JUMANNE
WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo:
1Pet 1:10-16
Zab:
98:1, 2-3ab, 3cd-4
Injili:
Mk 10:28-31
Nukuu:
“Kwa
hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu
ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo,” 1Pet 1:13
“kwa maana imeandikwa,
Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu,” 1Pet 1:16
“Hakuna mtu aliyeacha
nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au
mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa
wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na
mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk
10:29-30
“Lakini
wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk
10:31.
TAFAKARI:
“Kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika
mwenendo wenu wote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na ukweli kwamba tupo hapa duniani kwa muda mfupi, je, inatosha
kuridhika na hali hiyo na kutokufanya chochote? La hasha! Uchache wa muda wetu
hapa duniani unasema zaidi kuhusu thamani ya maisha yetu, na kila mmoja kadiri
ya wito wake. Kumbe licha ya mahali hapa-duniani kuwa ni sehemu pekee ya
maandalizi ya maisha yale ya umilele, muonekano huo unatukumbusha kwamba maisha
ni dhamana. Maisha ni dhamana tukiutazama ‘Utakatifu’ ambao ndio kikomo cha
zawadi hii ya uhai tuliopewa na Mungu. Furaha ya Mungu ni sisi kuwa Watakatifu
kama Yeye alivyo Mtakatifu, “kwa maana imeandikwa, Mtakuwa
watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu,” 1Pet 1:16. Hivyo tungali tunaishi leo na
sasa na katika uchache wa miaka yetu hapa duniani, tuelewe maisha ni dhamana
tukiutazama ule utakatifu na umilele wa maisha mara baada ya maisha ya hapa
duniani.
Utakatifu tunaoutamani
unatukumbusha na kutuwajibisha kupungua kila siku ili Kristo aongezeke katika
maisha yetu bila kupoteza au kusahau kile ulichoitwa kufanya hapa duniani
katika uchache wa miaka hiyo. “Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia
zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa
katika ufunuo wake Yesu Kristo,” 1Pet 1:13. Utakatifu huu tunaoutamani
unatutaka na kutuwajibisha kuvishinda vilema vyetu kila siku kwa kulenga
ukamilifu. Licha ya udhaifu tulionao kama wanadamu kamwe tusijifananishe na
udhaifu huo kwa sababu Mungu kwa kutuumba kwa sura na mfano wake anatuwazia
mambo makubwa kila siku. Na kwa sababu hiyo, “Kama watoto wa kutii
msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu,” 1Pet 1:14. Mungu
hakutuumba na kutuacha tujiendee wenyewe kama mwendo wa saa ya mshale. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana,
ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za
mwisho,” Yer 29:11. Tumaini hilo la siku za mwisho ni hili: “kama
yeye aliyewaita alivyo Mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo
wenu wote,” 1Pet 1:15, ili tuweze kuurithi uzima wa milele. Hakuna maisha ya
umilele pasipo ‘Utakatifu’ kwa sababu alipo Mungu Mtakatifu katika makao yake
ndipo ulipo Utakatifu kwa sababu yeye ni Mtakatifu. Je, utawezaje kuwa na Mungu
Mtakatifu katika makao yake bila wewe kuwa Mtakatifu?
Wapendwa wana wa Mungu,
safari ya kuelekea taji lile la ‘utakatifu’ inatutaka sadaka iliyo hai na yenye
kumpendeza Mungu. “Basi, ndugu zangu,
nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai,
takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana,” Rum 12:1. Sadaka
hii kama sehemu ya maisha yako kila siku itoe pasipo manung’uniko, marejesho,
na wala malinganisho. Sadaka yako iwe ya thamani na ya pekee kwa Mungu kama
shukrani kwa sadaka ile ya Yesu Kristo pale Msalabani yenye thamani kubwa
kupita sadaka zote. Hakika niutazamapo Msalaba na kuutafakari nagundua
nimekombolewa na kununuliwa kwa thamani kubwa sana! “Wala ninyi si mali yenu
wenyewe; maana mlinunuliwa kwa
thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu,” 1Kor 6:19b-20.
Bwana wetu Yesu Kristo
anakutaka wewe na mimi tusifanye marejesho, au malinganisho, na wala
manung’uniko utoapo sadaka ya maisha yako kwake na kwa Injili, yaani, Habari
Njema ya Wokovu wetu. “Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu
wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili
ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu
wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu
ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Yesu Kristo kama alivyomwondolea mashaka
Petro ndivyo hivyo hivyo anavyokuondolea mashaka wewe na mimi tutoapo sadaka ya
maisha yetu kwa ajili yake na Injili. Hivyo licha ya kuyapata haya ya leo na sasa kadiri ya hitaji
letu, tuna hakika ya uzima wa milele
ndani na katika Kristo.
Ndugu yangu, kujitoa sadaka ya
maisha yako kwa ajili ya Kristo na Injili kwahitaji fadhila ya unyenyekevu.
Hapa ndipo kwenye kushushwa na Kristo pale unapojipandisha mwenyewe na pasipo
haki, na kupandishwa na Kristo pale unapojishusha kwa kumpa nafasi Kristo ndani
ya maisha yako. Kwa maana hiyo, “wengi
walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31. Hii ndiyo changamoto kubwa katika
maisha yetu ya kiroho.
Ukimruhusu Yesu Kristo ndani ya maisha
yako uwe tayari kuyapokea yote kama alivyoyapokea Kristo hadi kuwambwa pale
Msalabani. Utatemewa mate, utachekwa, watakushangaa, utakejeliwa, utazushiwa,
utashangiliwa, utaonewa huruma, na mwisho utawambwa kama utimilifu wa sadaka ya
maisha yako kwa Kristo na Injili. Haya ndiyo maisha ya utauwa. “Naam, na wote wapendao
kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa,” 2Tim 3:12. Kwa maana
nyingine hii ndiyo heri ile ya kuishi umasikini wa roho, Mt 5:3, kwa kumpa Yesu
Kristo nafasi ndani ya maisha yako, na mwisho wa siku kuupata Ufalme wa
Mbinguni. Ni kama asemavyo Mtume Paulo kwamba, “Kama katika maisha haya tu
tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote,” 1Kor 15:19. Ni
umasikini kwa kupungua ili Kristo Yesu apate nafasi ndani ya maisha yako, nawe
uwe na furaha isiyo na kipimo. “Basi ninyi
hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na
furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Wapendwa nani kama Yesu Kristo?
Hakuna!
TumsifuYesu Kristo!
“Lakini
wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk
10:31.
Tusali:-Ee
Yesu Mwana wa Mungu uliye hai, nifundishe kutii hata pale penye shaka katika
kutii, kama ulivyotii Wewe pasipo shaka hadi mwisho kwa kutukomboa sisi na
ulimwengu nzima. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario