miércoles, 25 de mayo de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 8 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo: 1Pet 4:7-13
Zab: 96:10, 11-12, 13
Injili: Mk 11:11-26
Nukuu:
Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala,” 1Pet 4:7 

 “Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina,” 1Pet 4:11

Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia,” Mk 11:13-14 

 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24 

Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu,” Mk 11:25 

Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mk 11:26 

TAFAKARI: “Mwaminini Mungu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya kutokukamilika kwetu kama wanadamu, Mungu ameweka ndani yetu uwezo wa kumtafuta na kumfikia kama tutamtafuta. Hali na uwezo huu ndani yetu ni namna ile tuliyoumbwa kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Hivyo kwa Imani na hali ya msukumo uliopo ndani yetu Mungu anapatikana tunapomtafuta. “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu baribu,” Isa 55:6. Ni kwa uwezo huu uliopo ndani yetu unatupa uwezekana wa kumrudia Mungu kwa sala na toba naye uturehemu. Mungu kamwe hapendi tuangamie katika uovu na ubaya wetu. Bado kuna nafasi ya kujenga tena mahusiano mazuri na nafsi yako mweyewe, na binadamu mwenzako, na  Mungu, na mazingira unayoishi. “Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Huruma ya Mungu ipo wazi muda wote. Ni mimi na wewe tu kuitafuta kwani haipo mbali.

Uwezo na hali hii iliyo ndani mwetu yenye kutuwezesha kufika pale alipo Mungu kama tutamtafuta, inakukata kila mara uwe zaidi ya kile ambacho kwa mazingira ya kawaida ungepaswa kuwa-“be productive and positive wherever and whenever you are.” Muono huu wa kuwa zaidi ya kile ulicho kwa sababu ndani yako upo uwezekano, ndicho kinachotokea kwa ule mtini ambao ulikuwa na majani ila haukuwa na tini kwa sababu haukuwa wakati wake. Yesu alijua fika kabisa si wakati wa tini, ila alienda kutazama kama tini zipo. Kwa mazingira ya kawaida mara chache msimu wa matunda fulani, upo uwezekano wa kuyapata yale yanayowahi kutoka kabla ya msimu husika kufikia. Ujio wa Yesu kwa watu wake, alitegemea kuwepo na muono chanya. Kwa maana nyingine alitegemea wawe na Imani hata kama mambo yote yalikuwa bado kufunuliwa kwao-wakati utakapotimia.

Adhabu iliyotolewa kwa mti ule wa mtini ni kielelezo kwa Wayahudi ambao hawakuwa na Imani juu ya ujio wa Mwana wa Mungu licha kwa mbali walitegemea mkombozi, na huu ndio ule uwepo wa majani yale ya mtini. Adhabu hii pia yanihusu mimi na wewe pale tunaposhindwa kuwa zaidi ya kile tulicho kwa sababu ndani yetu uwezekano ushawekwa kwa kuumbwa kwetu kwa sura na mfano wake Mungu. Yesu Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia,” Mk 11:13-14. Hii ndiyo nguvu inayosukuma imani yetu kwa sababu uwezo huo tushawekewa tayari.

Kuchukizwa huku kwa Yesu kutokana na uhaba huu wa Imani unajionyesha alipofika Hekaluni na kukuta ndivyo sivyo. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Mk 11:17. Kuifanya nyumba ya Mungu-“Hekalu kuwa pango la wanyang’anyi kuna tafsiri ya nyumba kama jengo, na nyumba kama mwili, yaani Hekalu la Roho Mtakatifu. Majengo haya yote (kama nyumba au mwili) katika tafsiri yake yapaswa kupewa stahili yake, yaani, “iliyotengwa kwa kazi ya Mungu tu: kusifu, kuabudu, kushukuru, kutolea sadaka. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu,” 1Kor 6:19-20. Ndugu yangu, Kristo kama kichwa na jiwe kuu la pembeni, sisi kwa Ubatizo wetu tumeunganishwa naye na kuwa Hekalu Takatifu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,” Efe 2:20-21. Hili ndilo Kanisa kama mwili wa Kristo, Kristo akiwa ndiye Kichwa nasi viungo vya mwili huo. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote,” Kol 1:18. Je, waamini hilo?

Baada ya kuona mtini ule umenyauka toka shinani, kwa mshtuko aliokuwa nao Petro, Yesu anamjibu, Mwaminini Mungu,” Mk 11:22. Alichokifanya Yesu ni kudhihirisha uwezo na nafasi yake na hasa kile alichokijia, yaani, kukuweka huru wewe na mimi kutoka utumwa wa dhambi. Huu ndio ukombozi wa kweli. Hivyo ukimwamini Mungu na huyu aliyetumwa na Mungu, yaani, Bwana wetu Yesu Kristo pasipo shaka mengi na ya ajabu yatatendeka kwako kwa jina lake. Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake,” Mk 11:23. Imani ujengwa na kuwa na nguvu katika maisha ya sala na kujiachia pasipo shaka. Ni kusali au kuomba ukijua ushakipata tayari hata kama kwa wakati ule bado. Hii ndiyo hali ya kuwa zaidi ya kile ulicho. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu,” Mk 11:24. Tatizo kubwa langu na lako tunaomba tukiwa na mashaka kama kweli Mungu anaweza kutupatia kile tuombacho kutokana na mazingira tuliyo nayo. Tusimwendee Mungu kwa majaribio. “Maana mawazo yangu si mawazo yetu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana,” Isa 55:8. Mungu wetu hajaribiwi kwa sababu ukamilifu ni asili yake.

Ila tusalipo yatupasa tusiwa katika hali ya hatia. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu,” Mk 11:25. Mfano: Tusalipo sala ya ‘Baba Yetu,’ sharti la kuipata huruma ya Mungu na msamaha wake, ni wewe kwanza kuwa tayari kusamehe. Hii ndiyo maana ya maneno haya; “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24. Mungu aliye mkamilifu na Mtakatifu hafananishwi na uchafu. Tuyasuluhishe kwanza mapungufu yetu nipo tumjongee katika sala na maombi. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu,” Mk 11:26. Je, bado umewekeza katika kutokusamehe? Mradi huo hautakuwa na faida zaidi ya hasara, tena kubwa ajabu.

Wapendwa wana wa Mungu, yeyote yule anayewekeza katika kusamehe anajua kuishi katika malengo na kuyaona maisha katika mtazamo wa kimungu, yaani, maisha kama jaribu, dhamana, na jukumu la muda mfupi. Maisha kama jukumu la muda mfupi ni kutambua kwamba, mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala,” 1Pet 4:7. Tunda la sala zetu liimarishe upendo kati yetu. Na kupendana kwetu kutuzamishe zaidi katika sala. Na penye sala na upendo wa kweli dhambi haina nafasi. Hivyo, Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi,” 1Pet 4:8. Sala na upendo wa kweli utukuza kimwili na kiroho na kwa namna hiyo hiyo tunawezeshwa kuvifahamu vipaji na karama zetu Mungu alizotujalia kwa ajili yetu na jumuiya ile tunayoishi. Ndugu yangu, kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu,” 1Pet 4:10. Mungu hakukupa kamara uliyonayo kwa kujifaidisha nafsi yako. Mungu amekupa karama hiyo akiwa na kusudi la huduma na kukamilishana ili kuwa na umoja katika utofauti ambao ndio Utukufu na uzuri wa Mungu. 

Wapendwa katika Kristo, uwezo huu Mungu aliouweka ndani yetu, “kumtafuta na kumfikia,” licha ya hali yetu ya kutokukamilika kama wanadamu, ndiyo inayotuweka karibu zaidi na Mungu. Hivyo, Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina,” 1Pet 4:11. Ndugu yangu, wewe si bahati mbaya na kamwe usijidharau.

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala,” 1Pet 4:7


Tusali:-Ee Bwana wangu Yesu Kristo, nikumbushe kila siku niamkapo kwamba muda wangu wa kuishi hapa duniani unakwisha, hivyo niwe zaidi ya kile kilichokuwa jana. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario