JUMAPILI
YA 6 YA PASAKA YA MWAKA-C
Somo
I: Mdo 15:1-2, 22-29
Zab:
67:1-5, 7 (K) 3
Somo
II: Ufu 21:10-14, 22-23
Injili:
Yoh 14:23-29
Nukuu:
“Wakashuka
watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama
desturi ya Musa hamwezi kuokoka,” Mdo 15:1
“Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike
mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28
“Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana
Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake,” Ufu 21:22
“Na
mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia
nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo,” Ufu 21:23
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba
atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia,” Yoh 14:26
“Amani
nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.
Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27
“Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea
mpate kuamini,” Yoh 14:29
TAFAKARI:
“Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.”
Wapendwa
wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya sita ya mwaka “C” wa
Kanisa. Tafakari yetu ya leo inalenga kwa kiasi kikubwa tukio lile la
Pentekoste, na hasa ahadi ile aliyotuhaidia Bwana wetu Yesu Kristo kwamba, ‘huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina
langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.’ Leo
anatukumbusha ahadi hiyo tunapotafakari neno hili: “Na sasa nimewaambia kabla
halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini,” Yoh 14:29. Roho huyu
Mtakatifu ndiye aliyeliongoza “Kanisa la mwanzo” kwenye changamoto mbalimbali, na
hasa swala zima la kupokelewa na kushiriki
huduma za kikanisa kwa wale ambao hawakuwa Wayahudi. Ni Roho huyu pia
aliyewawezesha Mitume kufanikisha Mtaguso ule wa Yerusalemu. Na Roho huyu
Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kupanuka na kuenea kila kona ya dunia
hadi leo. Hata hivyo kwa kupanuka huku na kuenea kila kona kwa Kanisa hili la
mwanzo, lilikumbwa na kasumba ya ubaguzi uliolenga mila na desturi za Kiyahudi.
Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tendo la kutahiriwa kwa
wayahudi lilibeba tafsiri mbalimbali kwa kadiri walivyoishi na kufanya maagano
yao na Mungu.
Kama
tulivyoona katika tafakari ya masomo kwa wiki nzima hii iliyokwisha, kwa mara
ya kwanza katika historia yao-Wayahudi, tendo hili la kutahiriwa lilibeba maana ya usafi na kwa yule aliyetaka
kuoa lilichukua maana ya “Bwana harusi wa damu.” “Ndipo
Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga
miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe
akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri” Kut 4:25-26. Kutahiri kulimaanisha pia agano kati yao na Mungu hasa kwa tendo la Mungu kuwatoa utumwani
Misri, na hapa wanatairiwa kwa mara ya pili. “Wakati huo Bwana
akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana
wa Israeli mara ya pili. Basi
Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko
Gibea-haaralothi. Na sababu ya
Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu
waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka
Misri,” Yos 5:2-4. Kutahiriwa pia kulimaanisha kushika torati kikamilifu. “Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya
torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?”
Rum 2:26. Pamoja na sababu nyingine zote tulizokwisha kuziona, hii ya
mwisho ndiyo iliyotumika kama kigezo cha alisiye Myahudi kupokelewa katika
jumuiya hii ya Wakristo wa kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa walikuwa Wayahudi.
Hapa tunaambiwa, “Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale
ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka,” Mdo 15:1
Mambo haya ya nje hayakupaswa
na hayapaswi kuwa sababu ya kutokuishi upendo wa Kristo katika Kanisa. “Hapo hapana Myunani
wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala
mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11. Maandiko Matakatifu,
hasa Habari Njema ya Bwana wetu Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili
Yohana inasema ukweli huu wa Kristo, kwamba, Uzima wetu, na uhai wetu kiroho ni katika
Kristo Yesu aliye mzabibu nasi matawi yake. Kuishi katika ukweli huu ni kuzaa
matunda, yaani kuwa watu wa upendo, haki
na amani kama Kristo mwenyewe. “Kila tawi
ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi
kuzaa,” Yoh 15:2.
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, “sisi sote tuna mastahili sawa mbele ya Kristo, yeye ndiye
aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda ya kudumu.” Yakiwa haya
ndiyo majumuisho ya Mtaguso wa Yerusalemu, Kristo anatupenda kama tulivyo na
kutuhesabia haki mbele zake na mbele ya Mungu Baba bila kujali familia
tulizozaliwa, koo tulizotoka, kabila tulizotoka, na hata mataifa tuliyotoka.
Hakika, ingekuwa haya niliyoyataja kuwa kigezo cha kuwa Mkristo na hata kuwa
Mtumishi katika Kanisa lake KRISTO, bila shaka ingekuwa ndoto leo mimi au wewe
kuwa kama nilivyo ndani na katika KRISTO. Ni katika msingi huu nilioutaja
(Kristo ametuchagua bila ya mastahili yetu), Mtaguso wa Yerusalema wanaafikiana
vyema kuhusu swala la watu wa mataifa waliolipokea neno na kuunda ujumuiya ya
Kikristo. Ukristo wetu hautokani na hayo matabaka niliyoyasema hapo juu.
Ukristo wetu unatokana na kuhesabiwa haki na Kristo mwenyewe, kulikotokana na
kutupenda upeo, Yoh 13:1. Hivyo Mtaguso wa Yerusalemu unatoa tamko lifuatalo, “sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja,
kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25. Mtume Paulo na Barnaba wanachaguliwa
kwa vigezo vya maisha yao kupeleka ujume huu kwa wale waliolipokea neno. Ni “watu
waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo
15:26.
Hata
hivyo Yuda na Sila ndio watakaosema kwa vinywa vyao juu ya ujembe huo. “Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia
wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao,” Mdo 15:27. Yuda na Sila bila shaka
ni watu waliokuwa karibu sana na jumuiya hiyo mpya ya Antiokia. Uwakilishi huu
ni njia mojawapo ya kuboresha ukaribu wao na jumuiya ya Yerusalemu, na kuanza
kuishirikisha jumuiya hii mpya ya Antiokia yale yote yamuhusuyo Kristo. Ukaribu na umoja huu si wakubebeshana mizigo,
bali ni fursa ya kuyatafakari makuu ya Mungu na upendo wake kwa kila mmoja
aliyeridhia upendo na umoja huo wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye mleta umoja
huo. “Kwa maana ilimpendeza Roho
Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28.
Hivyo
basi, ili kuendelea na umoja huu na upendo huu ndani na katika Kristo,
iliwapasa kujitenga na yale ambayo hayakuwa na mwelekeo wa Kimungu. Ni ukweli
kwamba kama tunataka kuishi katika Kristo, yatupasa kujikana wenyewe na
kumfuata. Yatupasa kuacha yale ya zamani na kuyachuchumilia yale yampendezayo
Kristo. Hivyo basi, jumuiya hii mpya ya Antiokia, inapaswa kufanya haya
yafuatayo; “yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu,
na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya
vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Tunapoachana na makandokando haya ya maisha ndipo
tunapokuwa karibu na upendo wa Kristo na kutimiza mapenzi yake. Huu ndio upendo
anaotutaka Kristo tuuishi kama familia yenye hofu ya Mungu na kuwajibika. “Amri yangu ndiyo hii,
Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Ndugu yangu, jambo hili si
rahisi! Mimi na wewe leo tupo hiki tulicho kama tokeo la historia yetu tangu
kuzaliwa, makuzi yetu ambayo yameathiriwa na mila na desturi zetu, ufahamu wetu
ambao umeathiriwa pia na mfumo mzima wa elimu tuliokuwa nao. Katika mazingira
hayo ya makuzi, lengo ni kuuona ukweli kama ulivyo, na siyo kuuona ukweli kama
tulivyo. Hapa ndipo penye tofauti kubwa ya kusoma na kuelimika. Wote
walioelimika wamesoma, ila siyo wote waliosoma wameelimika. Hapa kusoma
simaanishi kwenda darasani kama ilivyo ada, bali kuyaelewa vizuri mazingira
yanayokuzunguka, ambayo kwa kiasi kukubwa si lazima kwenda darasani kadiri ya
mfumo unavyotutaka. Hivyo kwa mazingira ya Kanisa la mwanzo, na changamoto
iliyowakabili, Mtaguso ule uliwalazimu kuyaona yote katika upendo wa Kristo na
hatma ya upendo huo ambao ni kifo kile cha Msalaba.
Ndugu yangu, kuukubali
ubinadamu wetu ni pamoja na kujitambua na kuzishika amri za Mungu kwani twataka
kuongozwa na Mungu na kuwa watoto wa Mungu. Hivyo Yesu anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye
anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na
kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Nani asiyependa kutambuliwa na Mungu? Embu
fikiri yote uyafanyayo leo kadiri ya wito wako mwisho wa siku yanakosa kibali
mbele ya Mungu. Kumpenda Mungu ni kushika amri zake. Kristo kesha tuambia ni
amri ipi iliyo kubwa kuliko zote. Je, neno UPENDO ni geni kwako? Yesu anasema, “Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu;
nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24.
Hata Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani hakujifanyia mambo yake
kadiri atakavyo. Alikuwa makini sana kutimiza mapenzi ya yule alimpeleka yaani
Mungu Baba. Swali la kujiuliza mara zote ni hili, je, hapa nilipo na kadiri ya
agano au maagano yangu kimaisha ninayafanya mapenzi ya Mungu? Kama jibu ni
hapana, Je, nimejiandaaje kujibu swali hili siku ya mwisho?
Ndugu yangu, mpango wa Mungu kwetu na hasa
swala zima la maisha ya umilele limeratibishwa vizuri sana. Nafasi uliyokuwa
nayo leo na “mawezekano yake kimaisha,” hayapo kwa bahati mbaya kwako au kwa upendeleo.
Yote haya yanasababu kubwa kuhusu maisha yako ya sasa na wale wanaokuzunguka,
na hatma yake, yaani, umilele. Hata
hivyo, kwa kutusaidia, Yesu Kristo anatukumbusha jambo muhimu sana ndugu zangu.
Naye anasema, “Lakini huyo Msaidizi, huyo
Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na
kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26. Hivi kama tumefundishwa yote na
kukumbushwa yote tunayosababu ya kushindwa mtihani ulio mbele yetu? Ni katika
maana hii Yesu anatuambia mwisho wa kiama jambo hili litatokea kwa hakika.
“Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na
Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje,” Lk
13:28. Neno hili “kusaga meno” limesemwa mara sita katika Habari Njema ya Bwana
wetu Yesu Kristo kama iliyoandikwa na Mwinjili Matayo, mara moja kama
ilivyoaandikwa na Mwinjili Marko na mara moja kama ilivyoandikwa na Mwinjili
Luka. Maana yake ni kwamba hakutakuwa na nafasi ya kujitetea kwani nafasi ya
kufanya vema ni leo na sasa. Kristo Yesu angali hapa duniani aliweka yote sawa na kusema bila kupindisha
neno, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Yesu Kristo ni
njia kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua
Yesu ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukuliana kindugu katika
misalaba ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu, tunakutana naye Kristo
katika hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii
tunakutana nayo katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno,
kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi
wa neno.
Na Yesu Kristo ni
uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika
mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi
ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni
ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa
ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh
6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo
la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa
kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na
roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.
Kuliishi kiaminifu
fundisho hili zito la Kristo, Yoh 14:6, kunatusaidia kuzama ndani ya ule ufunuo
wa Yohana na kuona uzuri wa maisha ya umilele kadiri ya somo letu la pili leo.
Naye anasema, “Nami sikuona hekalu ndani
yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake,” Ufu
21:22. Maana yake ni nini?
Basi mpendwa katika
Kristo kwa kuelewa zaidi juu ya neno hilo la Ufunuo 21:22, nikuache na mfano
huu:-Bila shaka wengi wetu tuna mawazo ya “kuwa TENA kile tulicho leo na sasa
baada ya maisha haya hapa duniani.” Mathalani, kama mimi leo Mama Kanisa
kanihesabia haki ya kuwa mtumishi wake na muhudumu kama ‘Baba Paroko au Askofu,’
kwenye maisha baada ya kifo-umilele, hakutakuwa tena na wajibu huo kama Paroko
au Askofu kwa sababu huko hakutakuwa na “mwonekano,” “muundo,” “mfumo” tena wa
kiparokia au kijimbo. Nawe ndugu yangu unayeishi leo Sakramenti yako ya ndoa ni
kukumbushe maneno haya ya Yesu; Naye anasema “Wana
wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini,
wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka
katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala
hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu,
kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:34-36. Je, maneno haya ya Yesu na yale
ya ufunuo wa Yohana 21:22, yanasema chochote katika maisha yako leo?
Wapendwa wana wa Mungu,
bila kujali mtindo wa maisha tunaoishi leo kila mmoja kadiri ya wito wake, sote
katika maisha ya umilele tutajulikana kwa cheo chetu tu, yaani, utakatifu wako. Na mahali pa kuutafuta
utakatifu huo ni hapa hapa duniani kwa muda huu mfupi tuliokuwa nao. Hivyo, haijalishi
mimi ni nani leo, ila kila siku yanipasa niyaone maisha yangu katika mtazamo wa
Kimungu, yaani: Maisha ya duniani ni jaribu, Maisha ya duniani ni dhamana, na
Maisha ni jukumu la muda mfupi. Utukufu
wa Mungu ambao ni UTAKATIFU WAKE ni mwanga na nuru ya kutosha katika maisha
hayo ya umilele. Utakatifu wa kila mmoja wetu ambacho ndicho cheo chetu, ni ile
hali halisi tutakayokuwa nayo wakati tulipoumbwa, yaani, ‘sura na mfano wake
Mungu,’ Mwa 1:27. Hivyo, “wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala
haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa,
tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo,” 1Yoh 3:2. Kumwona
Mwana-Kondoo huyu, Yesu Kristo kama alivyo kwawezekana tu katika hali ya
utakatifu wako. Kwa sababu, “Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza,
kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo,” Ufu 21:23.
Je, bado taa yangu inawaka, yaani, UTAKATIFU wangu? Je, ile sura na mfano wa
Mungu ndani yangu bado inang’aa, au ishafifishwa na mali yangu halali, yaani,
dhambi zangu? Tafakari!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini
huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,
atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26
Tusali:-Ee Yesu, uliye
Mwana-Kondoo na taa halisi ya Mungu, niwezeshe kila siku kutoififisha ile sura
na mfano wa Mungu ndani yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario