jueves, 12 de mayo de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU MATHIYA MTUME

Sikukuu ya MTAKATIFU MATHIYA Mtume
14/5
Somo: Mdo 1:15-17, 20-26
Zab: 113:1-2, 3-4, 5-6, 7-8
Injili: Yoh 15:9-17
Nukuu:
Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi,” Mdo 1:21-22

Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe,” Mdo 1:24-25

Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja,” Mdo 1:26

Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo,” Yoh 15:9
Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10

Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12 

Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki,” Yoh 15:13

Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:15

Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16

TAFAKARI: Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12 

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtume Mathiya. Tukumbuke kwamba Mitume waliochaguliwa na Yesu walikuwa kumi na mbili, na kufanya lile kundi lililokuwa karibu sana na Yesu, yaani Thenashara-kumi na wawili. Baada ya Yuda Iskariote kumsaliti Yesu na kujinyonga kundi hili la Mitume likawa na upungufu wa mmoja. “Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni shetani?” Yoh 6:70. Hivvo Mitume kwa umoja wao wanao waliona ni vyema kumchagua mmoja mwenye sifa zifuatazo; Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi,” Mdo 1:21-22

Baada ya vigezo na masharti kuzingatiwa kwa kina, walipatikana watu wawili, yaani, Barsaba na Mathiya. Hatua ya pili kabla ya kufanya uchaguzi, waliwaweka katika maombi kwa kuwakabidhi kwa Bwana Yesu Kristo awapatie yule atakaye fuata nyayo zake kimamilifu. Hivyo, wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe,” Mdo 1:24-25.

Baada ya hatua hii ya maombi, ilifuata hatua ya tatu yaani kupiga kura. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja,” Mdo 1:26. Mathiya akachukua ile nafasi iliyokuwa wazi baada ya kifo cha kujinyonga cha  Yuda Iskariote, aliyemsaliti Bwana wetu Yesu Kristo. Tangu nyakati hizo, Kanisa limekuwa likifuata taratibu hizi hasa pale ambapo mmoja wa maaskofu kufariki, au kustaafu, au kutokana na hitaji la mchungaji mkuu, yaani Askofu.

Wapendwa, mambo haya yote Mama Kanisa anayafanya ili kuendeleza na kuuishi ule upendo aliyotuachia Kristo. Upendo kwetu sisi wafuasi wake Kristo ni Amri. Mkristo bila upendo ni kichokoo fulani hivi. Kama mchungwa unavyojulikana kwa matunda yake, hivyo hivyo nasi kama wafuasi wake Kristo yatupasa daima kujulikana kwa upendo wetu na jirani zetu. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Kupenda huku kunaendana na kuishi katika kweli na haki. Ukipenda kweli utaishi katika kweli, na kweli hiyo itakufanya utende haki kwa wali unaoishi nao.

Kuishi katika hali hii ya upendo, ukweli na haki, ndicho kitakachotutambulisha mbele za watu na hasa wale wasiomjua Kristo. Leo sisi kama wafuasi wa Kristo tunasisitizwa sana kuishi ushuhuda wa ‘ukimya’ ambao unajidhihirisha zaidi kwa upendo, ukweli na haki. Ni ukweli usiotia shaka kwamba wapo watu ambao leo hawataki kusikia kabisa neo ‘Yesu,’ ‘Kristo,’ ‘Katoliki.’ Nasi hatuna sababu ya kuwalazimisha kuyasikia. Ila tunaweza kuwafanya kuyaelewa maneno hayo tunapotoa ushuhuda wetu wa ukimya kwa kupendana sisi kwa sisi, kuwapenda, kuwa wakweli, na kuwa watu wa haki kama alivyo Kristo mwenyewe. Huku ndiko kuzishika amri za Kristo, na kumtambulisha kwa wale wasiomjua na kumpenda au kutokutaka kumsikia. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10

Wapendwa wana wa Mungu, kukaa katika pendo la Kristo ni kuhesabiwa haki na Kristo mwenyewe. Kristo hapendi kuwa mchoyo wa upendo huu na ukaribu aliokuwa nao na Baba Mungu. Kipimo kile kile alichopendwa na Mungu Baba, ndicho kipimo hicho hicho anachotupenda sisi. Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo,” Yoh 15:9. Mfumo huu wa upendo, makuzi na kukomaa kwake ni kujitoa sadaka kila siku. Kujitoa sadaka kwa ajili ya upendo na kutambua upendo aliotupenda Kristo kama shukrani ya wokovu wetu. Kielelezo cha upendo sadaka ni Kristo mwenyewe. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki,” Yoh 15:13. Hapa ndipo tunapoona sababu ya kuumbwa wetu, na malengo ya kuwa katika ulimwengu huu.

Ndugu yangu, haukuumbwa kwa bahati mbaya, na usiyekuwa na malengo hapa duniani. Hapa hapa duniani kwa misioni maalumu ambayo yakupasa kuitimiza kadiri ya vipaji na wito aliokujalia Mungu. Kama utajua hupo hapa kwa misioni fulani unayotakiwa kuitimiza kila unapojaliwa pumzi, huwezi kuchezea Muda wako hata kidogo. Hii ndiyo sababu kubwa ya sisi kuitwa na Yesu marafiki zake. Ni marafiki zake kwa sababu anataka muda wote kutumegea siri ya yale yaliyojificha ndani mwetu, maishani mwetu, na kule tunakotamani kupajua na kufika. Hivyo Yesu anatuambia, Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:15. Ni fuaraha kubwa sana kuwa marafiki wa Yesu. Tumethaminiwa sana kupewa nafasi hiyo bure.

Uteuzi huu wa kuwa marafiki wake Yesu unaonyesha ni kwa namna gani Yesu achoki kutufikiria. Unapoelewa ukweli huu, huwezi hata mara moja kujisikia kutengwa na Yesu. Huwezi hata mara moja kujisikia mpweke au kutokuwa na msaada pale unapokumbana na matatizo. Hata kwenye matatizo hayo Kristo yupo. Lengo lake kubwa ni kukupata na siyo kukupoteza. Tunaposafiri naye katika vilindi hivi vya matatizo na mateso bila kukengeuka, utujaza neema na baraka kuyashinda matatizo na mateso hayo. Katika hali hii, Mungu hatuondolei uhuru wetu wa kutokuamua na kufanya vingine. Anatutaka tuwe huru na si watumwa. Tumfuate kwa uhuru wetu na kweli. Anatutaka tuwe hivyo muda wote kwa sababu aliona hivyo kabla yetu. Hivyo Yesu anasema, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16

Wapendwa wana wa Mungu, tukijua kiini hiki cha upendo wa Kristo ndani yetu, tutajua maana halisi ya wajibu wetu kama wafuasi wake. Kama najua napendwa na Kristo kama Yeye alivyopendwa na Baba Mungu, hivyo nami ili nizae matunda katika upendo huu wa Kristo na Mungu Baba yanipasa kupenda bila kipimo. Je, nianzie wapi zoezi hili? Anza hapo ulipo!

Tumsifu Yesu Kristo!

Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16


Tusali: Ee Yesu, tuwashie moyo wa upendo wako, nasi tupendane kama ulivyotupenda. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario