domingo, 22 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 8 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo: 1Pet 1:3-9
Zab: 111:1-2, 5-6, 10c
Injili: Mk 10:17-27
Nukuu:
Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4

ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo,” 1Pet 1:7

 “Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21 

 “Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27 

TAFAKARI: “Akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.”  

Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa wewe ni Mkristo uliye hai ni vyema ukafahamu thamani ya Ukristo wako, yaani umekombolewa kwa Damu ya thamani kubwa sana, yaani Mwana-kondoo, Yesu Kristo. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hivyo maisha yako na yangu hapa duniani tunapaswa kuyasalimisha yote na kwa asilimia zote kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai. Tendo hili la kujisalimisha ndiko kuabudu kwenyewe kuliko hai na kwenye kumpendeza Mungu.

Kujiita Wakristo bili Kristo ni kupotea muda kabisa kwa sababu kwa kufanya hivyo maisha hayo hayana njia, kweli, uzima (tungali hapa duniani) na ufufuo (maisha ya uzima wa milele), Yoh 14:6. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tungali hapa duniani wakuhimidiwa ni Mungu, na kwa njia ya pekee na ufunuo uliokamilika kwa Yeye aliyemwilishwa (Neno), Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa Kristo Yesu kuna Njia, Kweli, Uzima, na Ufufuo wa wafu. Kwake Yesu na kupitia kwake tunaheshabiwa haki na Mungu kwa wana na warithi wa ufalme wake Mungu. Na kwa namna hiyo, Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4. Ndugu yangu, tumaini yenye uzima lipo kwa Kristo Yesu, na siyo kwa kile tulicho au yale tunayoyamiliki hapa duniani. Tungali hapa duniani tu waangalizi wa muda mfupi kwa yale tunayoyamiliki. Kwayo (tunayoyamiliki) kama yalivyo hayana umilele ingawa tuliyakuta na tutayaacha.

Hivyo wapendwa katika Kristo, yatupasa mimi na wewe kuyashinda majaribu tukiwa na ufahamu kwamba ‘maisha ni jaribu,’ na kulishinda jaribu ndipo kunakotupatia Imani yenye thamani kupita yote tuwezayo kuwa nayo. Vita vyetu vya kiimani kama anavyotufundisha Mtume Petro ni kulishinda jaribu ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo,” 1Pet 1:7. Tokeo la kubebwa na ulimwengu wa vitu ni anguko kubwa la ‘uzuni.’ Furaha ya kweli ipo pale tunapoyasalimisha yote kwa Kristo Yesu. Kristo awe tegemeo na msukumu wa yote tuyafanyayo, na tumuone kwa wengine yale yote tuyafanyayo katika jamii tunayoishi. Lengo hapa siyo tu kuzishika au kuzifahamu amri za Mungu kama ndege yule ‘kasuku,’ bali amri hizo za Mungu zimulike uhai uliopo ndani yetu binafsi na wale wote tuliowekwa dhamana kwao ikiwa ni pamoja na  wale wenye uhitaji wa pekee.

Ndugu yangu bila shaka, hii ndiyo sababu ya Yesu leo kwenye Injili kumuuliza yule Mtu aliyetaka kujua afanye nini ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu. Yesu anamuuliza, Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako,” Mk 10:19. Kwa moyo wa ukunyufu na furaha Mtu yule anamjibu Yesu,  Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu,” Mk 10:20. Jibu hili linamfurahisha sana Yesu. Ila Bwana wetu Yesu Kristo hakuishia hapa tu. Yesu anakutaka wewe na mimi tufanye zaidi kwa ya yale ya kawaida (katika kupenda, kutenda, na hata kukopesha, Lk 6:32-34) kwani hayo hata wenye dhambi huyafanya. Hivyo Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21. Hapa ndipo penye utata na tatizo kubwa kwangu na kwako. Wengi wetu ni vigumu sana kujibadua katika ulimwengu wa vitu. Tupo tayari kufa na tai shingoni kuliko kuviachia vitu na kuwa huru; kifikra, kitendaji, na kihuduma, ili kuwa huru kufanya tu yale yaliyo ndani yetu kadiri ya mpango wa Mungu. Kwa kufanya hayo na kujishikilia kwa hayo hakuna fadhila ndani yake. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu,  na ndani yake hakuna fadhila,” Lk 6:35.

Hitaji hili la pili, yaani, ‘kufanya zaidi’ ili kujipatia fadhila linakuwa anguko na uzuni mkubwa kwa mtu yule aliyekuwa na hamasa kubwa sana ya kuurithi ufalme wa Mungu. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi,” Mk 10:22. Ndoto na furaha yake ya kuujua na kuurithi ufalme wa Mungu anakubali iyeyuke kwa sababu ya ulimwengu wa vitu. Ndugu yangu, leo hata ungekuwa na utajiri wa aina gani kuna mambo hutoweza kuyapata kwa utajiri wako huo hata kama bado tungali hapa duniani. Ngoja nikujuze machache; kwa utajiri na fedha ulizonazo waweza kuwa na marafiki wengi ila siyo wa kweli na watakatifu. Kwa fedha na mali ulizonazo waweza kujenga nyumba nzuri, ukawa na kitanda kizuri cha dhahabu (na chenye nakshi zote), ila huwezi kuununua uzingizi. Kwa fedha na mali ulizonazo leo hapa duniani unaweza kwenda kokote upendapo ila Mbinguni ni swala la kuhesabiwa haki na mastahili ya Mungu Mwenyewe.

Ndugu yangu, kwa fedha na mali ulizonazo leo waweza kununua chakula kizuri na chenye gharama, kichwaji kizuri na chenye gharama, ila hutoweza kununua hamu ya chakula hicho. Kwa fedha na mali ulizonazo waweza kuwanunua watu na kuwahonga watu, ili utimize hazma yako ya kuwa kile utakacho, ila hutoweza kumnunua Mungu wala kumrubuni. Mwisho wa siku Mungu atakudhihirishia kile kilichokuwa haki yako mbele ya watu wake uliowarubuni. Ayubu aliyepatwa na majanga makubwa katika maisha yake, na kupoteza yote aliyokuwa nayo, anatuambia hivi kuhusu mali na utajiri; “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe,” Ayu 1:21. Utajiri wake na mali alizokuwa nazo haikuwa sababu ya kumkufuru Mungu hata pale ilipoondolewa yote pasipo yeye-Ayubu, kwenda kinyume na matakwa ya Mungu.  Maandiko Matakatifu yanatuambia, Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu,” Ayu 1:22. Kwa nini basi mimi na wewe twaulinganisha au kuufananisha uhai wetu na mali tulizonazo na kumkufuru Mungu? Mali tunazoongelea hapa ni zote ikiwa pia zile zisizoshikika kama vipaji alivyokupa Mungu. Mbona basi twavimba vichwa na kujisahau pale tunapofanikiwa kutokana na zawadi aliyotupa Mungu ikiwa ni pamoja na ufahamu wa kiwango cha juu? Ndugu yangu, hayo yote si mali yako. Umekopeshwa au kupewa kwa muda tu, na ukiwa navyo ni kwa faida ya wengine. Huku ndiko kushirikishana utajiri wa Mungu na Utukufu wake. Mali yako halali ni dhambi zako.

Hivyo ni vigumu sana, tena sana, kuingia katika Ufalme wa Mungu tukishikamana na kulandana na vitu na katika fursa hiyo kutokumpa Mungu nafasi na mastahili yake. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” Mk 10:23. Kushikamana huko na vitu hakutupi heri yoyote, na badala yake ni anguko kubwa. Ndugu yangu, ni wale tu walio masikini wa roho (wenye nafasi ya Mungu ndani ya mioyo yao, Mt 5:3, na wasiokata tamaa wanapoudhiwa kwa kutenda haki kwa wote, Mt 5:10, ndio watakaourithi Ufalme wa Mbinguni. Na kwa sababu hiyo, kama washikamana na ulimwengu huu wa vitu na kutokumpa Mungu nafasi, Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mk 10:25. Fundisho hili lenye kweli yote linakuwa mshangao mkubwa kwa wanafunzi wa Yesu, yaani, wale Thenashara. Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27. Hivyo, ukijiachia kwa Mungu bila kujibakiza yote hufanyika kwako kadiri ya mapenzi yake Mungu na hitaji lako na wale wanaokuzunguka.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27


Tusali:-Ee Yesu, kwa Upendo wako tujalie Neema na Hekima ya kufahamu yale tunayohitaji ili kwa namna hiyo hiyo tuweze kufahamu hitaji au mahitaji ya wengine, na sote kwa pamoja tuweze kuurithi Ufalme wako wa Mbinguni.

No hay comentarios:

Publicar un comentario