini, na wenye kuijua iliyo kweli, na hata kama hatuiamini kwa kupitia utaratibu uliowekwa kwa taasisi husika kama hatua ya kuhesabiwa haki ya kuwa kile ulicho, tumekuwa waogeleaji wa kufuata mawimbi ya maji bila kujali ustadi wa kuogelea kwetu tukitazama ng’ambo ile na iliyo salama tunayotamani wote kuifikia. Hapa ndipo penye chimbuko la unafiki. Hapa ndipo kwa makusudi makubwa kabisa katika fikiri, amua na tenda yetu, wafuasi wetu hutushangaa kwa kwenda kinyume kabisa cha matazamio ya kweli ile tunayoihubiri na matamanio yake. Hapa ndipo tunapoonekana si tu vituko, bali watu tusiokuwa na maono na uelewa wa kile tukisemacho, na mwisho kuutabiri unabii tusioujua ili tuenende na mawimbi ya nyakati zetu tusiyoyajua.

Mkristo mwenzangu, niyasemayo siyo mageni mbele ya macho yako. Manabii hawa wa kubumba hawaoni shaka wala haya hata kidogo leo kusema Edgar ndiye “chaguo lile la Mungu” leo kwa watu wa Mungu. Je, kwa nini wanasema kama wasemavyo? Je, wanajua kile walicho na yale waliyoyalia kiapo kwa ajili ya taifa la Mungu? Kwa nini basi wanadanganyika kiasi hicho? Je, wanaifahamu karama ya Mungu ndani ya maisha na utume wao? Mtume Paulo anamwambia Timotheo hivi, Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu,” 2Tim 1:6. Kutokuchoka maana yake, usitafute urahisi wa jambo na kuutafsiri vinginevyo na karama uliyonayo kwa kuyaona mawimbi ya muda tu katika wakati wako. Kwa maana nyingine, palipo na giza tusema giza, na tufanye kadiri iwezekanapo kuuleta mwanga, na palipo mwanga tusema mwanga na uutetee mwanga huo ili udumu. Kwa nin basi katika hali hii twaingiwa na woga? Kwa  nini tunakufa gazi pasipo ganzi?Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7. Katika mazingira ya utata kama huu tufanye nini?

Wapendwa wana wa Mungu, katika mazingira na utata kama huo yatupasa kusimama katika kweli, hata  kama nikibaki mwenyewe. Yesu Kristo kwa kutambua ugumu huu anakuambia wewe na mimi leo kwamba, tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yoh 8:32, 36. Mwana anatuweka huru, unapokuwa tayari kujiachia katika minyororo ya upumbavu kwa kuwa tayari kujifunza na kumsikiliza. Hii ndiyo habari njema ya wokovu, yaani, kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa shuhuda ya neno hilo kwa maisha yako ya kila siku. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,” 2Tim 1:8-9. Je, hili lasema lolote juu ya maisha yako kama Mkristo leo?

Leo mimi kama mfuasi wa Kristo na muhudumu wake wa karibu, habari njema ya wokovu, yapaswa kuwa kipaua mbele changu. Na habari njema ya wokovu kwa ufupi kabisa ni kulishinda giza (dhambi) kwa kuukumbatia mwanga (utakatifu). Kwa habari hii njema ya wokovu, inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu,” 2Tim 1:10-11. Leo mimi kama mfuasi wa Kristo, na kwa upekee kama mhudumu wa karibu (Mkleri), bila kuijua habari njema, na kusoma alama za nyakati kadiri ya habari njema ile, ufuasi wangu na ukaribu wangu hautakuwa na mguso wowote kati ya kile nilicho na ushuhuda ule nipasao kuutoa. Nitabaki kuwa tukio kama utaratibu wa kawaida bila historia kama sehemu ya mang’amuzi. Ndugu yangu, unakuwa historia kama sehemu ya mang’amuzi unapoyachukulia yale yaliyotokea katika maisha yako, ukitazama kule unapokutamani kama hitimisho la kila kitu. Hapa tumaini lipo hata kama linachelewa au kucheleweshwa. Hapa ndipo mateso kama matukio katika maisha ya kila siku yanapata maana kama asemavyo Mtume Paulo, kwamba, Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12. Hapa siku ‘ile’ ya maanisha ‘uzima ule wa milele’ tunao utamani.

Ndugu yangu, kutokuyaona maisha katika mtazamo huu wa umilele, ni tatizo kubwa sana leo, na hasa katika jamii yetu ya Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa tunaishi katika ulimwengu wa kufikirika na usiowezekana. Leo wengi tumeaminishwa uongo, na tumeupokea uongo huo kuwa ndiyo kweli. Hili ndilo analojaribu kulibadili Yesu katika akili za watu kwa nyakati zake zile na mazingira yake, na hasa kuhusa swala la kiyama. Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao,” Mk 12:18-19. Yesu Kristo haoni haya kusema lililo kweli na haki hata kama jambo hili limeaminika kuwa kweli ilhali kweli haipo ndani yake. Kristo anatutaka tutofautishe maisha tunayoishi leo na sasa, na maisha yale tutakayoishi mara baada ya kifo chetu.  Maisha ya ufufuko, yaani, maisha baada ya kifo, ni tofauti kabisa, kwa sababu tutakuwa na miili tofauti na hitaji tofauti. Miili tutakayokuwa nayo ni miili iliyotakatifuzwa,’ na isiyo shikiliwa au zuiliwa na ‘muda na nafasi.’ Ni miili iliyo huru kwa kila jambo na katika kweli na haki, na yote katika utukufu wa Mungu.

Na kwa namna hiyo Yesu anasema, watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni,” Mk 12:25. Tunaoa au kuolewa kwa sababu tupo chini ya shikamanizi la muda na nafasi. Ndugu yangu, katika egesho au kipimo muda na nafasi, hatuna chaguzi nyingine zaidi ya kile kilichopo katika kipimo hicho. Kumbe maisha ya ufufuko ni tofauti kabisa. Katika kweli hii Yesu anatutaka tujue hili, kwamba,  kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?” Mk 12:26. Huyu Mungu kwa lugha nyepesi ni Mungu aliye hai, na hai kwa kila kitu. Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana,” Mk 12:27. Tunapotea pale tunapomwona Mungu kama mfu kadiri ya ubinadamu wetu. Mungu wetu ni mwanzo na mwisho, Alfa na Omega, Ufu 22:13.

Tumsifu Yesu Kristo! 

Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahayari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile,” 2Tim 1:12


Tusali:-Ee Yesu, nijalie niwe kielelezo chako halisi popote pale nitakapokuwa, na iwe sehemu ya ushuhuda wangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario