JUMATANO
WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo:
Yak 4:13-17
Zab:
49:2-3, 6-7, 8-10, 11
Injili:
Mk 9:37-39
Nukuu:
“Haya
basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo
mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida,” Yak 4:13
“walakini
hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao
kwa kitambo, kisha hutoweka,” Yak 4:14
“Badala
ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi,” Yak 4:15
“Lakini
sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya,”
Yak 4:16
“Basi
yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi,” Yak 4:17
“Yohana
akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye
hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi,” Mk 9:38
“Yesu
akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu
akaweza mara kuninenea mabaya; kwa
sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu,” Mk 9:39-40
TAFAKARI:
“Yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi,”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni kweli ugonjwa wa Malaria na UKIMWI umekuwa tishio kubwa kwa afya na
maendeleo katika Taifa letu la Tanzania kwa muda mrefu sasa. Maradhi haya
yamekuwa huzuni na wakati mwingine sababu kubwa ya mahangaiko na mifarakano
kifamilia, kiuko, na hata mahusiano ya karibu baina ya watu na ndugu. Pamoja na
maradhi hayo niliyoyataja na mengine mengi tu yakiibuka kila kukicha, jamii
yetu leo kama Watanzania imetikiswa na tunateketea kwa “Saratani unafiki.”
Mtume Yakobo leo ameielezea kwa undani saratani hii unafiki. Ni hali ile ya
kuujua ukweli/kweli lakini hutaki kufanya au kutenda kadiri ya kweli ile, na
badala yake unafanya ndivyo sivyo ama kuwafurahisha watu, mtu (bosi wako), au
itikadi fulani kadiri ya mfumo fulani usiopenda kweli na haki kwa sababu tu
kulinda maslahi fulani tena ya wachache fulani tu.
Wapendwa wana wa Mungu
na yeyote yule wenye hofu ya Mungu, unafiki huu kwa namna nyingine ni dhambi ya
kijamii, yaani, “social sin.” Dhambi hii ndiyo ambayo Mtume Yakobo anasema, “yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake
huyo ni dhambi,” Yak 4:17. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii,
nikuombe utazame hali halisi hapo ulipo (familia yako, jamii inayokuzunguka,
kazini mwako, hali halisi na mazingira ya sasa ‘kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni,
na kijami’) na ugonjwa huu hatari, yaani UNAFIKI. Je, wewe kama Baba au Mama
katika familia yako, kiongozi wa serikari au dini wauona ukweli na kufanya
kadiri ya kweli hiyo? Kama unaona na hufanyi dhamiri yako bado ipo hai? Na kama
unaona kweli hiyo ila unafanya kinyume chake, je wamfurahisha nani? Je, wamjua
unayetakiwa kumtumikia katika kweli na haki? Ndugu yangu, kama umepewa dhamana
na umma wa watu na kwa nafasi hiyo unawaangamiza kwa maslahi niliyokwisha
kuyasema hapo juu, muogope sana Mungu ukijua unawiwa deni kubwa kwa pumzi
aliyokupa. Unafiki wa kiwango hiki huwezi kuwa na ujasiri wa kuyasema maneno
haya mazito aliyoyatamka Mtume Paulo: “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa;
katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona
njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza
mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Flp 4:12-13
Ndugu yangu, nafasi
uliyo nayo, uwezekano ulio nao na dhamana uliyopewa ni kupigana kuliondoa giza
la ujinga, chuki, umasikini wa watu na mazingira yao, uonevu na ukandamizaji wa
hali za watu. Kwa namna nyingine hapo ulipo kuwa chumvi na mwanga kama Kristo
Yesu anavyotusihi, kwamba, “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na
kukanyagwa na watu,” Mt 5:13. Tu chumvi katika jamii kwa kuuona ukweli, kuwa
sehemu ya ukweli huo, na kuibadilisha hali ile isiyo ya kweli kwa kuleta ladha
nzuri zaidi kama chumvi ifanyavyo. Tendo hili litakufanya uchanganyike na watu
ili kuleta na kukoleza ladha hiyo, yaani, pale pasipo na haki, basi haki
itendeke, pale pasipo na utu, basi utu uheshimiwe, pale palipo na ubaguzi, basi
usawa uwepo, na pale palipo na chuki, basi upendo utawale. Huku ndiko kuona,
kujua, kuguswa, kutenda, na kutetea kuliko kweli na haki kama alivyofanya na
kutufundisha Bwana wetu Yesu Kristo. Na hili ndilo fumbo la “kuwa chumvi.”
Hivyo chumvi ikikosa ‘uchumvi’ huu ni ‘kuputwa nje na kukanyagwa na watu,’ Mt
5:13b. Vita hii si rahisi. Gharama yake ni kubwa kama tusivyoweza kuutenganisha
utukufu na msalaba. Hivyo yanipasa kuishinda hofu ili niwe mbali na unafiki na
kutenda kweli na haki hata kama kwa kufanya hivyo itanibidi kutoa sadaka kubwa
ya maisha yangu.
Wapendwa
wana wa Mungu, tu mwanga kwa kuwa na kuishi maadili mema. Kila kazi au taaluma
fulani ina maadili yake na miiko yake. Hivyo, kazi hiyo au taaluma hiyo
ikipoteza nguvu yake ya kimaadili ni sawa kuendesha gari katika kiza kinene
pasipokuwa na taa. Ni wazi katika hali hiyo lolote linaweza kutokea, na
haliwezi kuwa jambo zuru katika usalama wako na chombo chako cha usafiri, yaani
gari lako. Hivyo, Yesu anatuambia, “Taa ya
mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga;
lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Angalia
basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza,” Lk 11:34-35. Mwaliko wa kuwa
mwanga ni kutenda kimaadili katika uelekezi wa hofu ya Mungu ndani yetu.
Tunakosa kuwa chumvi na mwanga tunapoikubali na kufifishwa na “Saratani
unafiki.” Hapa ndipo penye chanzo na dhambi hii ya kijamii-“social sin.” Ndiyo
maana kila kukichwa hatukosi kusikia habari za uovu uliokidhiri katika jamii
yetu leo. Neno ‘kupiga dili, ufisadi, n.k,’ yanataka kuwa maneno ya kawaidi na
sifa katika jamii. Wachache wetu kwa kuwezeshwa na mfumo tuliokuwa nao wamepata
fursa ya kujineemesha na kuzikanyaka haki za walio wengi, masikini na wanyonge.
Mitazamo na maisha ya wacheche hawa ni kama asemavyo Mtume Yakobo, “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia
katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata
faida,” Yak 4:13. Kila kona ni ‘kupiga dili na harufu ya ufisadi.’ ‘Saratani
unafiki’ inaangamiza Taifa la wana wa
Mungu!
Jambo la kukumbuka kwa yeyote yule
asiyependa kutenda lililo jema ilihali anajua, ajue kwamba maisha ya hapa
duniani ni jukumu la muda mfupi. Kuishi na kutotambua ukweli huu ni kuishi bila
kujua “yatakayokuwako
kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha
hutoweka,” Yak 4:14. Ndugu yangu, katika
ulimwengu huu, mwanadamu hawezi kudumu milele katika fahari yake. Tupo kwa muda
fulani tu, tena uliofichwa na Yule aliyetupa pumzi yaani Mungu. Jeuri yako na yangu
inatoka wapi? “Badala ya kusema,
Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi,” Yak 4:15. Tumekuwa watu
wa kutamka maneno mazito utafikiri tu washauri wa Mungu! Kiburi chetu kinatoka
wapi? Ndugu zangu, “Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu;
kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya,” Yak 4:16. Tumwogope Mungu tukijua tu
binadamu tu, na uhai wetu tumeazimwa kwa muda fulani tu. Ukweli ni ukweli tu hata ukisemwa na yule
ambaye haendani na mitazamo yetu na itikadi zetu. Hiki ndicho anachokikemea
Yesu kwa wanafunzi wake, na hasa pale Yohana anapotoa taarifa ya utume wao na
kusema, “Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye
hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi,” Mk 9:38. Hali hii ya
“USISI” Yesu anaikemea kwa maelezo yafuatayo: “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya
mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu
upande wetu,” Mk 9:39-40. Kweli hubaki kuwa kweli hata ikisemwa au tendwa na
yule au wale wasiofuata mitazamo na itikadi zetu. Je, tuyaonayo leo katika
jamii yetu yanamulika fundisho hili la Yesu?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yesu
akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu
akaweza mara kuninenea mabaya; kwa
sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu,” Mk 9:39-40
Tusali:
Ee Yesu, uliyesimama imara katika upendo, kweli, na haki hadi mwisho, tena
mwisho katika kifo kile cha msalaba, nijalie neema na nguvu ya kuona, kujua, kuguswa, kutenda, na kutetea kuliko
kweli na haki kama ulivyo ishi na kufia. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario