miércoles, 4 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 6 YA PASAKA

JUMAMOSI WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo: Mdo 18:23-28
Zab: 47:2-3, 8-9, 10
Injili: Yoh 16:23-28
Nukuu:
 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko,” Mdo 18:24

Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi,” Mdo 18:26

Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28

Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27

TAFAKARI: “Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni siku nyingine tena na kwa neema ya Mungu twalitafakari neno lake la uzima. Leo, kwa namna ya pekee tulitafakari neno hili, “Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi.” Upendo wa Baba kwetu ni matokea ya upendo wetu kwa mwanaye, Yesu Kristo. Kumpenda Kristo ni kushika na kuishi yake aliyotufundisha. Hatuyafanyi hayo kwa ajili yetu binafsi, ila kwa ajili ya wengine. Kristo kautoa uhai wake si kwa ajili yake binafsi, bali kwa ajili yetu sote, na kutufanya huru kutoka kifungo cha dhambi. Kwa sadaka yake pale msalabani sote tumerudishiwa ile hadhi ya kuwa warithi na wana wa Mungu.

Tukiyafanya hayo na kuishi msingi huu wa Imani, ni kielelezo tosha kwa kumpenda Mungu kwa kuishi yale aliyotufundisha Kristo. Tendo hili litatupa uhalali wa kuomba na kupata bila vizingiti vyovyote kwa sababu tumempenda Mwana, ambaye mwana na Baba ni kitu kimoja. “Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba,” Yoh 16:26-27.

Apolo aliyekuwa Myahudi kweli kweli, anaguswa na upendo huu wa Kristo, na anatoa ushuhuda kwa Wayahudi wenzake ambao hawakumkubali Kristo. Huku ni kumpenda Kristo bila kuona haya mbele za watu. Ni kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo. Hata hivyo hatutaweza kutoa ushuhuda wa kweli juu ya Kristo kama hatumfahamu Kristo. Apolo anamfahamu Kristo kwa kuyasoma maandiko Matakatifu na kuyaelewa. Huwezi ukatoa kile usichokuwa nacho. Kwanza ni lazima ukielewe kitu hicho ndio uwe na mamlaka la kukisema. Imani hukuzwa kwa hatua. Huwezi kukurupuka tu na kuanza kutoa ushuhuda, isipokuwa kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko,” Mdo 18:24. Mkristo mwenzangu inakupasa kuzijua na kuzipitia hatua hizi sita; kulisikia neno la Mungu, kulipokea neno la Mungu, kulisoma neno la Mungu, kulitafakari neno la Mungu, kulishirikisha neno la Mungu, na mwisho kutoa ushuhuda wa neno hilo kwa kuwa shahidi wa neno. Kwa kuanzia, jiwekee utaratibu kila siku wa kusome neno la Mungu. Ukishalisoma jiulize swali hili moja tu: Je, neno hili linasema nini juu ya Maisha yangu?

Kulinena neno na kuliishi kwa ujasiri kama tokeo la kuzipitia hatua hizo sita nilisozitaja hapo juu, hukuzwa pia na wenzetu waliokwisha ijua njia hiyo. Apolo anasaidiwa na Prisila na Akila. Lengo la ndugu hawa si kumdhoofisha Apolo, bali kumtaka awe makini zaidi kuhusu neno la Mungu. Huku ndiko kunakobeba maana halisi ya kushirikishana neno la Mungu. Ni kumfanya Apolo awe hodari zaidi. Ni kumwongezea maarifa ili afanye vizuri zaidi. Hapa tunajifunza pia unyenyekevu wa Apolo kukosolewa na kuwa msikivu. Ni mara chache sana wale ambao wanajiona wanajua na wakati mwingine kwa kuchukua vigezo vya kuwa na kundi kubwa nyuma yao, kuwa tayari kusikiliza ushauri. Apolo ni tofauti kabisa. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi,” Mdo 18:26. Mafanikio yetu katika maisha yasitutie upofu wa kujifunza zaidi.

Utayari wa Apolo kujifunza maarifa zaidi, unamwongezea ustadi wa kile alichokuwa anakijua awali. Kwa sababu hiyo, aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28. Ndugu yangu, tusichoke kujifunza mambo mapya na hasa pale unaposhauriwa kufanya hivyo na wenzako kwa sifa na Utukufu wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo,” Mdo 18:28


Tusali:-Ee Bwana Yesu Kristo, uwe njia na wokovu wangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario