martes, 24 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 8 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo: 1Pet 1:18-25
Zab: 148:12-13, 14-15, 19-20
Injili: Mk 10:32-45
Nukuu:
Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19

 “Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu,” 1Pet 1:25

 “Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40 

 “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45 

TAFAKARI: “Hamjui mnaloliomba.”

Wapendwa wana wa Mungu, matamanio yanayosukumwa na hali ya ubinafsi wetu mwisho wake hayana heri kwako wewe uyatamaniyo na wala kwa wale wanaokuzunguka. Kumbe leo na kwa namna ya pekee Injili, inatualika kutafakari kwa undani kuhusu yale tunayoyatamani au kuyapata. Ni vyema kujibu maswali yafuatayo kwa uelewa; Je, unafahamu vizuri unachokitamani? Je, wafahamu vizuri wajibu wa kile ukitamanicho? Nini  hasa lengo ya hicho ukitamanicho? Je, hicho ukitamanicho na baada ya kuwajibika kwako kwacho kitakupatia utakatifu na kuupata uzima ule wa milele?

Kwa kutokufahamu vizuri  kile wakitamanicho, wana wa Zebedayo, Yakobo na Yohana, wanajichagulia sehemu za kuketi, mmoja mkono wa kuume wa Yesu, na mwingine mkono wa kushoto wa Yesu, katika utukufu wake. Mitume hawa hawakuwa na muda wa kutafakari fumbo lile la kifo alilokuwa anawasimulia Bwana wetu Yesu Kristo, yaani,Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka,” Mk 10:33b-34. Walijitazama wenyewe na nafsi zao tu. Kutokana na tamaa hiyo, walikuwa tayari kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu aliyowauliza Yesu. Kwa vile walithibitisha kuwa wapo tayari kukinywea kikombe kila cha mateso, Yesu anawataka wazame zaidi kwa kile wakitamanicho kwa kuwaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40. Kumbe kukaa na Yesu katika Utukufu wake siyo swala la kujitwalia tu, au kupeana kwa kujuana au kwa urafiki kama tuonavyo katika malaka za kibinadamu, bali licha ya gharama zake, Mk 10:39b, ni swala la kuhesabiwa haki, Mk 10:40. 

Pamoja na ugumu huo, Yesu anatutaka tutofautishe namna yetu ya kutenda na kuishi ili tulenge fumbo lile la kifo chake cha Msalaba ambapo ndipo ulipotundikwa wokovu wetu na kumpatia Kristo Utukufu wake, nasi kuhesabiwa haki ya kuwa wana wa Mungu bila ya mastahili yetu binafsi. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Damu hii yenye thamani kubwa iwe chachu na kielelezo cha imani yetu na kumwamini Mungu. Ni kwa Damu hii ya Mwana-kondoo huyu aliye na hila, Yesu Kristo, ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu,” 1Pet 1:21. Hivyo tenda na ishi yetu isukumwe kwa kuthamini kukombolewa kwetu huku kuliko kwa thamani kubwa ajabu.

Kristo Yesu hali akijua hulka yetu wanadamu anatukumbusha kuepuka kutawala wengine kwa mabavu kama asemavyo, “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42. Kristo hataki hilo litokee kwa Mitume na wafuasi wake. Kinyume chake tutangulize mbele ‘kutumika vyema’ na siyo ‘kutumikiwa wala kuogopwa.’ Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45. Maana yake nini?

Wapendwa wana wa Mungu, Kristo anatutaka tuelewa kuwa utumishi ni kujitoa kwa watu kwa upendo na kuwapenda. Huwezi kuwatumikia watu vizuri kama huwapendi. Na ukifanya hivyo (kuwatumikia ukiwa huwapendi) basi nyuma yake kuna ubinafsi mkubwa na kujitazama wewe tu, familia yako, ndugu zako, marafiki zako, na mwisho kupoteza dhima nzima ya kutumika na umma. Hapa tunahitaji nidhamu ya hali ya juu na yenye kusukumwa na utii wa kweli. Hivyo, Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo,” 1Pet 1:22. Kupendana kwa moyo ni kumwona Kristo Yesu kwa wote unaotumika kwao. Hapa ndipo kule kutoa nafsi yako iwe fidia ya wengi, Mk 10:45b.

Pili, kuwa tayari kutumika kunatutaka kusahu uzamani wetu na mazoea yetu. Ni kuzaliwa mara ya pili kwa kuliishi neno la Mungu lenye uzima. Kuliishi neno la Mungu lenye uzima kwanza kabisa ni kuwa  tayari kuhusu neno hilo. Pili, ni kuwa na uwezo wa kusikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa shahidi wa neno hilo likiakisi maisha yako. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele,” 1Pet 1:23. Ndugu yangu, neno hili tunahubiriwa kila siku. Lifanye kuwa sehemu ya maisha yako kwa sababu, Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu,” 1Pet 1:25.

Tatu, kuwa tayari kutumika ni kuukubali utumishi kwanza ambao mwisho wa siku ndio utakao sadifu ukubwa ule kama kweli ndio unaoutamani. Hivyo, bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu,” Mk 10:43b. Pili, kuikubali hali ya utumwa kwa ajili ya wote. Hali hii ya utumwa ndiyo itakayotuweka kuwa wa kwanza au wa mwisho. Hivyo, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,” Mk 10:44. Ndugu yangu, huu ndio utumishi na kutumika kwa yeyote yule mwenye hofu ya Mungu. Na kama upo tayari kutumika na unamatamanio haya, omba hivyo  ukifahamu wajibu wa kile ukiombacho. La sivyo hutotumika vyema na mwisho wa siku ni kupoteza vyote: Utakatifu wako, na uzima ule wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari,” Mk 10:39b-40


Tusali:-Ee Yesu, tufundishe namna ya kuomba kile tukitamanicho tukiusahau ubinafsi wetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario