JUMANNE
WIKI YA 7 YA PASAKA
Somo:
Mdo 20:17-27
Zab:
68:10-11, 20-21
Injili:
Yoh 17:1-11a
Nukuu:
“Basi
sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni,
nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa
Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki
vyaningoja,” Mdo 20:22-23
“Lakini
siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo
wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya
neema ya Mungu,” Mdo 20:24
“Kwa
maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu,” Mdo 20:27
“Na
uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo,”
Yoh 17:3
“Mimi
nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio
wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10
“Wala
mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako,” Yoh
17:11a
TAFAKARI: “Uzima wa milele ndio huu; kumjua
Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu
hapa duniani kaitwa kwa namna mbalimbali na ya pekee kadiri iliyompendeza
Mungu. Kuitwa huku na Mungu kwa itaji mwitikio wetu. Hivyo kila mmoja wetu
anavyoitikia bila kujibakiza ndivyo anavyojazwa uzima huo wa milele ambao ni
tayari katika hatua, na ambao bado katika utumilifu wake. Hapa haijalishi
mwitikio huo umechukua taswira gani. Kwa maana nyingine haijalishi wewe ni
mlei, matawa, au mkleri. Hivyo basi, mwitikio huu lazima ulenge kumjua Mungu wa
pekee wa kweli, na Yesu Kristo.
Ni katika mwitikio huo kimaisha Mtume Paulo hajuutii
kumjua na kumtumikia Mungu aliye hai, na Yesu Kristo. Hivyo Mtume Paulo yupo
tayari kwa yote na lolote litakalotokea kuhusu maisha yake na uhusiano wake na
Mungu. “Basi
sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni,
nisiyajue mambo yatakayonikuta huko; isipokuwa
Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki
vyaningoja,” Mdo 20:22-23. Kwa maneno haya ya Paulo Mtume tunakumbushwa
kusimama imara hasa nyakati zile za sintofahamu katika maisha yetu kila mmoja
kadiri ya wito na nafasi yake.
Mtume Paulo anajua wazi
maamuzi yake aliyoyachukua katika maisha msingi wake ni Kristo mwenyewe, na
hajuutii uamuzi wake huo. Siri yake ni kwamba, tunapojitoa kwake Kristo bila
kujibakiza tunauhakika wa uzima wa milele, na safari yetu kuelekea katika
utumilifu huo wa maisha ya umilele ni safari salama na yauhakika. Hivyo, “siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani
kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu,
kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu,” Mdo 20:24. Je, wewe na mimi tunao
ujasiri huu na kuyatamka maneno mazito haya ya uzima katikati ya kiza kinene
cha sintofahamu ya maisha kama Mtume Paulo? Kwetu kama wafuasi hai wa Kristo ni
changamoto kubwa!
Wapendwa wana wa Mungu,
tufanyapo maamuzi haya katika maisha licha ya magumu tunayokumbana nayo,
tunajua mbele yetu yupo Jemedari Mkuu Yesu Kristo aliyeyashinda yote, na
asiyeshindwa kwa lolote. Mateso na magumu tunayokutakana nayo katika maisha
Kristo anayajua, na ndiye yeye atakayetutoa kwenye mikwamo hiyo kiimani endapo
tutaweka matumaini yetu yote kwake kama mweza wa vyote. Katika ukweli huu Yesu achoki
kutuombea na kutujaza neema na baraka akisema, “Mimi
nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio
wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao,” Yoh 17:9-10. Je, kwa nini Yesu
hauombei ulimwengu? Ulimwengu huu ni kama tanuru la kufulia chuma. Kupata chuma
bora na imara lazima kipite kwenye moto mkali sana. Nasi katika kuyashinda
mateso haya hapa duniani ndivyo tunavyojiimarisha katika imani na kunyakua taji
ile tuliyoandaliwa. Kwa hiyo ulimwengu kama ulivyo ni sehemu ya kukomaza Imani
yetu na kukua Kiroho na kimwili.
Ndugu yangu, Je, mateso
na maisha yako kwa ujumla yana mwelekeo huo wa uzima wa milele, yaani, kumjua
Mungu wa kweli na Yesu Kristo?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Lakini
siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo
wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya
neema ya Mungu,” Mdo 20:24
Tusali:-Ee
Mungu, niwezeshe kusimama imara kiimani ili maisha yangu yalenge kukujua Wewe
Mungu wa kweli na Yesu Kristo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario