IJUMAA
WIKI YA 7 YA MWAKA-C
Somo:
Yak 5:9-12
Zab:
103:1-2, 3-4, 8-9, 11-12
Injili:
Mk 10:1-12
Nukuu:
“Ndugu,
msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya
milango,” Yak 5:9
“Lakini
zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa
kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo,
msije mkaangukia hukumu,” Yak 5:12
“Lakini
tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke,” Mk 10:6
“Kwa
sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili
watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja,” Mk 10:7-8
“Basi
alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe,” Mk 10:9
“Akawaambia,
Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini,” Mk 10:11-12
TAFAKARI:
“Tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.”
Wapendwa wana wa Mungu,
hakuna hata mmoja kati yetu ambaye yupo katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya. Ni
kwa maana hiyo hiyo kwamba hakuna kati yetu aliyejipangia kuwa kama alivyo;
kijinsia, kuchagua azaliwe na wazazi wa aina gani, kabila gani, au taifa gani.
Tupo kama tulivyo kwa makusudi yake Mungu kwa sababu anampango mzuri na kila
mmoja wetu. Je, una sababu yoyote ya kumlaumu Mungu au kumkosoa Mungu kwa kile
ulicho? Angalizo: “Ndugu, msinung'unikiane,
msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango,” Yak 5:9. Leo
kutokana na matumizi mabaya ya neno ‘uhuru,’ tumefikia
hatua ya kukosoa kila kitu ambacho kimsingi ni kwenda kinyume kabisa na kusudio
la uumbaji wetu.
Kwa mfano swala la jinsia Maandiko Matakatifu
yanatufundisha kwamba, “tangu
mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke,” Mk 10:6. Leo walio wanaume wanataka kuwa wanawake na walio
wanawake wanataka kuwa wanaume kwa kisingizio cha kutumia uhuru wao. Baadhi ya
nchi za ulaya wazazi hawana tena mamlaka ya kuamua juu ya watoto wao. Mtoto
akifikia umri ufaao kisheria ujiamulia jinsia aipendayo. Je, tunaenda kinyume
na mpango wa Mungu? Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Mungu
akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba,” Mwa 1:27. Hii ghiliba na kasumba ya kujibadili na kuwa kitu kingine
inatoka wapi? Kwa nini tunashindwa kujipokea?
Kumkosoa
Mungu katika suala la uumbaji wake ni sawa na kuhasi na kuikataa ile ‘ndiyo’
iliyomo ndani mwetu. Ukosoaji huu utupelekea kuishi maisha yasiyo na malengo na
mwisho wa siku tunageuka kuwa vituko.
“Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa
mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe
ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu,” Yak 5:12. Je,
unayekwenda kinyume na matakwa ya Mungu ndiyo yako ipo wapi?
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa upendo wake juu yetu Mungu hakuishia tu kumuumba Adamu, bali aliona inafaa
Adamu akawa na mwenza wake na kuifanya familia kama shina na msingi wa maisha
kumwelekea Yeye mwenyewe kama ulivyo ule Utatu Mtakatifu wa umoja
usiogawanyika, yaani, Mungu Mmoja na nafsi tatu; Baba, Mwana, na Roho
Mtakatifu. Tukirudi kwenye kusudi na hitaji la uwepo wa familia, ni kwa “sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye,
ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali
mwili mmoja,” Mk 10:7-8. Familia itatoka wapi kama tutafuata matamanio yetu na
tamaa zetu kwa kisingizio cha uhuru usio na mipaka?
Ndugu zangu, “alichokiunganisha Mungu, mwanadamu
asikitenganishe,” Mk 10:9. Leo mwanadamu amejitwalia mamlaka yasiyo yake na
kujaribu kuuvaa umungu ambao pamoja na umungu huo wa kijivika, kifo hakijaacha
kumwaibisha. Hata hivyo kwa kiburi chake mwanadamu huyu hapendi kujirudi na
kuwa kile kilicho kusudi la Mungu juu yake. Kusudi la Mungu la kumfanya mtu mme
na mtu mke kuwa kitu kimoja ni kuufunua upendo wake kwetu, mshikamano wake, na
ukaribu wake wetu usiokoma. Ni jukumu na wajibu wetu kuudhihirisha upendo huo
wa kweli kati yetu. Hilo “pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo
ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza
wenzenu,” Rum 12:9-10. Tunapokosa upendo huu na umoja huu na hasa katika
funganishi la Sakramenti ya Ndoa na kujishikamanisha na mwingine nje ya ndoa
husika, muonekano huo hauna jina lingine zaidi ya ‘uzinifu.’ Hivyo, “kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine
azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini,”
Mk 10:11-12. Ndugu yangu, ukubali mpango wa Mungu ndani yako. Mungu anasababu
kubwa ya kukuumba kama ulivyo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi
alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe,” Mk 10:9
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tufungamanishe siku zote na kusudi la Mungu katika maisha yetu.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario