SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU-C
Somo:
Mit 8:22-31
Zab: 8:3-8 (K) 1
Somo
II: Rum 5:1-5
Injili:
Yoh 16:12-15
Nukuu:
“Ndipo
nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku;
Nikifurahi daima mbele zake,” Mit 8:30
“Nikiifurahia
dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu,” Mit
8:31
“Basi
tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye
kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani
yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu,” Rum 5:1-2
“na
kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na
tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika
mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi,” Rum 5:4b-5
“Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh
16:13
“Na
yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo
yangu, na kuwapasheni habari,” Yoh 16:15
TAFAKARI:
Tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, tu na amani kwa Mungu, kwa njia
ya Bwana wetu Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu tuliyepewa. Huu ndiyo Utatu
Mtakatifu na umoja usiogawanyika.”
Wapendwa wana wa Mungu
leo Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya Utatu Mtakatifu. Jumapili iliyopita
Mama Kanisa alisheherekea Sikukuu ya Pentekoste kama siku rasmi ya kuzaliwa
kwake, yaani Kanisa. Sherehe ya Pentekoste, yaani kuvuviwa kwa Roho Mtakatifu
kwa Kanisa na Waamini wake kunalifanya Kanisa kuwa chombo na Sakramenti ya Wokovu
katika umoja usiogawanyika, yaani Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Na
ndiyo maana agizo msingi la Yesu na kwa Kanisa baada ya Pentekoste ni
kuuinjilisha ulimwengu wote, na kuwabatiza kwa Jina la Baba, na la Bwana, na la
Roho Mtakatifu wale wote watakao upokea wokovu huo.
Leo kwa namna ya pekee
tunaalikwa kuzama ndani zaidi juu ya Utatu Mtakatifu na Umoja huu
usiogawanyika. Mpendwa tunayesafiri sote katika tafakari hii, ya kupasa kuelewa
ukweli huu kwamba, Ukristo na tukienda ndani zaidi Ukatoliki kwetu, siyo tokeo
la ugunduzi wa akili ya mwanadamu au wanadamu, bali ni dini ‘funuliwa’ na Mungu
mwenyewe kwa watu wake na aliopendezwa nao. Hivyo ni zawadi ya Mungu mwenyewe
aliyopenda kuwashirikisha watu wake. Ufunuo huu wa Mungu kwa watu wake
umejidhihirisha kwa matukio mbalimbali katika historia nzima ya wokovu wa
mwanadamu, yaani, Uuumbaji, Ukomboaji, na Utakatifuzwaji wa kile kilichoumbwa
na kukombolewa. Hapa ndipo tunapoweza kuona Utatu huu Mtakatifu na Umoja huu usiogawanyika.
Hivyo mwanadamu huyu aliye huru na bila kushurutishwa anao wajibu wa kuitikia
ufunuo huu. Mwitikio huu wenye lengo la kuelewa siri na fumbo hili la ufunuo wa
Mungu kwa watu wake ndiyo tunayoiita Teología-‘tahuidi ambayo imegawanyika
katika matawi tofauti.’ Hata hivyo leo siyo lengo langu kuyaongelea mgawanyiko
huo kiteologia.
Wapendwa wana wa Mungu,
masomo yetu yote matatu ya leo yanatutafakarisha na kutuwezesha kwa kiasi
fulani kuuona Utatu huo Mtakatifu. Ni kuuona katika maana ya kutafakari, na
siyo kuujua katika maana ya uhasili wake kwa sababu ni Fumbo. Utatu Mtakatifu
ungekuwa ni ‘tatizo’ basi tungekuwa na jibu lake. Kwa vile Utatu Mtakatifu ni
‘fumbo’ hatuna jibu lake katika ukamilifu wake. Tunachojaribu kufanya ni
kuueleza katika maana ya kuzama katika tafakari ya fumbo hilo. Na katika kuzama
huko ndipo tunapozidi kufunuliwa siri hiyo. Ni Utatu Mtakatifu katika maana ya
nafsi tatu: Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Ni umoja usiogawanyika katika
maana Mungu ni mmoja. Tofauti ipo tu katika utendaji. Hata hivyo katika
utendaji wa moja ya nafsi hizi tatu za Mungu, siyo kwamba katika tenda yake
(nafsi moja) hizo nafsi nyingine hazipo.
La hasha!
Somo la kwanza linatupa
jibu la utendaji huu katika kuifunua wazi nafsi moja, na wakati huo huo
nyingine zikiwa katika utendaji uleule. “Ndipo
nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku;
Nikifurahi daima mbele zake,” Mit 8:30. Ni
wazi kazi ya uumbaji na inavyojionyesha imefanywa na Mungu-nafsi ya kwanza ya
Mungu, ila hapo hapo nafsi ya pili ya Mungu, yaani Mungu Mwana kushiriki kwa
kiasi kikubwa sana. Mwinjili Yohana anatuambia ukweli huu kwa kusema, “Vyote
vilifanyika kwa huyo (Mwana); wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika,” Yoh 1:3. Maneno “ndipo niliokuwa pamoja naye,” katika nukuu
kutoka somo la kwanza yanaturudisha kwenye uhasili wa Neno kabla ya kumwilishwa
na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Mwinjili Yohana katika hili anasema, “Hapo
mwanzo kulikuwako Neno (Mwana), naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno
alikuwa Mungu,” Yoh 1:1. Huu ni uthibitisho wa umoja usiogawanyika katika
utendaji.
Neno, yaani Mwana nafsi
ya pili ya Mungu, kufanyika mwili na kukaa kwetu ni tokeo la upendo usio na
kipimo wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Hii ndiyo furaha ya Mungu kama
tulivyosikia kutoka somo letu la kwanza, kwamba, “Nikiifurahia
dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu,” Mit
8:31. Mungu hakuwahi kutuacha hata mara moja tangu alipokusudia kutushirikisha
furaha yake katika uumbaji wake. Furaha ya Mungu na mshikamano huu kwa viumbe
vyake ulijidhihirisha kupitia nafsi ya pili ya Mungu, yaani Neno lile lililomwilishwa
na kukaa kwetu-Yesu Kristo. “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila
mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Kumwamini Mwana
wa Mungu si tokeo la akili na nguvu zetu, wala tokeo la kina kama sehemu ya
tafakuri yetu. Kumwelewa Mwana wa Mungu tunawezeshwa na nafsi ya tatu ya
Mungu-Roho Mtakatifu. Roho huyu Mtakatifu ni tunda la upendo wa Mungu Baba na
Mwana. Hivyo Mtume Paulo anatuambia, “wala
hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu,” 1Kor 12:3b.
Roho huyu Mtakatifu anakazi ya kutuweka pamoja katika umoja aliyotuombea Mwana
kabla ya kujongea kikombe kile cha mateso Yoh 17:11b, na kulitakatifuza Kanisa
lake, yaani, wabatizwa wote.
Wapendwa
wana wa Mungu, wewe na mimi leo tunauishi Utatu huu Mtakatifu na umoja
usiogawanyika tunapoambatana pasipo kujipoteza katika malimwengu tukiwa ndani
ya Utatu huu kila mmoja kadiri alivyoitwa kutumika hapa duniani kama viumbe
shirikishwa katika uumbaji wa pili na Mungu-“co-creators of God.” Hivyo wito na
maisha yako unayoyaishi kwa uaminifu ni kwa namna hiyo hiyo unashiriki fumbo
hili Takatifu katika (kuumba, kikombo, na kutakatifuza malimwengu). Hapa ndipo
twawezwa kuhesabiwa haki katika imani hiyo. Hivyo “Basi
tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye
kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani
yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu,” Rum 5:1-2. Na kuishi Imani hii katika kweli, tumaini na
haki, tunawezeshwa na Roho Mtakatifu tuliyepewa. “Na kazi ya uthabiti wa
moyo ni tumaini; na tumaini
halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo
yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi,” Rum 5:4b-5. Je, ninalo la kujivunia au
kuona fahari juu ya kufunuliwa siri na fumbo hili la Utatu Mtakatifu na umoja
usiogawanyika? Sina!
Ndugu yangu, sina cha
kuona fahari isipokuwa jambo hili tu: “nisione
fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa
huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Kwa
kupitia Msalaba huu Mtakatifu mimi na wewe leo tupo huru na kuhesabiwa haki
kama wana na warithi wa Ufalme wa Mungu. Na kwa kutambua ukweli huu na
kushikamana nao ndivyo hivyo hivyo Roho Mtakatifu utufunulia kweli yote ya
mambo yale aliyotufundisha Kristo Yesu ikiwa ni pamoja na siri ya maisha ya
umilele. “Lakini yeye
atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh
16:13. Hapa pia tunaona umoja usiogawanyika wa Utatu Mtakatifu. Kwa maana Yesu
anasema, “Na yote aliyo nayo Baba ni
yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni
habari,” Yoh 16:15. Usifiwe Utatu Mtakatifu na Umoja usiogawanyika. Amina.
Wapendwa wana wa Mungu niwaache na mfano
huu tunaoujua wote, CHAI. Bila shaka licha ya sukari kuwa bidhaa Ghali na adimu
kwa sana, sote tuipendayo chai twaendelea kuisaka sukari kwa gharama yoyote
ile. Kuipata chai kama kinywaji na kiburudisho yakupasa kuwa na vitu vitatu:
Maji moto, Majani chai “Mchaichai,” na Sukari. Ukikosa kimoja wapo hapo,
hautakuwa na “kinywaji-chai.” Na vyote vikiwa pamoja na kufanya “kinywaji chai,”
kwa macho ya kibinadamu hutoweza kubainisha kipi ni kipi. Usifiwe Utatu
Mtakatifu na Umoja usiogawanyika. Amina
Tumsifu Yesu Kristo
“Na
yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo
yangu, na kuwapasheni habari,” Yoh 16:15
Tusali:-Ee
Yesu uliye Mwokozi wetu, Roho Mtakatifu umoja na mtakatifuzaji wetu, na Mungu
Muumba wetu, twakiri katika Mungu mmoja na nafsi Tatu. Tuwezeshe daima kwani ni
furaha yetu viumbe vyako kuwa katika Umoja huo daima na milele. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario