jueves, 19 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 7 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo: Yak 5:13-20
Zab: 140:1-2, 8
Injili: Mk 10:13-16
Nukuu:
 “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii,” Yak 5:16 

Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi,” Yak 5:19-20

 “Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14 

Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” Mk 10:15 

TAFAKARI: “Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo ni kujiachia pasipo shaka kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai katika hali ya unyenyekevu, Imani, na Upendo. Ni kuungana na Kristo na kushiriki neema zake kama watoto wadogo kwa wazazi, walezi, au walimu wao. Ni kuipokea Habari njema ya wokovu na mafumbo yake yote. Ni kuambatana na Kristo na kumuishi pasipo kiburi, chuki, au hisi mbaya. Kama watoto, hatupaswi kuwa na mashaka na lile atufundishalo Kristo wala lile atuelekezalo kulifanya. Hivyo, “Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” Mk 10:15. Unyenyekevu na upole ndiyo siri ya kuupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo.

Kwa hali hii, watoto wadogo wanauishi wongofu wa kweli kwa sababu hawana walipojishikilia kama sehemu ya usalama wao zaidi ya wazazi wao, au walezi wao, au walimu wao. Kwa maana hiyo Yesu anasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Wongofu huu unatutaka mara zote kulenga lililo kamilifu licha ya kwamba udhaifu upo. Ni kuyatafuta yale yaliyo juu kule Kristo alipo. Ni kuishi maisha mapya ya ufufuko. Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.” Kol 3:1. Ni kuamini yapo maisha ya milele mara baada ya maisha ya hapa duniani ambayo ni jukumu la muda mfupi.

Wapendwa katika Kristo, na huu ndio mwaliko wa wale wote wanaoishi kama watoto wadogo katika hali ya Unyenyekevu, Upole, Upendo na Imani kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14. Kuwazuia watoto wadogo kwa weza maanisha hali ile ya kupandikizwa hofu na kuwa mbali na upendo wa Mungu Baba. Na inawezekana pia kutokana na mitazamo yetu, mila na desturi zetu zinatufanya kuwa mbali na upendo huu wa Mungu Baba. Milango ya Neema na Huruma ya kweli imefunguliwa kwa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Hakuna sababu ya kuwa na hofu ndani na katika Kristo Yesu. Kwake Kristo kuna baraka muda wote, Mk 10:16. Ndugu yangu uhitaji baraka kutoka kwa Kristo Yesu?

Jumuiya ya kwanza ya Wakristo walishirikishana Neema na Baraka hizo za Mungu pale walipoishi ndani na katika Kristo Yesu. Ni kwa namna hiyo Mtume Yakobo anasisitiza maisha hayo ya ufufuko ndani na katika Kristo Yesu: Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana,” Yak 5:14. Hapa tunaona uwepo wa Sakramenti ya Wagonjwa. Wagonjwa walipewa Sakramenti hii kuwarudishia afya ya mwili na roho, na kwa namna ya pekee kuwaandaa katika kifo chema na chenye matumaini makubwa na yaliyobeba fumbo zima ya ufufuko. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa,” Yak 5:15. Licha ya kwamba maisha ya Kikristo katika jumuiya yanatupa fursa ya kushiriki na kushirikishana upendo wa Kristo, maisha hayo pia yanatupa fursa ya kutakiana mema na kusamehana pale zinapotokea sintofahamu.

Tendo hili la msamaha wa kweli lilikuwa moja ya nafasi ya kuyaponya maumivu ya ndani. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii,” Yak 5:16. Maisha ya kusamehana na kuombeana yanafundisha kutokumpa ibilisi nafasi ya kuzitawala nafsi zetu. Hivyo hata pamoja na kuwa na hasiri, mkazo mkubwa wa kupatana uliwekwa pale ndugu katika jumuiya walipokoseana. Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi,” Efe 4:26-27. Kukawia kutoa msamaha ni kukaribisha makazi ya yule mwovu ibilisi kwani hayupo mbali nasi pale tunapofarakana. Katika kweli hii Mtume Petro anasema, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5.8. Kuwa na kiasi katika kila jambo ni kusema “sasa inatosha, na nisingependa kuendelea kuwa mtumwa katika jambo hili.” Ni kujiondoa katika minyororo hiyo (mizizi ya dhambi) isiyo na uzima ndani yake.

Minyororo hiyo yawezekana kuwa hii ifuatayo: moyo usiosamehe, chuki, kiburi majivuno, dharau, kujiona, kujitanguliza kwa kila kitu, wivu, nk. Ni katika maisha ya pamoja kama jumuiya hai ya Wakristo tunaweza kuonana vizuri na hasa katika vilema vyetu. Mwenye upendo wa kweli kwa mwenzake huwa kama kioo cha kujitazama kwa mwenzake ili kumrudisha katika kweli. Kwa maana hiyo  “Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi,” Yak 5:19-20. Kuna furaha kubwa sana mbele ya Mungu tunaporejeshana katika kweli, kusamehe, na kuanza upya ndani na katika Kristo Yesu. Ha ndiyo maisha ya Ufufuko.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi,” Yak 5:19-20


Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ya kuona vilema vyetu vinavyozuiya kuuona uso wako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario