JUMATATU
WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo: Mdo 19:1-8
Zab: 68:2-3ab, 4-5acd,
6-7ab
Injili: Yoh 16:29-33
Nukuu:
“Paulo
akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye
atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu,” Mdo 19:4
“Na
Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao;
wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo 19:6
“Basi
wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo
yote,” Yoh 16:29
“Tazama,
saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na
kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo
pamoja nami,” Yoh 16:32
“Hayo
nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini
jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33
TAFAKARI:
“Kuongozwa na Roho Mtakatifu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Roho Mtakatifu hakuwahi kuliacha Kanisa lake tangu zama hizo. Roho Mtakatifu
amekuwa kielelezo cha yale yote tuyafanyayo kuliendeleza na kulijenga Kanisa la
Kristo pale ambapo Kristo hajajulikana. Roho Mtakatifu amekuwa muhimili mahiri
kabisa kuliongoza na kulitakasa Kanisa nyakati za matatizo na migogoro
iliyoibuka kwa sababu mbalimbali katika historia ya Kanisa. Roho Mtakatifu
aliwaongoza vyema Mitume, Mababa wa Kanisa, na katika shughuli za kimisionari,
maamuzi mbalimbali na mafundisho sahihi yaliyokuwa yakifanyika katika mitaguso
mbalimbali katika historia ya Kanisa.
Leo kwa namna ya pekee
tunasukumwa na neno hili katika tafakari yetu; “kuongozwa na Roho Mtakatifu.”
Kuongozwa na Roho Mtakatifu ni kuomba mapaji yake saba ambayo kwayo kwa
kuyaishi ni utimilifu wa yale aliyokusudia Mungu kwetu, na ukamilifu wa yale
tunayoyatamani katika uzima wa milele. Mapaji hayo ni kama ifuatavyo; Hekima,
Akili, Ushauri, Nguvu Elimu, Ibada na Uchaji. Mapaji haya yote yanalenga
kumfahamu Mungu, na kuishi katika kweli yake. Tukimfahamu Mungu na kuishi
katika kweli yake, maisha yetu hapa duniani yanapata malengo yake halisi, yaani
kuelekea uzima wa milele.
Ni kwa sababu hii,
Mtume Paulo anawauliza Waefeso, kama walipokea Roho Mtakatifu walipoamini, na
walibatizwa ubatizo gani. Maswali haya mawili yana maana sana. Kama tunaimani
bila kumpokea Roho Mtakatifu tunaupungufu wa mapaji yake ambayo ndiyo kielelezo
sahihi cha kumjua Mungu na kuishi katika kweli yake. Kwa maana hiyo, kama hili
halipo, basi hata malengo ya maisha yetu hapa duniani yanakosa mwelekeo sahihi.
Jibu la Waefeso ni kwamba hawajawahi kusikia kuhusu Roho Mtakatifu, na ubatizo
walioupata ulikuwa wa Yohane Mbatizaji.
Mtume Paulo anatoa
ufafanuzi wa ubatizo huo wa Yohane kwa kusema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa
toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu,” Mdo
19:4. Ubatizo huu ulikuwa maandalizi ya kumtambulisha na kumwamini yule atakaye
kuja baada ya Yohane, ambaye ni Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye ufunuo halisi wa
Mungu Baba, na kwa maana hiyo, Yesu anasema, “Na
yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika
yaliyo yangu, na kuwapasheni habari,” Yoh 16:15. Jambo hili ndilo analojaribu
kulisema Yohane, kwamba ukamilifu wa tendo analolifanya yaani ubatizo huo wa
toba litakamilishwa na Yesu Mwenyewe.
Mtume Paulo
analikamilisha lile lililokamilishwa na Kristo kwa Sakramenti hii ya Ubatizo
kwa kuwawekea mikono juu yao. Hivyo, “alipokwisha kuweka mikono yake juu yao,
Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo
19:6. Tunaona baada ya Roho Mtakatifu kuwa ndani yao, mapaji yake yanajionyesha
mara kwa kuanza kunena kwa lugha na kutabiri. Haya ni matunda ya Roho Mtakatifu
kwa wale aliowaridhia.
Ni ukweli usio shaka
kwamba Mitume hawakufahamu ukweli aliokuwa akiuongelea Yesu alipokuwa akisema
‘Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi
mtaniona,’Yoh 16:16. Kwa sasa Mitume
wanaufahamu ukweli aliokuwa akiusema Yesu. “Basi
wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo
yote,” Yoh 16:29. Roho huyu Mtakatifu ndiye atakayetufunulia yale tusiyojajua. “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo
mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi
si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami,” Yoh 16:32. Roho Mtakatifu ndiye
mfariji wetu, kwani Kristo kesha ushinda ulimwengu. Ulimwengu huu tutapata
matatizo ila Roho Mtakatifu atatufunulia yale yaliyojificha. “Hayo
nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini
jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33. Wapendwa, tumwombe Roho
Mtakatifu na kutushushia mapaji yake saba ili tuzaliwe upya ndani yake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na
Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza
kunena kwa lugha, na kutabiri,” Mdo 19:6
Tusali:-
Ee Roho Mtakatifku, utushushie mapaji yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario